Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia taarifa ya CAG. Ni kwamba Wabunge wengi wamezungumza hapa kwa hisia kali, na wanaonesha wanavyoguswa namna upotevu wa fedha za Serikali. Hata hivyo kitu kinachonishangaza ni kwamba; mimi nilikuwa naangalia pamoja na ugeni katika Bunge hili kwa miaka miwili. Taarifa hizi zinazosomwa hapa za CAG ni hadi tarehe 28 mwezi wa pili mwaka huu. Sasa, kutokea mwezi wa pili mwaka huu tunakuja kusoma taarifa hizi kuja kuanza kuzichambua, ni mwezi wa kumi na moja, tofauti yake ikiwa takribani miezi kumi au tisa ipo pale.

Mheshimiwa Spika, sasa hapa kunakuwa na ombwe kubwa sana hapa katikati; mambo mengi yanakuwa yamekwishakuharibika au yanakuja kurekebishwa wakati taarifa hii inaonekana kama inakuwa imepitwa na wakati. Kwa sababu kuna jambo linakuja kuzungumzwa hapa sasa hivi, limeshafanyiwa kazi. Sasa tunauliza, kwa nini hili jambo tusianze tu baada ya taarifa ya CAG kuletwa na kupelekwa kwa Mheshimiwa Rais ikapokelewa. Pale pale, Kamati yako ya PIC ianze kazi hapo hapo, halafu na Bunge hili la Mwezi wa Tatu, tuanze kujadili kwa siku nyingi siyo hizi siku tisa; twende kwa siku 30 ili tuweze kuwaadabisha hawa watu.

Mheshimiwa Spika, fedha zinazopotea ni nyingi sana. Leo mimi nimekuja na vitabu hapa, yote nimeyasoma, nilikuwa naangalia. Hiki ni kitabu tu kwa ajili ya Sengerema peke yake, Jimbo langu, ninapotoka mimi. Hii ni kwa ajili ya Serikali za Mitaa, taarifa hii ni kwa ajili ya mashirika ya umma. Sasa ukichukua hizi taarifa na hii nyingine niliyonayo hapa, yakikaguliwa haya yote, hata yakisomwa haya, bado hatuwezi, sisi Wabunge, kwa nafasi yetu finyu na ratiba zetu za Bunge hatuwezi kwenda sawa kuzichokoa zote hizi tukaziweka zote hapa kwako. Kamati yako hii ya PIC pamoja na kazi nyingi ulizokuwa umeipa. Wanazunguka sana na hao wanaokwenda kuwaita kwenda kwenye hao mashirika ya umma au taasisi za Serikali wanaonesha wana kiburi kikubwa.

Mheshimiwa Spika, sasa hili Bunge lako tunataka kujiuliza, je, tulichokosea hapa ni wapi? Ni mfumo wetu wa Bunge? Tuangalie Mabunge ya wenzetu kule Jumuiya ya Madola yanashiriki vipi katika shughuli hizi zinazoletwa na taarifa ya CAG kuzifanyia kazi. Tukijifunza kwa wenzetu tukaona wanadhiti namna gani hili jambo, halitajirudia. Hapa kuna taarifa za tangu mwaka 2011. Kwa hiyo, wameshaona taarifa hizi zinazoletwa hapa labda zinaletwa kama taarifa za mapato ya harusi au zinaletwa hapa za michango ya kanisani, kwamba labda hii michango haitakaguliwa au michango ya msikitini.

