Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nami naungana na Waheshimiwa Wabunge wote wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri, kwanza kukupongeza sana kwa mwenendo na uongozi mzuri wa Bunge. Hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile nami nichukue nafasi hii kama Mbunge ambaye nimekuwepo hapa Bungeni muda mrefu, kuwapongeza sana Wabunge. Nadhani nichomekee kidogo, kwamba Wabunge na Bunge hili asilimia kubwa ni wa Chama cha Mapinduzi kwa kutekeleza wajibu wao vizuri wa kuisimamia Serikali. Kwa hiyo, kwa kweli nawapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu kwamba sisi ambao tuko kwenye front bench hapa, ni mawaziri ambao pia tunatokana na Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, tunawaahidi hatutawaangusha, tutayachukua yote tuyafanyie kazi na mwisho wa siku tunachotaka kwa kweli ni utendaji mzuri wa kazi za Serikali. Pia tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuliendeleza Taifa letu na juhudi hizo tunaziona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakwenda moja kwa moja kwenye maeneo kadhaa yaliyojitokeza kwenye hoja ya CAG na vilevile yamechangiwa na Wabunge. La kwanza ni malimbikizo ya muda mrefu ya haki na stahiki za watumishi wa Umma. Malimbikizo haya yamejigawa katika maeneo tofauti, nami nitazungumzia eneo ambalo liko ndani ya Ofisi ya Rais. Naomba Waheshimiwa Wabunge kwa pamoja tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa sababu alipoingia tu ndani ya madaraka kwenye Serikali hii ya Awamu ya Sita, kwenye eneo la malimbikizo ameshalipa malimbikizo ya mishahara (arrears) kwa watumishi 113,969 na tayari Shilingi bilioni 196,083 zimetumika. Kwa hiyo, kwa kweli eneo hilo amelifanyia kazi kwa kuzingatia ripoti ya CAG.

Mheshimiwa Spika, pia kwenye ripoti ya CAG kulikuwa na hoja ya madaraja ya Watumishi. Naomba nikuhakikishie, ndani ya muda mfupi Mheshimiwa Rais na Serikali yake kupitia ofisi hii tayari watumishi 262,008 wameshabadilishiwa muundo wa madaraja; na Serikali kwa sasa kila mwezi inatumia fedha za Kitanzania Shilingi bilioni 58,253 kila mwezi kwa ajili ya madaraja hayo mapya. Kwa hiyo, Mheshimwa Rais jambo hili amelizingatia.

Mheshimiwa Spika, imezungumzwa sana hapa ndani kwenye hoja ya CAG kwamba kuna tatizo la watumishi katika sekta mbalimbali. Unakumbuka tulishatoa taarifa hapa Bungeni kwamba Mheshimiwa Rais aliridhia kibali cha ajira 44,099 na kimeshatolewa na ajira zinaendelea kutolewa katika sekta mbalimbali. Pia tumeendelea kuagiza wale tuliowakasimia madaraka ya usimamizi wa rasilimali watu katika Serikali za Mitaa na hasa Regional Secretariat.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki kifupi Mheshimiwa Rais aliridhia kufanya recategorization kwa watumishi zaidi ya 25,000. Tumesema kwamba, tuna tatizo kweli la Watumishi ila haingii akilini kwenye Regional Secretariat tumewapa mamlaka ya kusimamia namna ya upangajia rasilimali watu katika maeneo yao; tuna eneo hili la recategorization ambalo Maafisa Rasilimali Watu wanaweza kulitumia vizuri sana; kwa mfano, kama unaona katika eneo lako labda una walimu wengi wa somo fulani waliozidi kwenye ikama, lakini una upungufu wa wataalamu katika eneo lingine, unao uwezo wa kuwachukua wale walimu na kuwasomesha wakaziba pengo la eneo ambalo halina watumishi wa kutosha. Kinachotakiwa kufanyika ni kuomba tu kibali cha recategorization. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tu niseme, tunaendelea ku-control wage bill. Hii wage bill tunakwenda nayo kwa kuangalia kile kilichopo katika mfuko wetu wa Serikali. Tukisema tuajiri kujaza mapengo yote, hatutaweza. Kwa hiyo, ni suala tu la kujiongeza tu kwa wale tuliowapa kazi ya kusimamia na kupanga rasilimali watu nchini. Pia tuna mfumo ambao sasa hivi unafanya Staff Auditing.

