Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu. Naunga mkono hoja za kamati zote tatu ambazo zimewasilishwa na wenyeviti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naanza kuchangia; mengi wenzangu wameyasema. Serikali kama ni ya kusikia itasikia lakini kama itafanya kama ilivyozoea miaka yote kwamba tunasema mwisho hatimaye yanayotendewa kazi ni machache basi wataendelea na utaratibu wao kwa sababu labda wanaona unafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ripoti za CAG pesa zinapigwa kwelikweli, yaani watu wanatumia pesa kinyume cha utaratibu tena bila woga. Mimi nimejipa muda kidogo nikasoma. Ukiangalia ile ripoti ya Hesabu za Serikali za Mitaa, nakupa tu mfano wa maeneo manne halafu uone ni pesa kiasi gani ambazo zimeliwa na wajanja wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza CAG ile ripoti ya Serikali za Mitaa anasema matumizi yasiyo na manufaa, yaani kwamba yametumika tu, ukiuliza yamefanya nini hakuna manufaa yoyote ambayo yanaonekana kwa wananchi, milioni 664 na point, ukurasa wa 275, kasome utakuta kaeleza vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine malipo ya bidhaa na huduma zisizopokelewa. Watu wameandika tutatoa huduma hii, tutaleta vifaa hivi lakini havikupokelewa, shilingi ngapi bilioni 8.44 watu wamekula na mambo yako kimya. Malipo yaliyofanywa bila kudai risiti za electronic; tunaambiwa ukiuza toa risiti, ukinunua toa risiti; mimi mwananchi wa kawaida tu nikienda kwenye kituo cha mafuta, nikinunua chochote nadai. Lakini Serikali hiyo inayosisitiza wanafanya manunuzi risiti hakuna, shilingi ngapi; bilioni 6.07. Hapa sizungumzii namba tu nazungumzia pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka leo Mheshimiwa Deo Utumishi simuoni Mheshimiwa Jenista mimi nahudumia Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI); kila siku za Mungu tunakuja kufundishwa mifumo, kwamba kuna e-government lakini mpaka leo ripoti ya CAG siyo maneno yangu mimi leo sisemi ya kwangu. CAG anasema hivi mpaka mwaka unaoishia Juni kuna wafanyakazi wamelipwa ambao hawako kazini. Mifumo ipo lakini waliostaafu wamelipwa milioni 343. Mifumo ipo inajua Tunza unastaafu lini lakini unalipwa. Watoro kazini wamelipwa milioni 81 mifumo ipo Mheshimiwa Deo. Waliofariki wamelipwa milioni 63 mifumo ipo, wengineo, yaani ambao hawaeleweki tu. Hawa ambao walistaafu, watoro, ambao hawako kazini ni wengineo, sasa sijui CAG alikuwa na maana gani; maana hawa walikuwa wanarandaranda, tu wamelipwa milioni 68, na mifumo ipo na kitengo cha mifumo kipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nahudumia Utawala na Serikali za Mitaa ambayo ndiyo kamati yangu. Tumekwenda kuangalia mifumo, wataalamu wa mifumo wapo kwa nini haya mambo yanatokea? Maana watu wanapiga tu, huku tunasifia mama anaupiga mwingi anapita kutafuta hela huku watu wanakula na siku zinakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko kwenye ulimwengu wa sayansi na teknolojia. Leo tunaambiwa Kariakoo ilipoungua moto na nyaraka zote za mapato na matumizi zimeungua, yaani hazijulikani. Shilingi ngapi sasa hizo tunazungumzia? tunazungumzia bilioni 3.562; ni hela nyingi. Tupo tuna mifumo na kuna watu wanalipwa lakini tunaambiwa Kariakoo ilipoungua moto na mambo yote yameungua. Kwakweli kama taifa hatupo serious. Kwa sababu, sasa hivi wewe ukiwa na simu yako ikaibiwa unaweza ku-recover data zako; sikwambii kitu ambacho kinaingiza mapato mengi hivi kwa nchi. Unaambiwa soko la Kariakoo lilipoungua moto basi kila kitu kimeungua. Haya si maneno yangu ni maneno ya CAG, someni ripoti mtaona. Wameshindwa kuleta udhibitisho hizi hela ziko wapi, hakuna, vimeungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na MSD. Watu wamechangia MSD mimi nikasema ngoja kwanza nikasome.