Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii na pia nakushukuru kwa muda uliotoa ili tuweze kujadili taarifa hizi tatu zilizowasilishwa na Kamati zetu. Awali ya yote, sishauri tuanze kufikiria adhabu ya kunyonga, kumnyonga mtu ni kumhamishia kwenye mamlaka nyingine ambayo hatuna udhibiti nayo na ni kumpelekea Mungu wahalifu ambao bado hatujashughulika nao. Hawa tushughulike nao kwanza hapa, itakapofika wakati wameshatubu basi ndipo waweze kunyongwa na kupelekwa huko. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwenye mchango wangu nitajielekeza kwenye Kamati ya PIC kidogo, lakini pia na kwenye Kamati yangu ya USEMI. Kwanza nianze kusema kwamba, naipenda sana Wizara ya Kilimo na hii ni kwa sababu, jimbo langu ambalo wananchi waliniamini na kunileta linategemea sana kilimo. Mwaka huu wakati wa bajeti wote kwa pamoja tulipitisha kwa kauli moja kuongeza bajeti kwenye Wizara ya Kilimo na moja kati ya maeneo tuliyosema tuweke mkazo ni kwenye utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili utafiti uweze kufanyika unahitaji vifaa. Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali inasema TARI iliomba vifaa vyenye dola elfu 50 hatukuwa nayo. Bill & Melinda Gates wakatoa msaada, tena hata kabla hawajaachana hawa maana wameshaachana. Vifaa vile vikaletwa bandarini mwaka 2018, bandari wakavishikilia, vifaa vya utafiti vya virusi ambavyo vinaweza kuleta athari kwenye hii nchi na hicho kilimo chote kisiwe na maana, 2018, wakasema wanataka kodi. Msaada umeletwa mabilioni ya Melinda Gates, vifaa hivyo huenda pia vina vitendanishi ambavyo ni sumu vimebaki bandarini, hadi hivi tunavyoongea viko pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumesikia juzijuzi kuna nchi bandari iliungua kutokana na kemikali. Sisi tunawekaje vitu hivi kwenye bandari yetu ambayo nina uhakika wanaovishikilia hawana utaalam huo na bado tunategemea hii nchi itaendelea kuwa salama ambapo tumeweka vitu ambavyo hata hatuvifahamu, lakini ambavyo vingekuwa vinatumika kwenye maabara sasa hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapata shida za magonjwa, virusi, kule kwangu mimi vitunguu kuna ugonjwa unaitwa kaukau hata hatuujui, maabara zetu vitendanishi viko bandarini toka 2018, kisa Wizara ya Kilimo imeomba msamaha. Ndio ile sasa jini likila kwingine linakula hata wakwake, Wizara ya Kilimo Serikali, imeomba msamaha kwa Wizara ya Fedha, msamaha 2018 hakuna, 2019 hakuna, 2020 hakuna, 2021 na leo hakuna, vifaa bado viko bandarini. Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali inasema vifaa hivi vinaweza kuharibika, vitolewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo mengine sijui yanasubiri maazimio au hapahapa tu useme kabisa waweze kufanya maamuzi, mimi sijui, lakini kuna vitu vya hatari kama hivi ambavyo tusipovisemea tutakuwa hatuwatendei haki wananchi ambao wanasubiri kilimo ili kiweze kuwatia moyo. Hili ni jambo ambalo ni moja kati ya mambo unaweza ukayaona yaliyoko TRA kwa namna ambavyo tumekuwa tukitaja. Pia kuna taasisi hapa haupiti muda hatujazisema, tukija tunazisema, tukiondoka tunasema, nadhani huko nje wanasema, watasema watamaliza, halafu sisi tutaendelea na mtindo huo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ufike wakati ieleweke kwamba, tunapokuja humu ndani tumetumwa na wananchi milioni 61 na wale wananchi hawawezi kuja huku kusema ndio wametutuma sisi ili tuwasemee, walipanga mstari tarehe 28 Oktoba, kutupigia kura ili sisi tuje tuwasemee mambo ambayo yanawaathiri wao, tukinyamaza tutakuwa hatuwatendei haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiacha hilo la TARI ambalo linawaumiza wananchi kwa sababu, utafiti haufanyiki kwa sababu vitu viko bandarini kwa sababu Serikali inasubiri kodi kutoka kwenye Serikali yenyewe. Sasa naomba nizungumze kidogo kuhusu hao hao TRA ambapo wameng’ang’ania hivyo vifaa. Ukienda kwenye ripoti inasema kabisa, lita milioni 2.6 za mafuta ambayo yalikuwa yanasafirishwa kwenda nje hayakwenda nje, hiyo ni fedha yenye thamani ya bilioni 1.7, yalipotelea humu ndani. Ripoti inasema mafuta haya kwa kuwa hayakutoka maana yake yatakuwa yaliuzwa humu ndani na Serikali haikupata kodi. Sasa badala ya kushikilia vile vifaa kule si wangeenda wakakusanya hii fedha ya mafuta ya kodi ambayo inapotea? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii TRA iangaliwe. Wakati inaangaliwa ikumbukwe pia kwamba, hii ndio inayofanya ukusanyaji wa mapato makubwa zaidi ili iweze kuangaliwa vizuri, iangaliwe pia na watumishi wake idadi yake kwa sababu, ina upungufu wa watumishi 2,695 kwa mujibu wa Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo, ni mambo ya kuangalia ili tuweze kufanya vizuri na tuweze kutekeleza vizuri Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo ningependa kuzungumza ni mifumo ya taasisi tunazoziunda na dhamira yetu ya kuzifanya ziweze kuendelea. Nimesema pale awali mimi ni Mjumbe wa Kamati ya USEMI, hizi halmashauri zina chombo chake kinaitwa ALAT. Hiki chombo ambacho kinaitwa ALAT kinatarajiwa kuendeshwa kutokana na michango ya halmashauri, sasa kati ya mwaka 2015 na mwaka 2021, jumla ya bilioni
4.56 hazikupelekwa ALAT na kwa kutokupelekwa, hiyo ni asilimia 91 ya mapato ya hii ALAT, maana yake ni kwamba, haiwezi tena kujiendesha. Kwenye taarifa inasema kabisa kwamba, kuna hatari ya ALAT kushindwa kujiendesha kwa sababu haina mapato.