Mheshimiwa Spika, kwenye ule mfumo ukienda kuangalia unapata taswira ya aina ya watumishi jinsi walivyopangwa kila mkoa. Kwa mfano, Mheshimiwa Waziri wa Afya amekuja kuomba kibali, pale walipozidi tuwahamishe wapelekwe mahali ambapo hawapo. Kwa hiyo, kama tukishirikiana kwa pamoja na hasa kwenye Regional Secretariat, ninaamini kabisa kwa rasilimali watu ndogo tunaweza kufanya mambo makubwa. Kwa hiyo, ni wito wangu kwa kweli tufanye kazi hiyo kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni la mifumo. Waheshimiwa Wabunge na ripoti ya CAG ilisema hapa, bado kulikuwa na mianya ambayo iliruhusu kuendelea na watumishi ambao wamefariki lakini bado wanaonekana kwenye taarifa za watumishi ambazo tunazo. Kipindi hicho cha Ukaguzi wa CAG tulikuwa na mfumo wa LAWSON, lakini kuanzia mwaka 2021 mfumo wa LAWSON tumeachana nao. Sasa hivi tuna mfumo mpya wa taarifa za Watumishi na mishahara.

Mheshimiwa Spika, naomba niwahakikishie kwamba mfumo huu una uwezo wa kukagua taarifa za watumishi wote wa nchi nzima kila mwezi. Kila mwezi tuna uwezo wa ku-audit watumishi wote waliofariki, waliostaafu na ambao hawana sifa na kuwaondoa kupitia huo mfumo. Kwa hiyo, tunaamini huko tunakokwenda, kwa kuwa LAWSON sasa tumeiondoa na tuna mfumo mwingine mpya tunaoutumia, haya yaliyojitokeza wakati wa ripoti ya CAG tunaamini kabisa yatapungua kwa kiasi kikubwa na ikiwezekana yataisha kabisa.

Mheshimiwa Spika, pia tumegundua na hapa imejadiliwa sana, kuna tatizo la uwajibikaji kwa watumishi wetu na hasa hii mianya ambayo imekuwa ikitumika ya rushwa na ubadhirifu wa fedha. Ndani ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, tumeshakamilisha ujenzi wa mifumo miwili mipya. Mfumo ambao utachukua nafasi ya OPRAS ili kupima utendaji kazi wa mtumishi mmoja mmoja kila siku; kwa siku, kwa wiki mpaka kwa mwaka. Vilevile tumetengeneza mfumo mwingine ambao utapima utendaji kazi wa taasisi zote za Umma. Mfumo huu mpya wa kupima utendaji kazi wa taasisi za Umma, unatupelekea sasa kufuatilia zile key performance indicators zote katika kila taasisi, je, hao wanaopewa majukumu ya kusimamia utendaji kazi wa taasisi, wanazifikia?

Mheshimiwa Spika, kuna Mbunge alisema hapa kuhusu suala la kufanya naming and ashaming; kupitia mfumo huu, kila mwisho wa mwaka taasisi zitakazofanya vibaya zitaangukia kwenye utaratibu wetu wa naming and ashaming kwa wale ambao hawatafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu kwamba kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, baada ya muda mfupi tutakuja na mageuzi makubwa ya kimifumo na kiutendaji itakayomlazimisha kila mtumishi kuwajibika kwa hiari yake mwenyewe, kuondoa upendeleo na kutoa haki na stahiki kwa kila mtumishi kwa kuzingatia kazi anazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TAKUKURU tumewapa kazi ya kujikita…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, sekunde 30.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, tunakuja na mpango wa kitaifa wa kupambana na rushwa. TAKUKURU tumewapa kazi kubwa ya kuzuia, tunataka wazuie. mabilioni ya fedha yote kama tungeweza kuzuia ubadhirifu usitokee, nadhani tungekuwa tumefanya kazi nzuri sana. Kwa hiyo, mtazamo wetu sasa hivi ni kuzuia mianya yote ya ubadhirifu na rushwa ili angalau kila kidogo kinachopatikana katika Serikali yetu kifanyiwe kazi vizuri na kiweze kuchangia katika maendeleo ya Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, tunayo mengi, lakini nadhani tutaendelea kutafuta muda wa kuyatolea maelezo na ufafanuzi hapa ndani ya Bunge lako Tukufu. Tunaunga mkono hoja hizi na sisi ndani ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora tutashirikiana kuhakikisha maazimio yanafanyiwa kazi na mwisho wa siku ni maendeleo na ustawi wa Taifa letu kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)