Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote nizipongeze hizi Kamati tatu za PAC, LAAC na PIC na nimpongeze CAG wote kwa pamoja ametuonesha njia ya kupita na njia ya kusemea.

Mheshimiwa Spika, nakuwa na maneno magumu sana ya kusema lakini hata lugha ya kutumia naikosea, sijui nitafanyaje, yaani najiuliza maswali mengi sana kwamba hivi hizi nyimbo tunaimba tunamwimbia nani? Yaani tunaimba ili iweje?

Mheshimiwa Spika, nitatoa ripoti baadaye kwa kutumia mfano wa halmashauri yangu, lakini najiuliza wewe unasoma na sisi tunasoma vitabu kwamba, kazi ya Mbunge ni kuishauri Serikali, sasa na wewe ni mtaalamu wa sheria utakuja uniambie tukishauri, tukishauri miaka thelathini tunafanyaje, yaani sisi kazi yetu ni kuishauri Serikali sasa tumeshauri,tumeshauri,tunafanyaje? (Makofi)

SPIKA: Wacha nikusaidie, kazi yetu siyo tu kuishauri Serikali; kuna muda wa kuishauri Serikali, kuna muda wa kuisimamia Serikali. (Makofi)

Wakati tutakapokuwa tunajadili Mpango yale mapendekezo ya Mpango, tutakuwa tunaishauri Serikali, wakati huu wa kujadili ripoti ya CAG tunaisimamia Serikali. Kwa hiyo kama kuna jambo limeshauriwa, likashauriwa, likashauriwa, wewe umeliona ambalo unaona Bunge lifanyie maamuzi fulani ndio wakati wako huu. kwa sababu Serikali kwenye jambo hili na wao watakuwa wachangiaji kama mwingine, yaani haya yote yeliyosemwa na Kamati, yanayosemwa na Wabunge hapa watakaokuja kuhitimisha hoja ili Bunge lifanye maamuzi ni Kamati zetu, kwa maana ya Wenyeviti. Kwa hiyo saa hizi tunaisimamia Serikali, kwa hiyo endelea na mchango wako, hatushauri tu tunaisimamia pia. Karibu.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante, umenipa ufafanuzi mzuri. Sasa nitoe mfano wa Halmashauri ya Bunda ambayo ukienda kwenye chati ya kwanza kabisa kwenye jedwali la kwanza la ripoti hii ya LAAC, ni halmashauri moja tu kati ya halmashauri 184 yenye hati chafu ambayo ni hati mbaya. Sasa juzi wakati LAAC inaendelea nilienda kwenye Kamati ya LAAC nikakuta kwenye ile ripoti ya Kamati ya LAAC wameandika Bunda imepata hati isiyoridhisha, nikajiuliza mbona CAG amesema ni hati mbaya? Mkaguzi aliyekuja kutoka Ofisi ya CAG akaniambia kwamba hiyo hati mbaya hatutumii, tunatumia lugha nzuri ya kutoridhisha, lakini ripoti ya CAG nimeisoma na ripoti ya Kamati nimeisoma imeandika Bunda hati mbaya. Sasa najiuliza ukaguzi wa CAG wanaenda kule halmashauri, wanakuta mambo mabaya, wanakuja kwenye Kamati halafu wanaanza kulemba, hiyo nayo hapana. Kwa hiyo tuache, kama mambo ni mabaya ni mambo mabaya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilitaka nitoe mfano…

SPIKA: Mheshimiwa Mbunge wa Bunda, acha nikusaidie, siyo hati mbaya ni hati chafu ama inaitwa mbaya? Ama mbaya na chafu ni sawa? Hii inaitwa hati chafu na ndiyo ilivyoitwa huku, ndiyo inavyoitwa huku, kwenye taarifa, ni hati chafu maana mbaya na chafu ni vitu viwili tofauti. Endelea.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, sasa sitaki kwenda kwenye hiyo lugha kwa sababu nimesoma ripoti ya CAG imesema hati mbaya, nimesema ripoti ya LAAC imesema hati mbaya iliyoko hapa sasa hivi, kwa hiyo Kiswahili tuachane nacho tuendelee na ambayo nataka kusema mimi. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, 2000 ni majedwali hapa nasema utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi miaka iliyopita 2012/2013, ripoti kama hii ilienda Bunda kukawa na hoja moja ya kujibiwa, haikujibiwa 2012/2013. Mwaka 2013/2014, hoja moja haikujibiwa; mwaka 2014/2015 hoja mbili hazikujibiwa; mwaka 2015/2016, hoja moja haikujibiwa; mwaka 2016/2017, hoja tatu hazikujibiwa; mwaka 2017/2018, hoja mbili, ikajibiwa moja; mwaka 2019/2020, hoja kumi na tisa, zikajibiwa tisa; jumla kutoka miaka yote hiyo tuna hoja 27 Bunda. Tukitoka hapo wanasema hati ya ukaguzi zilizotolewa miaka mitatu iliyopita, mwaka 2018, hati isiyoridhisha; mwaka 2019, hati yenye mashaka; mwaka 2020/2021, hati isiyoridhisha.

