Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Augustine Vuma Holle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru kwa nafasi hii nami niweze kuchangia kwenye hoja zilizopo mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kasulu Vijijini na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla kwa mambo mengi ambayo anayafanya, to be specific, mambo makubwa matatu: Jambo la kwanza ni ujenzi wa barabara za kiwango cha lami kwenye Mkoa wa Kigoma unaendelea kwa kasi kubwa sana, hizo ni barabara mbalimbali, pia ujio wa Umeme wa gridi ya Taifa katika Mkoa wa Kigoma ni historia kubwa na ya kuenziwa. Pia mpango wa kujenga SGR kuelekea Kigoma ambao bado upo kwenye hatua ya manunuzi ni jambo la kujivuna na la kihistoria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo nitaenda kwenye hoja ambazo ziko mezani. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja zote. Baada ya hapo nianze na Benki ya Kilimo. Naanza na Benki ya Kilimo kwa sababu asilimia kubwa ya Watanzania wamejiajiri kwenye sekta ya kilimo, hii ni sekta ambayo inabeba Watanzania walio wengi kuliko sekta yoyote ile.

Mheshimiwa Spika, mwaka huu kwenye bajeti tulitenga Bilioni zaidi ya 700 kwenye bajeti ya Kilimo ukiondoa Bilioni 150 ambazo zimetolewa kama ruzuku. Tume ya Umwagiliaji tulitenga zaidi ya Bilioni 361, sasa ukiangalia Wizara wamejipanga vizuri kuweka miundombinu vizuri sana kwenye upande wa umwagiliaji na sehemu zingine. Wanaweza wakajenga miundombinu vizuri kwa maana ya umwagiliaji, wao hawatalima wataenda kulima wakulima, lakini wakulima wetu hawa wa Tanzania uwezo wao wa kifedha ni mdogo mno.

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya benki nyingi zinatangaza kwamba zinakopesha wakulima lakini hazifanyi hivyo, benki nyingi hazikopeshi wakulima. Ni Benki moja tu ya Kilimo ndiyo ambayo imefanya kwa vitendo kuwakopesha wakulima kiwango kikubwa cha fedha, wengine wanafungua dirisha lakini ukienda wanakuambia hatujaanza kutoa mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nina ushauri, katika hizi Bilioni 361 ambazo zimetengwa kwa ajili ya umwagiliaji, kwa nini tusipeleke Bilioni 250 kwenye umwagiliaji halafu Bilioni 100, tukaenda kuwapa hawa TADB - Benki ya Kilimo ili wakulima kama Serikali ikiweka miundombinu vizuri, wakulima wawe na uwezo wa kwenda kukopa ili waweze kuendesha kilimo, otherwise unaweza ukajenga mifumo vizuri, miundombinu mizuri ya kilimo lakini baadae wakulima sasa wakawa wako weak halafu ikawa ni white elephant.