Mheshimiwa Spika, lakini hizi ni fedha za kodi za wananchi, tukiwemo sisi Wabunge, tunakatwa kodi, na wewe unakatwa kodi kwa sababu na wewe ni Mbunge. Sasa, ifikie mahali tuje na maamuzi makali, kwa sababu sasa hivi naangalia hiki kitabu kimoja, kinazungumzia taarifa zilivyo pamoja na vielelezo. Sasa najiuliza tuje na sheria, tukuombe hapa umwambie Mwanasheria Mkuu wa Serikali aje na sheria ya kuiongezea meno kumuongezea meno CAG. Kwa sababu akimaliza kukagua anawaomba wale watu walete vithibitisho; taarifa zinazokosa vithibitisho ndizo zinaletwa hapa kama zimeiva vilivyo; kwamba hizi ni sahihi; kwa nini asiwapeleke Mahakamani moja kwa moja, huyo huyo CAG, kwa sababu yeye ndiye mwenye ushahidi na watoa ushahidi anao yeye? Hao watu baada ya hapo wanapelekwa TAKUKURU, hili jambo linakwenda kufia kule na hawa watu unawaona wanaendelea kupata vitambi, wanapiga miluzi barabarani na mwaka kesho, tunakuja kujadili taarifa nyingine tena ya CAG.

Mheshimiwa Spika, mimi napata kigugumizi sana. Mama yetu Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu kama sasa hivi tunavyomuona anavyosafiri, leo yuko China, sijui kesho kutwa ratiba yake inasemaje hayo ni mambo ya kiitifaki. Lakini anapokwenda huko anakwenda kutafuta hizi fedha, na bahati mbaya fedha hizi zingine zinazoletwa ni madeni. Sasa zikija hizi fedha hapa zinakuja kuibiwa, na tunakuja tena na taarifa nyingine mwezi wa pili tena, mwaka kesho tutapokea vitabu vingine kama hivi; hivi havijafanyiwa kazi anachukuwa vitabu vingine. Sasa mama anahitaji usaidizi wa hatua akali kabisa, zibadilishwe hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kwa sababu sehemu ya Mawaziri na Manaibu wanatoka kwetu sisi kama Wabunge, na sisi ni wenzetu wale, lakini kule wanakokwenda kufanya nao kazi ni watendaji na wataalamu wa Serikali. La sivyo, taarifa zitakuwa zinakuja tunaondoka na Mawaziri, kesho tena tunaweka Wabunge wengine, tuanondoka nao. Sasa inaonekana tunajipiga sisi kwa sisi. Sasa jamani Wabunge ninachotaka kuwaambieni humu ndani, tukiwa pamoja lazima tuombe sheria kali kwa hawa watu; na anayetajwa na taarifa ya CAG kwanza hawa watu wangekuwa wako nje na wanaripoti polisi kila siku, mpaka kazi zao ziishe na mishahara ikatwe. Tuunde sheria kama hiyo, watu wataacha kucheza na hizi fedha (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kilichonisikitisha zaidi kumbe mpaka sasa na Ubalozini fedha zinaibiwa, tena Ubalozi wa heshimia kama Marekani. Naangalia hapa mimi fedha za visa tu ambazo zimeibiwa ni takriban milioni 670. Kule kule Marekani tumenunua jengo dola milioni 25 na lile jengo lilikuwa na sehemu za kukodisha lina floor sita na katika lile jengo floor mbili zinafanya kazi. Floor nne hazifanyi kazi na wateja waliokuwa katika zile floor nyingine nne wamehama kwa sababu ya kushindwa kukarabatiwa lile jengo. Tumepata hasara shilingi bilioni 27 sawa sawa na vituo vya afya zaidi ya 70.

