Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa nafasi kwa ajili ya kuchangia Taarifa za Kamati hizi tatu ambazo zimewasilishwa katika Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naunga mkono hoja katika taarifa zote zilizowasilishwa na Kamati za PAC, LAAC na PIC. Pia nipongeze Serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye yeye ametoa mazingira rafiki kuweza sisi wote kukaa hapa katika Bunge lako Tukufu na kuweza kujadili taarifa za Kamati hii kwa ajili ya Serikali yetu.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchovu wa fadhila nisipoipongeza Ofisi ya CAG ambayo kwa weledi na uzalendo imeleta taarifa zilizoshiba na sisi tukaweza kuzipitia na kudadavua na kuweza kutoa maoni kwa ajili ya maslahi ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba taarifa ya CAG tumeipitia, tumeiona, tumehoji Wenyeviti wa Taasisi na Maafisa Masuuli pamoja na wasaidizi wao. Katika maeneo hayo nitaomba nijikite katika eneo moja, dosari katika usimamizi wa mikataba na athari zake katika matumizi ya fedha za umma.

Mheshimiwa Spika, tutaona katika maeneo haya michango mingi imejikita katika eneo hili. Ni kwa sababu gani? Kwa sababu eneo hili ni eneo ambalo linagusa maslahi ya wananchi moja kwa moja, ambapo Mheshimiwa Rais anatafuta fedha ili ziende kuleta thamani ya fedha katika miradi mbalimbali ya maendeleo lakini tunaona watu wachache, wanaweza kufanya utendaji wa uzembe, usiozingatia misingi ya kanuni na sheria na kuweza kutumia hizi fedha kinyume cha taratibu.

Mheshimiwa Spika, naomba nijikite katika mfano wa baadhi ya taasisi ambazo tunaona katika utendaji kazi wake zimeweza kwenda ndivyo sivyo. Nianze na Taasisi ya TANROADS. TANROADS ni taasisi ambayo imepewa dhamana ya kujenga miundombinu ambayo inagusa moja kwa moja maslahi ya mwananchi katika miundombinu ya barabara na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, TANROADS wapo wataalam, wapo wanasheria wazuri, wapo viongozi ambao wamepewa dhamana na Serikali na ukiangalia wanajua sheria zote, lakini tunaona kwamba katika eneo hili badala ya kuzingatia sheria na kanuni zinazoongoza taasisi hiyo, watu wanatoa certificate za kumaliza kazi, siku zinaisha za kisheria 28, Mataifa ya nje 56 bado fedha hazijalipwa, Serikali inaingia katika hasara. Tunaona hasara ya bilioni 68.7.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nakokotoa kwa ufupi kuona hizi fedha kwa bajeti yetu ya TARURA ile ambayo majimbo yetu tunapokea bilioni 2.5, majimbo 30 yote yangepata bajeti ya mwaka mzima, lakini hizi fedha zote zimehama kwenda kulipa riba kwa sababu ya kuchelewesha malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo hili haliwezi kuvumilika. Kwa hiyo kupitia Bunge lako tukufu niombe hawa watumishi ambao walitakiwa kufanya kazi kwa weledi wajitathmini na Bunge lako litakuja na mapendekezo ambapo niombe Wabunge waniunge mkono ili iweze kuingia kama moja ya maazimio ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni eneo la Mkataba wa Mradi wa REA I, REA II, REA III ambao kwa uchache tu CAG ame-spot Mkoa wa Mara. Kwenye scenario hii unaona kampuni moja tu inaweza kutumia milioni 329 za Serikali haiguswi, haisemwi chochote, haichukuliwi hatua. Ukiangalia mambo mengine kwa kweli yanaumiza. Hii kampuni ya Derm Electrics Tanzania Limited hizi pesa ilinunua vifaa vya kuweza kusimamisha miundombinu ya umeme. Miundombinu haikusimamishwa, watu zaidi ya 4000 hawakupata huduma. Hivyo vifaa badala ya kuvikabidhi TANESCO, imebaki navyo na mpaka leo hakuna hatua yoyote ya kisheria ambayo imechukuliwa. Sasa unajiuliza katika eneo hili hivi kiburi hiki hii kampuni inakitoa wapi?

Mheshimiwa Spika, watumishi ambao wanasimamia kampuni hii na miradi hii kiburi cha kutokuchukua hatua wanakitoa wapi? Niombe kupitia Bunge lako Tukufu. Tabia hii tukiiacha ikaendelea itaambukiza na watumishi wengine ambao ni wazalendo kwa nchi hii waweze kuiga matendo ambayo siyo mazuri. Kwa hiyo niombe sana katika Bunge lako Tukufu tuweze kuchukua hatua ambazo baadaye nitapendekeza.

