Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja zilizopo mezani. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja zote zilizopo mezani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nijielekeze zaidi kwenye taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hasa katika Bodi ya Mikopo. Mwalimu Nyerere alitueleza kwamba maadui wakubwa kabisa katika nchi hii ilikuwa kwanza, ni ujinga na wengine wakafuata. Akaweka mifumo ya kufuta huu ujinga kwa maana ya kumtokomeza kabisa huyu adui. Pia Mwenye hekima mmoja Jeff Rich alisema:

“If you think education is expensive, then try ignorance”

Mheshimiwa Spika, anamaanisha, kama unafikiri elimu ni gharama, basi jaribu ujinga. Kwa muktadha huo tunamshukuru sana Rais Wetu Mama Samia Suluhu Hassan ambaye amejipambanua vizuri kabisa kuhakikisha kwamba anaondoa ujinga katika nchi hii. Tumeona mwaka jana alianza kutoa fedha nyingi ili kujenga madarasa ili Watanzania wengi wapate fursa ya kwenda kusoma na kuweza kufuta ujinga. Hata hivyo mwaka huu tena tumeona bilioni 160 zimetolewa ili madarasa 8,000 yakejengwe ili Watanzania wakaweze kusoma. Tunamshukuru zaidi kwenye kuongezea fedha kwenye Bodi ya Mkopo mpaka kufikia bilioni 570. Kwa kweli anajitahidi na anafanya kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika ripoti ya CAG inaonesha kwamba kwa kipindi cha miaka mitano ambacho amefanya ukaguzi ni 72% tu ya wanaostahili kupata mikopo ndio wamekuwa wakipata mikopo. Pia imeonesha kuna wanafunzi 492 ambao wao walishindwa kuendelea na masomo kwa sababu walishindwa kupata mikopo hali ya kuwa wao ni watoto wanaotoka kwenye familia maskini. Hivyo walishindwa kuendelea kusoma.

Mheshimiwa Spika, inaonesha vile vile kuna kiasi cha fedha Sh,1,768,000,000 ambapo katika mwaka 2017/2018 wanafunzi wapatao 5,650 walipokea mikopo ambayo hawakustahili. Tena aliendelea kutaja kwamba kumekuwa na changamoto kubwa kwamba mifumo haisomani. Wanafunzi wanapata shida wanapokwenda kuomba ili wapate mikopo. Kwa mifumo kutoka Baraza la Mitihani ukiangalia pia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini pamoja na Mamlaka ya Usajili wa Vitambulisho vya Taifa, hii mifumo haisomani. Kwa hiyo, kumekuwa na changamoto kubwa kwa wanafunzi kupata shida katika kuomba waweze kupata nafasi ya kupewa mikopo hiyo.

Mheshimiwa Spika, imeoneshwa pia kwamba Bodi kwa muda mrefu kwa kipindi hiki cha miaka mitano imekuwa ikitoa kiwango cha chini cha mikopo kwa kila anayekuwa akiomba. Pia kwa kiwango cha juu kwa kati ya Sh.3,100,000/= kwa wanafunzi kati ya 896, zote hizi ni chanagamoto ambazo CAG amezionesha. Hizi ni chanagamoto kubwa.

Mheshimiwa Spika, taarifa imeonesha katika kipindi cha mwaka 2018/2019, kuna wanafunzi wapatao 6,183 ambao walipangiwa mikopo kwa kiwango cha juu zaidi ya vile walivyostahili ambapo kiasi cha Sh.5,668,843,000/= kilitumika, lakini pia kuna wanafunzi 2,852 walipata kiwango cha chini cha uhitaji wa mkopo kiasi cha Sh.1,147,000,000/=. Kwa hiyo kunaonekana kwamba kuna fedha nyingi ambazo zimekuwa zikitolewa nje ya utaratibu. Kwa hiyo kwa miaka mitano inaonesha kwamba kuna jumla ya Shilingi bilioni 13.7 ambazo zimetolewa kwa watu ambao hawakustahili, ambapo kiasi hiki kingeweza kutosheleza wanafunzi ambao walipata mikopo ya chini kama 10,075 ambapo pia kingeweza kulipia wanafunzi wengine wapya ambao waliomba kama 3001. Kwa kweli changamoto ni nyingi.

Mheshimiwa Spika, nimeamua kuchukua kipande hiki kwa sababu nimekuwa nikipokea malalamiko mengi ya watoto ambao hawana uwezo, maskini kutoka katika Jimbo langu la Kalenga na majimbo mengine ambao wamekuwa hawapati mikopo kwa kukosa umakini kwa hawa wenzetu ambao tumewapa dhamana.

Mheshimiwa Spika, ukaguzi katika kipindi hicho cha miaka mitano, umeonesha kuna wanafunzi 756 ambao waliostahili kupata mikopo lakini hawakupata. Ni mambo mengi yamekuwa yakiendelea. Vile vile tunaoneshwa kuwa kuna ambao walistahili kupata mikopo kiasi cha 192,039 lakini ambapo walitakiwa wapate kiasi cha Sh.569,313,000,000/=, sasa hili sio tatizo la watu wa Bodi ya Mikopo kwa sababu ni uwezo wa Serikali kuwapa hiyo mikopo ulikuwa mdogo kwenye hilo eneo.