Mheshimiwa Spika, sasa huyu mama sijui tutamsaidiaje? Sisi Wabunge ndio tunatakiwa tumsaidie. Kama na mabalozi na wenyewe tena, ndio watu wa heshima, anaondoka anakwenda kule, balozi tena anakuwa naye ni sehemu ya upigaji, hii nchi sasa ni hatari hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naangalia hapa Ubalozi, sijui wa Uholanzi, Addis -Ababa, Kampala, Berlin; yaani hakuna balozi hapa ambaye yuko salama. Sasa kama tuna mabalozi 43 tunaibiwa fedha kiasi hiki, hata fedha za visa, wageni ambapo wanapita, yaani watu hawaogopi. Kwa sababu mgeni anayepita, atapitia mipakani uwanja wa ndege, taarifa ziko kote, halafu na hizo na zenyewe zinaibiwa. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakuja kwenye suala la Msajili wa Hazina. Hii KADCO ni sehemu tu ya kampuni ambazo ninyi mnaziona ambazo Msajili wa Hazina anazo ambapo kule Msajili wa Hazina ninyi mnaona hiyo ni sehemu ndogo tu, kuna TIPER kule. Pale TIPER kuna tatizo kubwa. Tuna wanahisa wenzetu pale. Msajili wa Hazina ni sehemu ya mtu ambaye anatakiwa kuitwa aje aoneshe mashirika yote ambayo sisi tuna hisa, tunayoyamiliki na watu wengine tofauti, yaje yakaguliwe na Kamati hii ya PIC.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hali hiyo, bado kuna PUMA. Kule PUMA, kumenza kuuzwa kwa sababu kuliuzwa Sheli, Sheli wakauza kwa BP na BP wakaenda kumuuzia PUMA. Sasa hivi PUMA sijui wanaenda kumuuzia nani tena! Kwa hiyo, kote kule Msajili wa Hazina na kwenyewe kule tuna mali zetu, siyo sehemu hiyo tu. Kwa hiyo, yaletwe mashirika yote halafu Msajili wa Hazina atakuwa anasema hapa hakuna fedha, hapa fedha ziko hivi.

Mheshimiwa Spika, pia tuna uwanja nyuma ya Chuo cha Mwalimu Nyerere pale Kigamboni na lile eneo linalozunguka katika hayo maeneo. Huu uwanja uko wazi, zaidi ya ekari 60 au 100 ziko pale, lakini ICD ziko Dar es Salaam sasa hivi kila kona, watu wanavunja nyumba wanaanza kuhifadhi makontena. Barabara ya kupeleka haya makontena kule kwenye huo uwanja ambao uko bandarini pale pale ng’ambo ya bandari, tungeweza kuweka makontena, haya makasha yote. Kasha moja linaanzia Dola 250 na kuendelea. Tungehifadhi makasha pale, hizi tozo zisingekuwepo. Inaonekana usaidizi kwa Mheshimiwa Rais bado hajapata watu sahihi wa kumsaidia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pamoja na mambo mengine, hivi viwanja ambavyo majengo yanavunjwa; anaonesha hapa CAG. Viwanja vinavunjwa na vile viwanja vinakaa wazi. Si tungekuwa tunaweka haya makasha matupu na yenyewe yakawa ni sehemu tu ya ICD kule, mpaka siku watakapokuja kujenga hayo majengo, tuanze kupata hizo fedha za kontena. Kwa hiyo, mahali pa kupata fedha papo na CAG hapa anatuonesha.

Mheshimiwa Spika, cha kusikitisha, CAG hapa amenishangaza mimi anasema, zaidi ya mashirika 60 ya Serikali hayana Bodi za Wakurugenzi. Sasa ni maajabu. Bado
anasema CAG ameshindwa kwenda kukagua… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Malizia sentensi, dakika moja.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, CAG ameshindwa kwenda kukagua hizi Bodi za Wakurugenzi kwa sababu sheria inamruhusu Katibu Mkuu wa Wizara husika kusimamia tu kwa muda wa miezi 12. Baada ya miezi 12, CAG hawezi kwenda pale wala Katibu Mkuu hawezi tena kwenda katika lile shirika. Kwa hiyo, wale Wakurugenzi (directors) waliobakia kule walewe wanaendesha yale mashirika kama mali zao binafsi. Imenitia hofu sana.

Mheshimiwa Spika, pia pale pale kuna bodi ambazo ni za muhimu sana katika nchi hii. Kama Bodi ya Pamba; unakuta Bodi ya Pamba na ya Mbolea; leo tunatoa ruzuku ya mbolea, hakuna Bodi ya Wakurugenzi kule.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)