Mheshimiwa Spika, nitaenda kwenye zao la pamba. Mwaka 2019 kidogo tuingie kwenye mkwamo kwenye zao la pamba, nakumbuka vizuri ulikuwa Naibu Spika, wakati ule zao la pamba lili-drop sana duniani na tulikuwa tunaelekea kwenye uchaguzi, presha ilikuwa ni kubwa sana Kanda ya Ziwa, Wabunge wa kule walikuwa matumbo joto. Hivi inakuwaje, inakuwaje! Pamba hainunuliki huko chini. Serikali iliwaita wafanyabiashara wa pamba, tena ambao karibia wote ni Watanzania. Ilivyowaita iliwapa assurance kwamba wanunue pamba kwa bei elekezi ya Serikali halafu Serikali itaenda kuwa- compensate au kuwapa ruzuku. Mpaka tunavyoongea hivi toka 2019 mpaka leo 2022 hawa wafanyabiashara wanadai zaidi ya Bilioni 21. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kutengeneza mjasiriamali Mtanzania ambaye ataenda kwenye level hiyo ya kuombwa na Wizara aweze kunusuru hali, siyo kazi ndogo! Hawa waliopo wachache Watanzania tujaribu kuwalinda na kuwatetea. Serikali inapata kigugumizi gani cha kuwalipa fedha zao? Wakati wanawaita Serikali ilitumia maneno mazuri sana ambayo ni very promising, sasa kwenye utekelezaji, yaani kukopa ni furaha halafu kulipa ni matanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa iko sababu na iko hoja, lazima Serikali ichukue hatua. Tulipata nafasi ya kukaa na Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Kilimo, wanasema ooh! kuna vikao. Mimi nasema kama hawa watu walivyoitwa 2019 na wao wangesema ngoja kwanza tuna vikao, mwaka wa kwanza kikao, mwaka wa pili kikao, tungeendelea na benki yetu, hivi nani angeweza kutuondoa kwenye huo mkwamo? Iko sababu ya msingi na iko hoja ya haraka hapa, Serikali ihakikishe inalipa madeni hayo haraka iwezekanavyo ili kuweza kutowaingiza kwenye mgogoro wa kiuchumi hawa wafanyabiashara wetu wa Kitanzania wazalendo, ambao walitutoa kwenye mkwamo wakati ule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wenzangu wa Kamati yangu wamezungumza suala la mwingiliano kwenye taasisi hizi ambazo tunazisimamia Kamati ya PIC, tunalo Shirika la Marine Services ambalo zamani ilikuwa chini ya TPA lakini sasa hivi ni linajitegemea lenyewe, ziko mali za marine services nyingi ambazo TPA wanazing’ang’ania ziko kwao, inaifanya marine service iwe weak ishindwe kuwa na kipato kizuri, ishindwe kupanga mambo yake vizuri kwa sababu mali zake nyingi zimeshikiliwa na TPA.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilete hapa, kama ni point za kisheria tuweze kufanya mabadiliko ya kisheria ili marine service wapewe mali zao waweze kujengeka vizuri. Walikuja kwenye Kamati wanalalamika, wanaomba msaada.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu bodi za mashirika mbalimbali. Kwanza mimi na-discourage sana kuwa na bodi hizi za ushauri. Mimi nadhani ni vizuri, na kwa taasisi kubwa kama TANROADS, TANROADS ambayo kila mwaka tunawapa ma-trilioni ya shilingi hapa, lakini wana bodi ya ushauri tu. Ipo tofauti kati ya bodi ya ushauri na independent board. Hii bodi ya ushauri sana sana ni kumshauri Waziri tu basi, lakini hii independent inao uwezo wa kupanga vitu na kuvisimamia bila kuingiliwa na mtu yoyote.

Mheshimiwa Spika, sasa kuwa na hizi bodi za ushauri kwenye taasisi nyeti kama hizi hiyo kwanza mimi na- discourage sana. Hata hivyo, lipo suala la ucheleweshaji wa uteuzi wa bodi. Mimi nakumbuka Machi Mheshimiwa Rais alikuwa anapokea ripoti ya CAG, CAG akasema kwamba yako mashirika mengi ambayo hayana bodi. Mheshimiwa Rais alishtuka pale, akasema mimi nikiletewa kila kitu pale huwa hakikai hata siku mbili au tatu.

Mheshimiwa Spika, sasa ziko bodi nyingi ambazo zimekufa miaka mitatu au minne. Kuna sheria fulani hivi wanasema eti bodi ambayo ina zaidi ya watu 10 ikiisha muda wake eti majukumu yale anachukua Katibu Mkuu wa Wizara. Yaani Katibu Mkuu wa Wizara kichwa kimoja kianze kubeba vichwa 10 vya bodi nzima? ni mambo ya ajabu kabisa.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo bado amepewa mwaka mmoja kwa mujibu wa sheria, hata huo mwaka unaisha bodi haijateuliwa. Sasa nashindwa kuelewa kwamba nchi hii Tanzania kweli hatuna wajumbe wa bodi, watu milioni 61 hatuna wajumbe wa bodi na wenyeviti wa bodi ambao wanaweza waka-fit kwenye hizi taasisi ambazo hazina bodi?

Mheshimiwa Spika, ninaomba, kama tunataka kunusuru mashirika yetu ni lazima tuhakikishe kwamba tunapata bodi kwa wakati. Kwa sababu bila kuwa na bodi, tumeona mashirika yenye bodi na yasiyo na bodi utendaji wao ni tofauti kabisa.

Mheshimiwa Spika, lakini, baada ya kupata bodi, hata hao wenye bodi ukiangalia hakuna mfumo imara wa uwajibikaji. Shirika kupeleka gawio Serikalini yaani ni mpaka wajisikie. Hakuna sheria ngumu ambayo inawalazimisha kupeleka gawio; na ndiyo maana akisimama Mheshimiwa Rais akiwakaripia akitoa tamko kali kuhusu kupeleka gawio, gawio linapanda, asiposema gawio linashuka. Hatuwezi Kwenda namna hiyo, lazima tuweke utaratibu mzuri wa kisheria.

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Kairuki ulivyompa muda wa kusalimia, akasema anaweka mifumo mizuri wizarani pale ili hata akiondoka yeye, ibaki inafanya kazi. Sasa hata hizi bodi zetu hizi lazima tuziwekee utaratibu ambao utawalazimisha, kwamba mkishindwa kufikia level hii ya mafanikio kwenye shirika fulani basi bodi ivunjwe. Hata utaratibu wa kupata hawa watendaji wakuu wa mashirika tunaweza tukawaangalia pia.