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Naibu Waziri Utumishi na Utawala Bora Mheshimiwa Deo Ndejembi.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpatia taarifa Mheshimiwa Tunza Malapo ambaye kweli Mheshimiwa ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, ambayo inatusimamia sisi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimtoe mashaka yeye na wewe Mwenyekiti na Bunge lako. Hiyo taarifa baada ya kuwa imetoka Serikali hii ya Awamu ya Sita, kwa kuwa ni Serikali makini sana, imehakikisha mfumo wa HCMIS, umetengenezwa kupitia Wakala wa Serikali Mtandao (e- GA), na tayari mfumo huo umeanza kutumika Mei, mwaka jana. Hivi sasa kuna kitu kinaitwa auto- termination. Mtu akishafika umri wa miaka 60 automatically anatolewa nje ya mfumo. Wakati CAG anafanya ukaguzi wake mfumo huu ulikuwa bado haujaanza kufanya kazi; lakini kwa sasa mtu yoyote anayetoka nje ya utumishi wa umma tayari kuna auto- termination.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii Mheshimiwa Tunza, iko makini sana chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, na yeye mwenyewe Mheshimiwa Rais ametuelekeza kuhakikisha tunakwenda kwenye mifumo zaidi na Ofisi yake hii ya Utumishi, nawe ni shuhuda tumekuonesha hata huu mfumo wa HMIS namna unavyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha taarifa.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Tunza Malapo, unapokea taarifa?

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo taarifa yaani ipo half half. Upande naweza kuipokea na upande siipokei. Siipokei kwa maana ipi? Hawa wanakuwa wana-exit meeting, yaani haya yote wangeelezana huko CAG asingeendelea kuyaleta. Yaliwashinda wapi kumweleza? Kwa hiyo, hapa ndiyo maana nikasema, leo siongea maneno yangu, naongea kutoka kwenye ripoti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hizi ni fedha za wananchi walipa kodi, kwa hiyo, ndiyo maana nasema, kwa upande mwingine kama mmeutengeneza mfumo, niwapongeze. Sina roho mbaya, nawapongeza mfanye vizuri, haya mambo yasijitokeze, kwa sababu hizi fedha zingeweza kusaidia mambo mengine. Hiyo ndiyo hoja yangu ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na MSD. Nimesoma ripoti ya CAG kuhusu MSD. Wenzangu wameongea vizuri tu. Sasa (MSD - Medical Stores Department), yaani Bohari Kuu ya Dawa Tanzania, maana yake Bohari, yaani ukisema tu neno bohari, ni kama godown, sehemu ambayo watu wanahifadhi au vitu vinahifadhiwa. Tunategemea nini? Tunategemea tukute wataalamu wa kumbukumbu, wataalamu wa kuhifadhi vitu. Kinachoingia mwanzo ndiyo inabidi kitoke mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenye ripoti ya CAG jambo la ajabu kabisa anasema hivi, halmashauri zinapelekewa dawa ambazo zimekaribia kwisha muda wake. Kwa nini zinapelekewa hivyo? Kwa sababu watu wa MSD hawana utaratibu mzuri wa kutoa dawa. Labda yeye ananunua huko anaponunua kwa wazalishaji, leo hii tunaongelea Novemba, dawa nyingine ananunua Januari, anaacha kuitoa hii ya Novemba iende kwenye halmashauri, anaenda kutoa ya Januari. Kitu kama hicho ninyi