Mheshimiwa Spika, sasa ni vizuri tukatafakari tu kama haina haja ya kuwepo isiwepo, lakini kama kuna haja ya kuwepo, basi hizi halmashauri ambazo hazipeleki zipeleke ili iweze kujiendesha. Hii ndio ingeweza kuwajengea uwezo hawa halmashauri, hii ndio ingeweza kuwajengea uwezo Madiwani wetu ili waweze kufanya kazi vizuri, hawajachanga, hawajapeleka, ofisi iko pale na mimi huwa napita pale karibu kila siku, ni njia ya kule naona kibao ALAT, pale ipo, lakini hii ni ofisi ambayo imekusanya asilimia tisa tu ya mapato yake kwa miaka karibu nane, inawezaje kujiendesha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwenye maazimio yetu ni vizuri kuweka mkazo kwenye zile taasisi ambazo zilitarajia kuchangiwa na hazikuchangiwa na ambazo haziwezi tena kujiendesha ili ziweze kufanyiwa tathmini na kuona uhitaji wake na kuona namna zinavyoweza kujiendesha, kama haziwezi kujiendesha basi maamuzi yafanyike ili zisiwepo, kwa sababu mwisho wake ni kuanza kuzalisha madeni ambayo Serikali yetu itakuja kuanza kuhangaika kuyalipa hapo baadae.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kidogo kuhusu hizi taasisi zetu. Mheshimiwa Sanga, aliyekaa alizungumza sana kuhusu GPSA, lakini tuzungumzie MSD ambayo pia imetajwa mara nyingi sana hapa. Huko nyuma nadhani kulikuwa na utaratibu wa taasisi kununua dawa MSD. Ikaonekana katika utaratibu huo MSD hailipi, Kwa hiyo ili kuweka utaratibu mzuri ikaamuliwa kwamba fedha ziende kwanza MSD halafu ndipo MSD ilete dawa. Sasa kibao kimegeuka, MSD inapewa hela na haitoi dawa. Kwa hiyo Bilioni 1.7 ambazo kila siku Waheshimiwa Wabunge tunalalamika, wananchi wanalalamika hakuna dawa, hizi fedha zililipwa MSD na MSD haikutoa dawa.

Mheshimiwa Spika, mwaka umekwisha, hizi fedha hazirudishwi kwenye Halmashauri na hazifanywi chochote. Kwa hiyo, kama mfumo huu ukiendelea maana yake ni kwamba MSD itakuwa inapokea hela zaidi ya kile ambacho huduma imetoa. Ushauri wangu ni kwamba iangaliwe mifumo ya ulipaji, huu wa GPSA na taasisi yoyote inayopata fedha kwanza, iwe GPSA, TEMESA, MSD au taasisi yoyote inayopokea hela kwanza, mfumo wake uangaliwe vinginevyo tuweke mtu kati, kuwe na taasisi ambayo hela ile inapelekwa, ukishatoa huduma unaenda unadai, siyo umeshapokea hela unakuwa sasa unaamua wewe unachotaka kukifanya, maana yake ni kwamba kunakuwa na ugumu kwa sababu tayari umeshalipwa, umeshapokea fedha. Sasa isipoangaliwa hii mifumo, hii hali itaendelea na hii ni hali ambayo inaweza ikawa changamoto katika utoaji wa huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati huohuo tuchunguze vizuri kwa nini dawa ambazo ni shida hazipatikani lakini kwenye taarifa inaonesha kuna dawa zenye thamani ya Shilingi Bilioni 7.3 zimeteketezwa. Inawezekana pia kuna changamoto kwenye mfumo wa uagizaji wa dawa, kwa hiyo dawa zinapofika kwa watumiaji zinakuwa zimebakiza muda mfupi na kwa hiyo zinatakiwa kuteketezwa. Sasa taasisi hizi ambazo zimetajwa mara nyingi humu zinatufanya tuone kuna haja ya kufanya maamuzi na maazimio yatakayoweza kukomesha jambo hili.

Mheshimiwa Spika, sisi umetuteua kwenye Kamati, tunakaa kule tunafanya maamuzi. Nakumbuka Kamati ya Bunge ya USEMI kwa mfano, Halmashauri zote zilikuja tukajadiliana nazo vizuri, wale ambao ni wa asilimia 10 tukawaambia. 2021 tuliwaambia asilimia 10 zote wapeleke kama ilivyopangwa, hawakupeleka! 2022 wamekuja wapo. Sasa tunawakuta ni walewale, Spika wewe umetutuma, tunawauliza tena walewale ambao tuliwatuma iliyopita na hawakufanya lakini wanarudi tena kwetu ni walewale.

Mheshimiwa Spika, hata kama ingekuwa wewe, yule mtu ulimwambia, hakufanya, anarudi unamwambia hakufanya! Hivi keshokutwa nakaa naye namwambia tena? Sasa ntamwambiaje ten ana mtu huyo hataki kutekeleza?

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo mimi naunga mkono hoja na ninaomba hatua kali zichukuliwe kwa wale wote ambao hawaitakii mema Serikali hii. Mungu awabariki sana, ahsante sana. (Makofi)