Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nianze kwa kukushukuru wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi ya kuzungumza ndani ya Bunge hili Tukufu. Ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kunipa uhai. Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na ninampongeza sana kwa kazi kubwa anayoifanya.

Mheshimiwa Spika, nimewahi kusema huko nyuma kwamba mwanadamu hupimwa kwa matendo yake, narudia tena kusema leo ya kwamba Tanzania ina Rais smart, Rais intelligent na Rais mwenye uwezo mkubwa sana wa kufanya kazi. Ushahidi wa jambo hili ni kwamba alichukua nchi hii ikiwa inakua kwa asilimia 2.2. Leo ninavyozungumza Tanzania inakua kwa asilimia 4.5, inaelekea Tano. Alichukua nchi hii ikiwa imeanza kupunguziwa misaada ya wahisani kwa sababu ilikuwa imeshatambuliwa kama nchi ya uchumi wa kati, wahisani walikuwa wanaondoa misaada kwa kuona kama vile mtoto sasa amekuwa anaweza kujitegemea. Alichukua nchi ikiwa kwenye ugumu wa uchumi lakini ameweza kudhibiti mfumuko wa bei.

Mheshimiwa Spika, ninavyozungumza hapa leo unaweza kusema kwamba Tanzania ina bei mbaya ya bidhaa. Lakini wacha nikupe record kidogo. Mfumuko wa bei nchini Sudan ni asilimia 285; mfumuko wa bei Nchini Kenya ni asilimia 6.7; mfumuko wa bei Nchini Uganda ni asilimia 7; mfumuko wa bei Tanzania ni asilimia 4.4. Tanzania ni nchi yenye lowest inflation katika nchi za Afrika Mashariki. Naomba tumpongeze sana Rais wetu kwa sababu anatupeleka vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, asubuhi ya leo nilikuwa napiga hesabu ya saa ambazo Mheshimiwa Rais amekwenda nje ya nchi kuitafutia Tanzania riziki. Amesafiri nje ya nchi saa 263, hivi ninavyoongea, Rais wangu yuko China anatafuta riziki kwa ajili ya watu wake. Kwa wanaosafiri kwa ndege wanaelewa maana ya saa 263. Tunastahili kumpongeza sana Rais wetu, mimi binafsi niseme jukumu langu la kwanza litakuwa ni kumlinda na kumtetea Rais wa nchi yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme – na Mungu anisaidie – niseme yale ambayo naamini Mungu ametaka niseme. Nchi yangu inaumwa. Tulipoitwa na Rais Ikulu wakati ule nilisema Tanzania inaumwa widespread Institutional failure; mtakumbuka. Taasisi zimefeli. Nataka niseme leo ya kwamba Tanzania nchi yangu inaumwa magonjwa makubwa mawili; ugonjwa wa kwanza ni anemia ya integrity; ugonjwa wa pili ni anemia ya accountability. Tanzania inaumwa ukosefu wa uadilifu na pili ni ukosefu wa uwajibikaji. Magonjwa haya ndiyo yamesababisha tatizo tulilonalo leo la widespread institutional failure.

Mheshimiwa Spika, tangu nimekuwa Mbunge nikiingia hapa ndani ripoti ya CAG ikija ni watu wameiba. Nilizungumza hapa mara ya mwisho nikasema na iko siku mtakuja kukubaliana na mimi ya kwamba iko sababu kubwa sana ya kuanzisha taasisi ya monitoring and evaluation. Mheshimiwa Engineer Ulenge huwa anazungumzia suala hili sana, na mimi ninataka kusisitiza, watu wanaiba. Sasa siyo kwamba hatuna watu waaminifu, wapo! Lakini katika asilimia kubwa ya watu wetu uadilifu na uwajibikaji umemomonyoka sana.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi katika Taifa hili niseme bila kupindisha maneno, tumefika mahali inaanza kuaminika kwamba mtu asipokuwa mwadilifu ni hero. Tanzania mtu asipokuwa mwadilifu ameanza kutafsirika kama hero. Kwamba alikuwa Mtumishi wa Umma akajenga ghorofa Nane, akanunua mashamba makubwa, sasa ameacha kazi anaonekana alikuwa smart, na watoto wake wanasema Baba yetu alikuwa Kiongozi, alikuwa very smart. Kumbe mwizi! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yule aliyekuwa mwaminifu sana kwa Taifa lake, akaitumikia Tanzania kwa akili yake yote, kwa uaminifu, akaondoka kazini maskini, wakati mwingine amemwagiwa tindikali kwa sababu alikuwa TRA hataki kupokea rushwa, leo hii anateseka wanasema Baba yetu alikuwa Serikalini lakini alikuwa mjinga. Hatuwezi kuwa na Taifa ambalo wezi wanaonekana heroes. Hatuwezi! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nipongeze sana Bunge leo, tangu nimeingia hapa ndani Bunge la safari hii nimefurahi sana. Natamani Bunge hili liendelee kama lilivyo hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakumbuka huko nyuma nilikuwa nawaambia kuna na Bunge la Speed and Standards. Natamani Bunge hili liwe la Quality and Perfection, chini ya uongozi wako ujipatie sifa ya kuwa na Bunge la 12 la Quality na Perfection ambalo tunakuja hapa kusimamia mambo bila hofu wala woga, tumsaidie Rais wetu aweze kuongoza Taifa letu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima tutibu tatizo la integrity na uwajibikaji ndiyo maana tuko hapa, ndiyo maana tumeaminiwa na Watanzania wote tuje hapa tutibu tatizo hili. Taasisi za dini BAKWATA, Episcopal Conference na CCT, walim-hire marehemu Prof. Ngowi ili afanye utafiti kuonesha ni kiasi gani cha pesa kinapotea kila mwaka, ripoti hiyo nimeisoma ina kurasa 64.

