Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii nami nichangie na mchango wangu utajielekeza kwenye taarifa ya Kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa maana ya PIC.

Mheshimiwa Spika, nitajielekeza zaidi kwenye Bima za Ndege (Aviation Insurance) za Shirika letu la ndege la ATCL. ATCL imekuwa ikikata bima za ndege zetu kupitia Shirika la Bima la Taifa NIC, ambao nao wamekuwa wakikata bima kwa kupitia kampuni ya nje (International Broker) inayojulikana kwa jina la MASH. NIC wamekuwa wakifanya hivyo. Kwa kutumia mfumo wa single source. Sasa kwa ufupi, kila mwaka Shirika la ATCL limekuwa likilipa bima ya gharama ya ndege zake, zifuatazo, nanukuu: -

“Mwaka 2018/2019 Bima ya Afya kwa mwaka ilikuwa takribani Shilingi bilioni 5.8; kwa mwaka 2019/2020, gharama ya bima kwa mwaka ilikuwa takribani Shilingi bilioni 14.5; kwa mwaka 2020/2021 gharama ya bima kwa mwaka ilikuwa takribani Shiligni bilioni 18.7 na kwa mwaka 2021/2022 gharama ya hizi bima za ndege ilikuwa takribani Shilingi bilioni 21.3.”

Mheshimiwa Spika, sasa kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023, Shirika la ATC liliamua kuitaka NIC walete kampuni nyingine ambazo zinaweza zikatoa huduma hii ili kufanya ulinganifu wa gharama ya bima kila mwaka ambayo Shirika la ATC wanalipia. Walipofanya zoezi hilo, waliweza kupata kampuni mbadala inayojulikana kwa jina la WILL STAWA, ambao walitoa quotation ambayo ilikuwa ni pungufu ya gharama ya yule international broker ambaye NIC anamtumia siku zote kwa takribani Shilingi bilioni tatu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kitendo hicho, Shirika la Bima la Taifa la NIC lilisababisha yule single source, International Broker wanayemtumia (MASH) naye akashusha quotation yake kwa gharama ya Shilingi bilioni tatu ili ifikie ile ya kati ya hao wapya ambao walikuwa wamejitokeza. Jambo hilo binafsi naona lina utata kidogo, inakuwaje kwa urahisi tu uweze kushusha kwa zaidi ya takribani bilioni tatu kwenye bima za ndege kwa mwaka?

Mheshimiwa Spika, ili Shirika la Bima la Taifa (NIC) liweze kukidhi Matakwa ya Sheria ya Manunuzi ya Umma inatakiwa yule international broker awe na partner wa hapa Tanzania. Kwa hiyo, ndivyo ambavyo wameendelea kuwa wanafanya hivyo. Yule partner wa Tanzania anapata 15% ya premium commission, lakini ikifanyika tafiti vizuri, inaonekana kwamba yule local partner ambaye ameandikwa yupo tu kwenye makaratasi, haonekani katika uhalisia. Jambo ambalo nalo linatiliwa shaka na inatakiwa tuliangalie kwa umakini.

Mheshimiwa Spika, kwa nyongeza, nimefanya tafiti ndogo kujaribu kulinganisha gharama ya bima za ndege zetu ambazo ATCL inalipa, kwa kulinganisha na gharama za bima za kila mwaka ambazo Mashirika ya Ndege ya Nchi za Afrika Mashariki wanalipa. Takwimu hizo ni kama ifuatavyo: -

(i) Kenya Airways wana ndege 39 na gharama ya bima kwa mwaka ni dola za Kimarekani ni milioni 9.7 kwa ndege 39;

(ii) Rwandan Airways wana ndege 12 na gharama ya bima kwa mwaka ni dola za Kimarekani milioni 2.8; na

(iii) Shirika letu la Air Tanzania lina ndege 11, lakini gharama ya bima kwa mwaka ni dola za Kimarekani 5.9.

