Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kutoa mchango wangu kwenye taarifa hizi tatu ambazo zimewasilishwa na Wenyeviti wetu wa Kamati.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusema kwamba, hivi vitu wakati mwingine vinalitia simamzi sana Taifa letu. Mambo haya ya ubadhirifu ambayo yanaendelea kwenye Taifa letu ni kitu cha ajabu sana na kinakwenda kutukatisha tamaa Watanzania hata kwenda kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo huko chini.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa kawaida kule chini, akiiba kuku anakamatwa, anapelekwa Mahakamani, anasomewa shtaka, anahukumiwa. Leo Mtanzania aliyesoma kwa kodi za akina mama kule chini; wapika pombe, wakulima wanahangaika kutafuta mbolea kwa shida, kasomeshwa na kodi hizo, amepata nafasi ya kulitumikia Taifalake, anaenda kuweka ubinafsi wa hali ya juu kwa kuweka fedha zote kwenye mfuko wake na tumbo lake, na bado sisi kama Taifa tunamwangalia, hatujitendei haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaomba nizungumzie mchango wangu kwenye suala zima la tozo zinazotozwa kwa ucheleweshaji wa malipo ya Wakandarasi kwenye miradi mbalimbali ya Serikali. Tunafahamu fika kwamba Serikali huwa inaandaa bajeti; wataalam wetu huko wanatuandalia bajeti, wanatuletea ndani ya Bunge ili tuweze kuijadili bajeti na tuweze kuona kwamba, kutokana na mradi fulani bajeti tuliyoletewa inakidhi mahitaji? Kama haikidhi tuishauri Serikali kuongeza ama kama inakidhi na kubaki, tushaurI Serikali na kupunguza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kinachonishangaza, kama Serikali huwa inaleta bajeti, tunajadili hapa, nao wanatuhakikishia kwamba itakwenda kukidhi mahitaji ya kukamilisha mradi, badala yake mradi ule haukamiliki. Mbaya zaidi, miradi hiyo, wao ndio wanaoenda kuingia mikataba na Wakandarasi. Kwenye mikataba hiyo kuna kipengele ambacho kinasema, ukichelewa kumlipa Mkandarasi utatakiwa kumlipa faini ya kumcheleweshea fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha kwenye miradi mbalimbali imeendelea kucheleweshwa kutolewa kwa Wakandarasi wetu wanaotekeleza miradi mbalimbali. Nitasema baadhi ya miradi hapa. Inapocheleweshwa, tukitozwa zile tozo tunakimbilia kwenda kulipa zile faini, tunaacha kwenda kuhangaika kupeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi hapa tukisema kuna dili linalochezwa baina ya mlipaji na mlipwaji tutakuwa tunakosea? Miradi haipelekewi fedha, haikamili, tunaletewa tozo ya kulipa kwa ajili ya ucheleweshaji wa malipo, tunakimbiila kwenda kulipa hiyo tozo. Kwangu binafsi naona kwamba kuna mchezo ambao tunachezewa na wataalamu wetu ndani ya Serikali wa kuchelewesha kwa makusudi kabisa; kwa sababu sisi kama Bunge, bajeti tunakuwa tumeshawapitishia. Kwa hiyo wanafanya makusudi wasipeleke zile pesa za utekelezaji wa miradi ili waweze kupata channel ya kwenda kupiga fedha kwenye tozo kule.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe mifano michache kwenye suala zima la ucheleweshaji wa ulipaji wa Wakandarasi, tozo ambazo tumetozwa. Daraja la Kigongo - Busisi kwa taarifa ya CAG tumetozwa faini ya Shilingi bilioni 1.5 kwa kuchelewesha kumlipa Mkandarasi. SGR halikadhalika, tumetozwa faini ya Shilingi bilioni 8.9. Yaani hizi tozo zote tunatozwa. Sisi tunahangaika huku hatuna mbolea; hatuna watumishi maana hatuwezi kuwalipa mishahara, tumeshindwa kuajiri; hatuna maji leo, tunashindwa kuchimba visima, hata kuleta maji kutoka Ziwa Victoria tu yafike hapa Dodoma; watu tunakuwa na foleni ya migao ya maji, lakini kuna watu, washikaji wako hapa wanapiga hela, wamekaa kimya na tunawaangalia, wala hatuna shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukija kwenye upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, kwa kuchelewesha tu kuwalipa fidia wananchi waliokuwa wanapisha ule mradi, zaidi ya kaya 1,125 tumelipa zaidi ya Shilingi bilioni 22 kwa Mkandarasi. Hivi vitu ni kwa nini nchi hii? Ni kwa nini Tanzania yetu hii? Halafu tunatoka tunaenda kuhangaika nje huko, wakati tuna hela ziko hapa, watu wanazichezea pasipo kuwa na sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukija Mamlaka ya Ndege halikadhalika tumepigwa faini ya Shilingi bilioni 11.3. Hizi fedha ukizijumlisha hapa nyingi ambazo zingetusaidia kama Taifa kuondoa changamoto mbalimbali tulizonazo ndani ya Taifa letu na tukaishi maisha ya kutokwenda kuhangaika barabarani huko kuombaomba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali na Mawaziri wanaosimamia baadhi ya Sekta. Mwaka 2021 tulipitisha tozo, Watanzania wakati wanalalamika kuhusiana na suala la tozo kuna watu walijitokeza wakasema kama hawawezi kulipa hizo tozo, wahamie Burundi, sijui wahamie wapi? Ila kuna watu wako humu wanapiga hizi fedha, hatushughuliki nao, wala hatuwajibu majibu ya namna hiyo. Hivi nikisema kwamba tunakula nao, nitakuwa na shida gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mtanzania wa chini kule anajihangaikia mwenyewe, tunahangaika naye, tunamkamua mpaka dakika ya mwisho, mpaka tone lake la mwisho la damu, halafu kuna watu fulani tu hapa wapo, wala hawana shida, wanakula bata, wanaendesha magari mazuri wakati kuna mama zetu huko vijijini wanatembea kwa miguu zaidi ya kilometa 20 mpaka 30 kwenda kutafuta maji. Watoto wetu wa kike leo kwa kushindwa kuwasogezea shule karibu, wanatembea umbali mrefu kwenda kutafuta shule, wanabakwa, wanapata mimba za utotoni, wanapata maradhi, tuko hapa, watu wanapiga hela, tunawapigia makofi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Bunge hili leo likafanye maamuzi yatakayoleta maslahi mapana ndani ya Taifa letu kwa kuokoa fedha zinazokwenda kuteketea kwenye maeneo ambayo hayana sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie pia suala la fedha za maendeleo, asilimia 40 kwa halmashauri ambazo zina mapato ya chini na asilimia 60 kwa halmashauri ambazo zina mapato makubwa. Fedha hizi nazo zimekuwa kizungumkuti. Leo fedha zinazotumika kukamilisha miradi ya maendeleo kwenye majimbo yetu ni fedha ya Mfuko wa Jimbo, fedha ya Mbunge. Lakini fedha ya makusanyo ya ndani kwenye halmashauri, Wakurugenzi wetu wamekuwa hawapeleki kwenda kukamilisha miradi mbalimbali ambayo wananchi wanajitolea kule chini. Hivi vitu navyo siyo vya kuvifumbia macho. Naomba tuchukue hatua stahiki kwa wale watu ambao mapato yao yanawaruhusu kwa mujibu wa sheria kuchukua fedha ya asilimia 40 kwenda kumalizia miradi mbalimbali inayotekelezwa na wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, naomba nilisemee suala la mbolea. Namshukuru Mheshimiwa Waziri ametoa ufafanuzi hapa. Pamoja na ufafanuzi alioutoa Mheshimiwa Waziri kwamba hawawezi kuifikisha mbolea kwa wananchi wetu kule chini, wameiweka hapa mjini; hivi mjini hapa ndiyo kuna wakulima? Jana wakati naangalia taarifa ya habari, kuna mwananchi mmoja Songea amefariki akiwa kwenye foleni anasubiri mbolea. Kapanga foleni, ameanguka chini, amekufa pale kutokana na msongamano wa kwenda kutafuta mbolea. Ametoka huko kijijini kwao, ni mbali, amefika pale, foleni ni kubwa.