mnaamini? Binafsi siamini. Ninachoona, kuna madili yanapigwa. Labda wanaenda kununua dawa huko za bei nafuu ambazo zimekaribia ku-expire halafu wanafanya dampo halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakupa mifano michache, leo mimi nina ripoti tu ya CAG hapa na namba na kila kitu. Dawa zinazohitaji kuteketezwa mwaka huu ulioshia Juni, Shilingi bilioni 3.5. Bilioni! Nikaenda kusoma sasa, ni halmashauri gani hizo zinazoenda kuteketeza dawa? Katika hizo halmashauri 46, halmashauri nne zinatoka Mkoa wa Mtwara. Halmashauri ya Wilaya ya Masasi dawa za Shilingi bilion
188. Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Shilingi milioni 97, Hamashauri ya Mji wa Newala Shilingi milioni 119, Hamashauri ya Wilaya ya Tandahimba, Shilingi milioni 76. Hizi ni fedha. Dawa zenye thamani ya fedha hizi zinaenda kuteketezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikajiuliza, hivi kweli Wamakonde wenzangu wanavyoumwa, wanakwenda hospitali wanaambiwa dawa hakuna, leo unasikia dawa za fedha zenye thamani hiyo zinakwenda kuteketezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa nia ya dhati kabisa, tuongeze azimio lingine kwenye maazio ya LAAC, tuseme hivi, hawa MSD wasipeleke dawa halmashauri ambayo labda bado miezi sita ku-expire, wapeleke dawa ambazo zina mwaka, zina miezi 24 kulingana na shelf life ya dawa. Wanachofanya MSD wakishaona hawajafanya utaratibu mzuri, dawa zinakaribia ku-expire ili lile bomu lisiwalipukie wao, wanachukua mzigo wanapeleka halmashauri. Kwa hiyo, kule wanafanya dampo. Sasa halmashauri tuongeze azimio. Halmashauri zisipokee dawa ambazo zimekaribia ku-expire, waziache hapo hapo bohari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua mpaka moyo unauma. Unateketeza dawa za Shilingi bilioni saba! Mwaka 2018/2019 wameteketeza dawa za shilingi bilioni 7.3, mwaka 2019/2020 dawa za shilingi bilioni 1.5, hapo ilipungua, tunashukuru. Sasa maajabu na kweli mwaka 2020/2021 wanaenda kutekeza dawa za shilingi bilioni 3.5. This is not fair. Siyo sawa! Kwa hiyo, watu wa Bohari Kuu tunaamini ni wataalamu, kama ni wataalamu, wafanye mambo kitaalamu, hizi ni fedha za walipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanaumwa, wewe mwenyewe ni shahidi, ukiwa kama Mbunge, hivi umewahi kuwachangia watu matibabu mara ngapi? Halafu leo uambiwe dawa za fedha zote hizi zinateketezwa. Huu ni uzembe wa hali gani? Tuweke azimio kuhusu MSD. Unajua watu wanatufanya sisi kama hatujielewi, lakini sisi tunajielewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwenye Bodi ya Mikopo. Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu inafanya mambo, kuna mengine nimejipa muda nimesoma. Kulingana na sheria yao, wao wanatakiwa wa-support wanafunzi wanaosoma shahada, lakini kuna maagizo yanatoka Wizarani. Wizara ya Elimu walipieni wanaosoma Diploma, hiyo ndiyo ripoti ya CAG inavyosema. Sasa hayo ni matatizo, lakini CAG pia anakwenda mbele anasema, kuna wanafunzi karibia 500 wana-drop kwa sababu ya kukosa ada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani mwanachuo kasoma mwaka wa kwanza, mwaka wa pili anakosa ada, ana- drop. Kwa hiyo, tunaposema kwamba shule za msingi na sekondari wana-drop na Vyuo wana-drop. Wizara ya Elimu inashindwa kusimamia Bodi ya Mikopo. Wamewaacha pale wakati wajibu wa kuwasimamai Bodi ya Mikopo ni wa kwao, wasikwepe jukumu, wawasimamie. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)