Mheshimiwa Spika, kwa hesabu za haraka haraka, unaona jinsi gani ambavyo Shirika letu la Ndege la Tanzania (ATCL) linalipa gharama kubwa kwa mwaka, kwa ajili ya bima za ndege ambayo haiendani na uwiano, yaani ukilinganisha na idadi ya ndege zilizopo na hii ni kwa kulinganisha na wenzetu wa nchi jirani kwa maana ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, bima za ndege kwa sasa hivi mkataba uliopo unakwenda mpaka mwezi Juni, 2023. Kwa hiyo kwa unyenyekevu mkubwa naomba kupendekeza kwamba, tuongeze nyongeza ya azimio katika mapendekezo ya Kamati hii husika, kuielekeza ATCL ifanye competitive tender zabuni kwa ushindani ili kuhakikisha kwamba tunakwenda kuokoa fedha za Serikali na umma. Maana hata taarifa ya Kamati imesema kwamba ATCL iko taabani kiuchumi. Sasa kama iko taabani kiuchumi wakati kwa upande mwingine tunalipa gharama kubwa kuliko inavyotakiwa kwenye gharama ya kila mwaka ya bima kwa ndege, hapo tunatakiwa tufanye jambo sisi kama Bunge ili kuhakikisha kwamba tunaokoa fedha za umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, liko pia suala la local content, ambalo hata Mheshimiwa Rais Samia Hassan, amekuwa akilisemea kwa mara nyingi na ushiriki wa sekta binafsi kwa Tanzania. Sasa Shirika la Bima la Taifa (NIC) hivi sasa ni kama lina monopoly. Kutokana na monopoly hiyo, NIC inakuwa na mamlaka ya kuamua kutumia single source international broker. Single source huyo pale ambapo inaelekea anaweza akatokea mbadala mwenye gharama ya chini, amepunguza kwa urahisi bilioni tatu kwenye quotation yake. Jambo ambalo naomba kwa unyenyekevu mkubwa tuone namna ya kuishauri ATCL, ihakikishe inatangaza zabuni za bima za ndege kwa kutumia ushindani na sio single source, kwa sababu single source inaweza ikapelekea mianya ya upotevu wa fedha za umma.

Mheshimiwa Spika, sisi kama Wabunge, tunao wajibu wa kuhakikisha jitihada za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan za kutafuta fedha na fursa mbalimbali kwa ajili ya nchi yetu na Watanzania hazififishwi kwa mianya hii ya single source. Kwa unyenyekevu mkubwa, naomba tutoe pendekezo hili la kuhakikisha kwamba zabuni za bima za ndege za ATCL zifanyike kwa competitive bidding.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili, ni matumizi ya TEHAMA. Hili nalo ni eneo ambalo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akilisemea kwa nguvu kubwa. Nimejaribu kutafakari katika uwekezaji wa miradi yetu mikubwa hapa Tanzania, nikifanya rejea kwenye SGR pamoja na mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere, ukifanya tathmini ya kujua ni makampuni mangapi ya Kitanzania ambayo yamepata zabuni za TEHAMA kwenye miradi ile, majawabu yake ni ya kusikitisha sana. Pia ukitaka kufahamu ni wataalam wangapi wa TEHAMA wa Kitanzania ambao wamepata nafasi ya kufanya na wenzetu wa nje waliopata zabuni hizo ili waweze kupata kile kitu tunachokiita transfer of knowledge, nayo utasikitika sana.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, naomba nitoe angalizo kwamba, kwenye miradi yetu mikubwa ya kimkakati, tunapotoa zabuni za TEHAMA kwa makampuni ya nje, tunajiweka katika hatari ya kiusalama wa mfumo. Suala la TEHAMA ni suala nyeti. Kwa mfano, ile kampuni ikiamua kuzima mtambo, sisi kama nchi tutafanyaje? Wakati hatutumii watalaam wetu wa ndani?

Mheshimiwa Spika, nikirejea kwenye suala la Sensa. Tumekwishajidhihirisha kupitia sensa. Shirika la Takwimu la Taifa limetumia wataalam wetu wa ndani na sensa yetu imeendeshwa kidigitali mpaka watu wa Mataifa ya nje wametusifia. Kwa hiyo, tunao uwezo wa kutumia wataalam wetu wa ndani.

Mheshimiwa Spika, tutoe maelekezo mahususi kuhusu Serikali kuweka jitihada pale ambapo kuna miradi ya kimkakati, hususani masuala ambayo yanaendana au yanaweza kupelekea masuala ya kiusalama, tuweke mbele kuhakikisha kwamba tunatafuta Makampuni ya Kitanzania ambayo yanaweza kutekeleza ile kazi au Makampuni ya Kitanzania yashirikiane na makampuni ya nje ili kulinda maslahi letu likiwemo suala la kiusalama.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kwa unyenyekevu mkubwa, nashukuru sana kwa fursa hii. (Makofi)