Mheshimiwa Spika, sasa tunachomwomba Mheshimiwa Waziri, hao Mawakala wake ambao amewapa hiyo kazi ya kusambaza mbolea, mbolea hii isikae Makao Makuu ya Wilaya ama kwenye hivyo vituo. Tuwapelekee wananchi wetu, tuwasogezee angalau kwenye Makao Makuu ya Kata ambapo kwanza tutapunguza msongamano mkubwa; pili, tutawasaidia wananchi kutembea umbali mdogo kuja kufuata hiyo mbolea kwenye hayo maeneo. (Makofi)

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Kunti Majala, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Hussein Amar.

T A A R I F A

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, nimpe taarifa Mheshimiwa Majala. Kufariki kwa yule mwananchi akiwa kwenye foleni akisubiri mbolea, hiyo ni ahadi ya Mwenyezi Mungu, na siyo sababu ya mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Kunti Majala, unapokea taarifa hiyo?

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, namheshimu sana Mzee Hussein, sana, sana. Huyu mtu ingekuwa ni ahadi yake, angefia huko nyumbani kwake. Hata kama alikuwa na maradhi yake, laiti ile foleni isingekuwepo na ule msongamano; na tunafahamu Watanzania wengi kwenye suala la afya pia sio watu ambao tuna utamaduni wa kwenda ku-check afya zetu. Yule mtu hata kama alikuwa na maradhi yake na kwamba ahadi yake imefika, lakini katika yale mazingira, chanzo kilichoripotiwa ni mkulima kufariki kwenye foleni ya kutafuta pembejeo, kwa maana ya mbolea na siyo kitu kingine chochote. Kwa hiyo, kama ilikuwa ni ahadi ama haikuwa ahadi, kafia kwenye foleni ya kutafuta pembejeo. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Kama unamtetea mwanao, well and good, siyo mbaya.