Mheshimiwa Spika, wakati roho yangu inaendelea kuuma na kusononeka kwa hujuma hizi dhidi ya Serikali, nikapitia hotuba ya mbeba maono wa nchi hii Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alivyohutubia Bunge lako Tukufu tarehe 22 April 2021. Naomba kunukuu. Katika eneo hili tukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ukurasa wa 32 amesema yafuatayo; “Serikali ya Awamu ya Sita kama ilivyokuwa Awamu ya Tano itaendeleza jitihada za kuimarisha nidhamu ya uwajibikaji kwenye Utumishi wa Umma. Tunakusudia kuimarisha taasisi na pia kuweka mifumo ya uwajibikaji ambayo itahakikisha kwamba viongozi na watumishi wa umma katika ngazi zote wanawekewa malengo yanayopimika. Mfumo uliopo wa sasa ikiwemo mikataba kati ya kiongozi na walio chini yake pamoja na OPRAS tutaiangalia upya.”

Mheshimiwa Spika, nitakuja kueleza kitu juu ya OPRAS. Hata hivyo, Mheshimiwa Rais akaenda mbali akasema: “Tutawapima viongozi na watumishi kwa namna wanavyotimiza majukumu yao na msisitizo akasema hatutawaonea aibu viongozi na watumishi wazembe, wezi, wabadhirifu wa mali za umma.”

Mheshimiwa Spika, leo Mheshimiwa Rais ameshatuwekea mambo kibla, tumsogezee kwenye 18 amalize kufunga mabao. Hawa wote ambao wamehusika katika kuhujumu fedha za Serikali, tumsogezee amalize kazi. Mheshimiwa Rais ahangaike kutafuta fedha, lakini usimamizi huu kupitia Bunge lako Tukufu, tuweze kumsaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo lingine, tunaona kwamba katika mapendekezo ambayo ningeomba kuleta kwenu, niombe kweli kupitia Bunge hili, Bunge liridhie watumishi wote waliosababisha hasara hizi na Maafisa Masuuli wote wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria pia mamlaka za uteuzi zinapoona yule aliyekosa na anahusika, ni suala dogo la Mheshimiwa Rais na viongozi waandamizi kuchukua hatua mara moja ili tutoe huu uozo uliopo ili tuweze kuleta watu wengine ambao wanaweza kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili ambalo niombe Bunge lako Tukufu, kupitia hotuba hii ya Mheshimiwa Rais kuna kipengele ambacho nimesoma anasema OPRAS tutaiangalia upya. OPRAS ni tathmini ya utendaji kazi ya watumishi wote wa umma, kuanzia Ma-CEO na wasaidizi wao. Ningeomba maboresho yanayoletwa yawahusu Maafisa Masuhuli. Katika eneo hili nimeangalia vipengele nane vilivyopo katika OPRAS vyote hakuna kitu kinachoongelea suala la hoja za Serikali za CAG katika taasisi husika. Kwa hiyo unampima kiongozi wa taasisi, hii OPRAS ambayo ni kipimo cha kazi, lakini hakuna sehemu ambapo tunamuuliza kwa nini ulipata hoja hii? Kwa nini hukujibu hoja hii na kwa nini uliweza kupata hati isiyoridhisha? Hakuna.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kupitia Bunge lako Tukufu niombe katika vipengele nane hivi kiongezwe kipengele cha tisa ambacho kitasaidia kuweka kipengele cha hoja za CAG ili Mkuu wa Taasisi awe anatathminiwa na anayemtathmini akienda pale inabidi agote kidogo ili kuhakikisha kwamba yote ameya-capture.

Mheshimiwa Spika, katika pendekezo la mwisho na ombi kwa Bunge lako Tukufu, nikuombe, kwanza kabla ya ombi hili nikupongeze kwa kuwa wewe umekuwa mtu wa maono na kabla ya taarifa hii kuja ulituongezea muda wa kufanya kazi kwa hizi Kamati zote tatu, tangu tarehe 10 sisi tuko hapa, tunakaa mpaka usiku. Pamoja na muda na maono yako ya mwanzo tumeweza kupitia taarifa hizi chini ya asilimia 10.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninachokuomba, kwa uweledi wako na maono, uangalie namna njema ambapo Kamati hizi zitaongezewa muda ili tuweze kupitia taarifa hizi kwa kina na kwa wingi. Hakika nakwambia kwa hili utakalolifanya kwa Taifa hili, tuko tayari kukujengea mnara mmoja ubandikwe Dodoma na mwingine tuupeleke Dar es Salaam kwa sababu utakuwa umefanya kazi ya kizalendo ambayo haijawahi kutokea katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuombe sana haya mambo ni mema kwa ajili ya nchi yetu, tuungane pamoja kumsaidia Mheshimiwa Rais ili hizi fedha zisimamiwe vizuri, miradi ionekane kwa wananchi katika majimbo yetu yote na baada ya hapo Serikali itapongezwa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nikushukuru kwa nafasi na naomba kuunga mkono hoja taarifa zote ambazo zimewasilishwa. Ahsante sana. (Makofi)