Mheshimiwa Spika, Tanzania inapoteza karibu Dola Bilioni Moja kila mwaka kwenye mapato yake kwenye mikono na mifuko ya watu wasiokuwa waaminifu. Lazima tuzuie mambo ya namna hii. Sitaki kupita kwenye details za kwamba ripoti ikoje, yameshasemwa yote hapa, kila mtu anasema ni madudu, ni wizi na wizi zaidi.

Mheshimiwa Spika, nami naungana na wote waliozunguma. Nilimsikia Kaka yangu Mheshimiwa Tarimba akiongea jana kwa uchungu, nikamsikia Dada yangu Mheshimiwa Kapinga anaongea kwa uchungu; na wote wameongea kwa uchungu kwamba tunaibiwa. Nasi kazi yetu kama Wabunge ni kuisimamia Serikali yetu tuzuie fedha zisiibiwe ili ziende kwenye huduma za jamii yetu.

Mheshimiwa Spika, wewe ni Mwanasheria unafahamu Katiba yetu imetamka na mimi nitanukuu Katiba ilivyotamka. Katiba imesema: “We, The People of The United Republic of Tanzania, do sovereignly agree that we are going to build a country under the principles of freedom, justice, fraternity and concord.” Tumekubaliana kujenga Taifa ambalo litajengwa chini ya uhuru, haki, udugu na amani.

Mheshimiwa Spika, tukizungumzia haki, haki ya Watanzania kupata huduma za afya, haki ya Watanzania kupata elimu, haki ya Watanzania kupata maji. Hatuwezi kutimiza haki hii kama watu wanaiba kiasi hiki. Ni lazima tuzuie wizi, na tunaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa maslahi ya muda niseme nini kifanyike. Jambo la kwanza, kuna kitabu kimoja aliandika Jack Welch ambaye anaaminika kama the number one General Manager in the world, aliandika kitabu kinaitwa ‘‘Straight from the Gut’’, akasema kuna njia mbili za kuongoza watu, njia ya kwanza ni persuasion (kuwasihi) ili waweze kwenda na wewe au compassion kuwalazimisha waende. Watanzania kwa kuwasihi hawawezekani, tuwalazimishe kuwa waadilifu, walazimishwe kuwa waadilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, moja, tupandikize uadilifu kwenye mioyo ya watoto wetu. Watoto wetu wasione kwamba wezi ndiyo mashujaa wa Taifa letu, ifanyike kwenye mitaala yetu, wazazi nyumbani watimize wajibu wa kuongea na watoto wao ili ionekane ya kwamba uzalendo, uadilifu kiwe kitu cha kwanza kwa kila mtoto wa nchi hii. Hilo likiingia ndani ya mioyo ya watoto wetu nakuhakikishia tutajenga Taifa la watu ambao watalipeleka mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, tukimalizana na watoto, sisi watu wazima tulioshindikana – rafiki yangu, Mheshimiwa Dkt. Ntara, amenipa maneno hapa, yanasema hivi: Waarabu wanao msemo unasema: ‘Yamshillah Jabari illah jadhaa’ ikiwa na maana kwamba punda haendi bila bakora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ingekuwa ni maamuzi yangu Shigongo ningetangaza tuwe na siku ya uchapaji bakora Kitaifa. Fimbo zitoke Mbeya, wachapaji watoke Tarime halafu tukutane Uwanja wa Jamhuri siku ya uchapaji bakora Kitaifa. Unakuja pale na mke wako na watoto wako kama siku ile ulipokuwa unaapishwa, halafu unatajwa, Hamisi Taletale, unakwenda mbele, unachapwa, ili tujenge jamii ya watu wanaoogopa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hatutaki kuwachapa watu wetu, tumepitisha Sheria Tano katika Bunge hili, sheria ya kwanza ni Sheria ya TAKUKURU; Pili, Sheria ya Fedha; Tatu, Sheria ya Manunuzi; Nne, ni Sheria ya Utakatishaji Fedha na Sheria ya Tano ni Sheria ya Uhujumu Uchumu. Bunge hili limepitisha sheria hizo zisimamiwe! Kuwe na law enforcement. Changamoto yetu ni law enforcement. Tunayo sheria nzuri lakini hatuzisimamii. Kuna watu wanaishi uraiani walitakiwa kuwa jela leo kwa sababu ya sheria hizi. Tuzisimamie sheria zetu, mwenye haki ya kuwa jela awe jela, mwenye haki ya kuwa uraiani awe uraiani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wa Jimbo langu la Buchosa pale, nimesoma ripoti hii wametajwa kabisa kwamba wamekula Milioni 94 za bakaa. Halafu mimi naona aibu, hela za amana wamekula bila wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema maneno machache tu. Kwanza, lazima sheria zisimamiwe. Mwisho Waheshimiwa Wabunge niwaombe, neno la Mungu linasema kwenye Mathayo 12.25 ya kwamba Taifa lolote linalopingana lililogawanyika, halidumu. Nyumba yoyote inayopingana na iliyogawanyika, hufa. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge kwa umoja wetu tusimame pamoja kwenye suala hili, tupambane kukomesha wezi kwenye Taifa letu, inawezekana. Utakumbukwa mbele tunakokwenda, Watoto wetu na wajukuu zetu watasema Bunge la 12 chini ya Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu lilibadilisha Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mungu wa Mbinguni awabariki sana. Ahsante kwa kunisikiliza. (Makofi)