Mheshimiwa Spika, tumeona sheria na miongozo katika Bodi ya Mikopo ambayo inawataka wanafunzi ambao wako katika uhitaji wa juu wa mikopo, kwa mfano, wale ambao wanatokana na kaya maskini ambao wanatakiwa wapewe mikopo, kiasi cha wanafunzi 22 hawakupata mikopo hiyo. Hii ni kati ya kipindi cha miaka miwili 2019/2020 na 2020/2021 kiasi cha Sh.84,000,000 zilitakiwa zitolewe lakini hazikutolewa. Pia inaonesha kuna watoto 95 ambao wanatoka katika zile familia za yatima (baba na mama wamefariki) na mwongozo unaonesha kwamba ni lazima wapewe, lakini hawakupewa. Walipoulizwa wanasema kwamba, mfumo hautambui kwamba wale watoto wanaotoka familia maskini au yatima ndio wanaotakiwa kupewa kwanza. Hayo ndiyo majibu ambayo bodi iliyatoa. Hii nayo tunaiona ni changamoto kubwa.

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ambayo bodi wamekuwa wakiipata ni kwamba, wakishapeleka fedha kwenye taasisi zile za juu kwamba kuna wanafunzi
100 katika pengine Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walitakiwa kupewa mkopo, bodi inapeleka, ikishapeleka kule, wale wanafunzi wasipopewa ndani ya siku 30 mwongozo unasema zile fedha zinatakiwa zirudi kwenye Taasisi ya Bodi ya Mikopo ili waendelee kuwakopesha wengine. Sasa imetokea tatizo kwamba kumekuwa na ucheleweshaji. Kwamba hawarudishi kwa wakati ndani ya siku zile 30, kwa hiyo, kunainyima furs ana uwezo Bodi ya Mikopo kuendelea kukopesha wanafunzi.

Mheshimiwa Spika, sasa nakuja na mapendekezo kulingana na yale ambayo nimeyaona, niombe wenzangu wa Kamati, najua walikuja na mapendekezo yao, naomba wapokee na hii nyongeza ya mapendekezo ambayo nimeona kutokana na kile ambacho nimekisoma kutoka kwenye Taarifa ya CAG.

Mheshimiwa Spika, pendekezo la kwanza, niombe taasisi zote ambazo zinahusiana na usajili wa wanafunzi yaani mifumo yake iweze kusomana. Nikimaanisha Bodi ya Mikopo, Vitambulisho vya Taifa pamoja na Usajili, Ufilisi na Udhamini mifumo yake isomeke ili iwe rahisi kuondoa matatizo yanayotokana na forgery. Pia bodi ihakikishe wale wanaopewa mikopo ni wale wanaostahili kupewa mikopo kama wale watoto maskini kutoka katika kaya zile zinazohudumiwa na Serikali, watoto yatima, ihakikishe kwamba wanapewa. Wanachotakiwa kufanya ni kubuni tu mbinu za namna gani ya kuwasaidia, wanaweza wakawa pengine na dawati maalum la kuweza kuwasaidia hawa, kama mfumo hauwatambui, basi waweze kuandaa dawati maalum la kuweza kuwasaidia.

Mheshimiwa Spika, pia tufanye tafiti kuona nchi nyingine zinafanya nini kusaidia Bodi hizi za Mikopo na taasisi nyingine ambazo zinasaidia watoto kusoma, kuona vyanzo vyake vinatoka wapi ili tutafute vyanzo vingine, lakini tunaweza kujifunza kutoka nchi nyingine. Pia taasisi za elimu ya juu kwa maana ya vyuo vikuu zihakikishe kwamba wanafuata mwongozo wa Bodi ya Mikopo kwa maana kwamba zile fedha ambazo hazijaenda kwa wanafunzi waliotakiwa kupewa na hawakupewa ndani ya siku zile 30 basi zirudishwe ndani ya wakati kama mwongozo unavyosema, ndani ya siku 30.

Mheshimiwa Spika, mapendekezo mengine, naomba uchunguzi ufanyike kulingana na haya makosa ambayo yameainishwa ni mengi mno. Uchunguzi ufanyike ili waone kama ilikuwa ni maksudi ya kuibia Serikali ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa haraka. Pia kuwe na kitengo maalum kama huduma kwa wateja cha kusaidia kupokea na kutoa ufafanuzi pamoja na kutatua changamoto kwa wakati ambazo zinaikabili Bodi ya Mikopo.

Mheshimiwa Spika, ushauri mwingine ni kwamba TAKUKURU watumie hii ripoti ya CAG kuhakikisha kwamba wanafuatilia na kuhoji hizi Taasisi za Serikali Bodi ya Mikopo ikiwa mojawapo na nyingine ambazo zimetajwa na kazi yao iwe ya muda mfupi kwa sababu wamerahisishiwa. Suala la TAKUKURU kuchukua miaka miwili miaka mitatu, wakati taarifa hizo wameshatafuniwa hiyo inatia mashaka, kwamba inaweza ikawa kuna coalition pia hata huko ndani ya TAKUKURU pia kwa sababu nao pia ni binadamu.

Mheshimiwa Spika, hivyo, tuombe kwamba ripoti hii waifanyie kazi kwa muda mfupi, hatutaki kusikia miaka miwili miaka mitatu, unachunguza nini wakati tayari umeshatafuniwa. Kwa hiyo, naomba TAKUKURU hili walifanyie kazi.

Mheshimiwa Spika, mimi niliomba nichangie hayo kwa uchache, ni eneo hilo moja tu, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Ahsante sana. (Makofi)