SPIKA: Mheshimiwa Kunti Majala, kuna taarifa nyingine kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Godwin Mollel.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nilitaka tu kumpa mwenzangu taarifa. Kwanza nimpongeze kwa mchango wake mzuri wenye input nzuri sana. Ila kwa anachokizungumzia, kwa sababu tunazungumza kwenye Bunge na huwa sababu za vifo haviamuliwi na magazeti, mtu unaweza ukafa ukitembea, unaweza ukafa ukifanya chochote, lakini sababu iliyopelekea kifo ni clinical. Kwa hiyo, namwomba, inawezekana anataka kuonesha uzito wa jambo analolisema, lakini sababu ya kifo haiwezi kuwa kukaa kwenye foleni.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Kunti Majala, unapokea taarifa hiyo.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, naomba Wabunge, hatuna sababu za kuanza kuvutana, ila mtu amekufa akiwa kwenye foleni ya kusubiri mbolea. (Makofi)

(Hapa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Alisimama)

SPIKA: Mheshimiwa Kunti Majala, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesimama.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kanuni ya 71(1)(a) Wabunge hatupaswi kutoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli.

SPIKA: Mwanasheria Mkuu wa Serikali, taarifa gani haina ukweli? (Kicheko/Makofi)

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya kifo; kifo cha binadamu huthibitishwa na daktari na vile ville kifo cha mashaka kimetolewa mwongozo kwenye kifungu cha 7 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai. Kwa hiyo, mchango wake inawezekana yeye ana taarifa ambazo ni za upande mmoja, lakini mwenye kuthibitisha cause of death kwa mujibu wa postmortem examination report Kifungu cha 8 huwa inatajwa pale. Kama haijatajwa haiwezi ikawa taarifa ambayo inakuwa classified kuweza kutolewa kwenye mamlaka na kufanyiwa kazi.

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, amesimama Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akatupeleka kwenye Kanuni ya 71 fasili ya (1) ambayo inazungumzia mambo yasiyoruhusiwa Bungeni. Pia ametupeleka kwenye mchango wa Mheshimiwa Kunti Yusuph Majala ambapo wakati akichangia alikuwa anaeleza namna ambavyo kuna changamoto kwenye jamii kwa maana ya upatikanaji wa huduma kwa sababu ya taarifa ambazo zipo za CAG na namna ambavyo kuna upotevu wa mapato ambayo yangeweza kusaidia kwenye hayo maeneo mengine. (Makofi)

Sasa hapa jambo ambalo halibishaniwi ni kwamba mtu ni kweli amefariki; na huyo mtu amefariki akiwa kwenye eneo ambalo linatolewa mbolea. Ikiwa hilo siyo linalobishaniwa, kwa sababu mimi katika kusikiliza; maana la sivyo itabidi niitishe Taarifa Rasmi za Bunge; sijasikia kama anasema kilichosababisha kifo ni foleni ya mbolea. Anachoeleza ni eneo alilofia huyo Mtanzania. Ni kwamba eneo alilofia ni eneo la kusubiri mbolea. (Makofi)

Sasa kama kuna taarifa yoyote, pengine kama huyo mtu hajafa, moja; la pili, kama amekufa na hajafia pale ambapo mbolea inatolewa, labda hilo ndilo linaweza kubishaniwa. Ila kwa maana ya kwamba mtu amefariki na amefariki sehemu ambayo mbolea inatolewa, hiyo siyo sababu ya kifo, lakini ni kwamba amefia pale. Eneo ambalo amefia ni la kusubiri mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Kunti Majala, kwa sababu hapa nilikuwa sijaombwa mwongozo, ndiyo maana hamjasikia nikisema mwongozo, lakini ilikuwa inatolewa taarifa ili mchangiaji apokee taarifa vizuri. Kwa hiyo, lazima niliongoze vizuri ili hiyo taarifa iwe imetolewa kwa namna inayostahili. (Makofi)

Kwa hiyo Mheshimiwa Kunti Majala, kwa sababu sijaitisha Taarifa Rasmi za Bunge hapa, mimi ndivyo nilivyosikia. Ila kama umesema kwamba yule mtu amefariki kwa sababu ya kusubiri mbolea, nadhani hata gazeti litakuwa halijaandika sababu ya kifo, ila limeandika eneo ambalo huyo mtu amefia.

Mheshimiwa Kunti Majala, endelea na mchango wako.

MHE. KUNTI MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kutoa huo ufafanuzi vizuri na naamini ulinisikia vizuri na umenielewa vizuri. Wabunge ni lazima tuwe watu ambao tunasikiliza na kutafakari ili tuweze kuchukua maamuzi. Hizi biashara za kuwa tunateteatetea na kujizingazinga na kutaka kufichaficha vitu, unaficha kitu gani wakati kitu kiko hadharani? Ndio maana tunaendelea kuibiwa humu ndani ya Taifa letu kwa sababu ya kubebanabebana kusikokuwa na tija na kuteteanateteana kusikokuwa na tija.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa nafasi uliyonipa na naomba niishie hapo kwa mchango maana yake naweza nikaendelea kuharibu hali ya hewa aaidi. (Makofi/Kicheko)