Mheshimiwa Spika, tunaweza tukaweka utaratibu, mtu anatakuwa Mkurugenzi wa TANESCO ruhusu watu waombe, watu waombe ukurugenzi wa TANESCO halafu Mheshimiwa Rais apelekewe majina ateue; maana inawezekana labda ukateua mtu labda hataki. Maana kuna mtu mwingine unamwita kwenye Kamati, anakuja pale unaona yaani nia ya ndani ya kusaidia shirika hana kabisa, yupo tu pale anakula posho basi. Ukimuuliza mpango mkakati hana, kama ipo haitekelezeki, yaani hasaidii chochote Serikali. Mimi nadhani tuunde utaratibu waombe hawa watu, tutafute watu competent, waombe, wakishaomba baadaye apelekewe Mheshimiwa Rais kwa mamlaka yake ateue. Haya mambo wakati mwingine, maana tuko watu wengi kidogo…

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa nani kasimama, Mheshimiwa Mtaturu, Mheshimiwa Vuma Holle kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mtaturu.

T A A R I F A

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mchangiaji kwamba ni jambo zuri kuwa na bodi katika mashirika, katika taasisi kwani bodi hizi zina nafasi kubwa sana katika kutoa ushauri. Naomba achukue taarifa kwamba taasisi imara kama za Simba zina bodi ambayo inaongoza mambo mazuri.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa taarifa. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Vuma Augustino Holle unapokea taarifa hiyo.

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, mimi nashauri mmoja, kama utaratibu wa kupatikana kwa bodi umekuwa ni mgumu kidogo pale ambapo bodi zimemaliza muda wake, tumetoa ushauri hapa; labda wale wajumbe wateuliwe kwa muda tofautitofauti, si wako wanne, leo teua wanne, halafu mwakani teua wanne, ili kwamba hawa wanne wakimaliza wanne wabaki wana-save. Au tuletewe sheria tubadilishe, tuseme kwamba bodi hata kama ikimaliza muda wake kwa mujibu wa utaratibu, kama haijatumbuliwa basi iendelee kufanya kazi mpaka pale ambapo bodi nyingine itakapopatikana na si kuacha tu Katibu Mkuu pale eti ameshikilia. Kuna bodi zingine unashangaa wamemaliza vizuri unakaa hata mwaka baadaye wanarudishwa walewale, sasa maana yake nini?

Mheshimiwa Spika, mimi nadhani tuweke utaratibu, watu kama huwataki watumbue waondoke, lakini kama hujawatumbua muda wao umeisha hujaleta wengine wapya, Serikali iwaache waendee kukaa kama bodi ili waweze kuteua watu wengine.

Mheshimiwa Spika, nataka niguse kidogo kuhusu Bodi ya Mikopo. Pale Bodi ya Mikopo, mimi juzi nilikuwa napitia ripoti ya CAG, nikagundua hata walivyokuwa wanamgomea Waziri wao kwa kweli sijashangaa. Ukipitia ile ripoti ya CAG vizuri huwezi kushangaa kwa nini Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ilikuwa inamgomea Waziri wake, kwamba ile kamati yake hawataki kuipa ushirikiano, yaani huwezi ukashangaa.

Mheshimiwa Spika, watakuja kusema wenyewe kwa sababu umewaita. Lakini madudu yaliyoko kwenye ripoti ya CAG kuhusu Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ni jambo serious na ambalo mnahitaji kufanya hatua za haraka sana; na ndiyo maana hawataki kuchunguzwa maana ukiwachunguza utaona madudu yao. Lakini CAG ameshatusaidia kuyaonyesha yatima hawapati mikopo, maskini hawapati mikopo, wanatoa hela excess ambazo hawatakiwi kutoa, zaidi ya nilioni tano. Sasa unataka uambiwe na nani kwamba hawa watu hawafai?

Mheshimiwa Spika, mimi niseme, tunao utajiri mkubwa sana kupitia mashirika haya, hayawezi kuwa operated kama mashirika ya Private Sector lakini yapo mambo ambayo tunaweza tukakopa kule tukayaleta kwetu, tukabadilisha sheria zetu kama ndicho kikwazo ili tuhakikishe tunaweza kwenda kwa speed ambayo Mheshimiwa Rais anaitaka. Mheshimiwa Rais anasema kazi iendelee lakini yako mashirika ambayo hayaendani na kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja nashukuru sana sana. (Makofi)