Mheshimiwa Spika, sasa nataka kujenga hoja yangu kutokea hapo, kwamba sasa tukisoma ripoti za 2012/2013, 2013/2014 na 2014/2015, zote zina ushauri wa CAG na Wabunge na matatizo yako palepale. Sasa niseme tuchukue uamuzi mgumu sasa tuseme, kwa ushauri huu sasa, kabla sijaenda Bunda, tuseme hivi katika hoja za LAAC na PAC, Bunge liseme hivi idara yoyote, wizara yoyote, taasisi yoyote ya umma ambayo haikutekeleza maagizo ya CAG na Wabunge mpaka tarehe 30 mwezi wa bajeti zao tusipitishe, si ndio tunasimamia au tunasemaje sasa, kwa sababu sasa tunamwambia nani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme maneno mazuri hapa, kwamba CAG anaenda mbele ya Rais, anasema maneno mazito mazito umma unasikiliza, rais anatoa maelekezo tunasema vikao vya PAC na LAAC vitaangalia. Vikao vinakuja vinaangalia, vinaleta ushauri hapa, tunatoa ushauri miaka inapita, tunatoa ushauri miaka inapita, tunatoa ushauri, miaka inapita, ni lini sasa tutafanya maneno ambayo wananchi wanaweza wakasema tumechukua hatua.

Mheshimiwa Spika, naomba kwenye Bunge hili tuchukue hatua, ndiyo maamuzi yangu, popote ambapo kuna fedha imeliwa, ukisoma fedha zilizoliwa katika idara mbalimbali ni kichefu chefu. Watoto wetu hawana madawati sasa hivi, watu wanalilia shule za msingi kuna maboma, bado tuna matatizo ya maji, tuna matatizo mengi, tunamhurumia nani anayekula fedha za umma? Kwa nini watumishi wa Serikali wa Tanzania hawaogopi hela ya umma? Wenzetu waliotutawala hapa juzi tu, siyo tu kula hela ukisema uongo Bungeni umeondoka, ukileta kabajeti hakana faida umeondoka, hapo uongee nini sasa? Sisi watu wanaokula hela ni walewale, wanaokula hela ni walewale, wanaendelea tu, kuna nini kinaendelea hapa? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, sasa niende Bunda, Bunda nimekwenda kwenye LAAC, bahati nzuri Mwenyekiti aliyekuwepo ni aliyekuwa anaongea hapa, ukienda kwenye zile fedha za ile 4.4.2 haikwenda 41,461,000,000. Ukienda kwenye 20% za vijiji kurudishwa kwenye maendeleo 11,465,000,000 haikwenda; ukienda fedha za maendeleo 260,000,000 hazikwenda; ukienda fedha mbichi 96,000,000 zimeliwa kabla hazijaingia benki; tumepewa 1,000,000,000 na mama ya kujenga Halmashauri ya Wilaya, 626,62,000 wamepewa wazabuni, hawajaleta vifaa, yaani wamepewa tu nenda mkanunue, nenda mkanunue, bila ukaguzi wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, LAAC imeomba kwenda Bunda, naomba uwape ruhusa waende, wasimamie watakuletea madudu. Leo tunapozungumza hapa mama ametoa fedha 467,000,000 kwa sekondari mbili, karibu milioni mia sita na kitu, wamekwenda kwenye kiwanda cha dragoni, wamenunua bati moja 69,140 badala ya 52,000 tumeenda Madiwani, tumekwenda mpaka tumepata vielelezo vyote vya kutosha, tukawaambia watumishi rudisheni hela, hawajarudisha wanasema eti TAKUKURU imechukua taarifa inapeleka. Hivi hizi hela za umma zitaliwa mpaka lini?

Mheshimiwa Spika, leo ukimwambia mwananchi wa kawaida kwamba fedha yake ya hospitali imeliwa shilingi laki moja ni tofauti na kumwambia bandari imekula 30,000,000. Wananchi wanapopelekewa fedha na mama inawauma sana kuliwa kwa sababu miradi yao haitaenda. Sasa hivi vitu tunafanyaje kweli kama tuna Mawaziri, tuna nani, tunafanyaje? Hivi kweli tunamlilia nani kila siku hii Serikali? Mimi si nimwombe mama aniteue hata Waziri wa TAMISEMI jamani hata siku moja? (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hivi tunafanyaje sasa vitu vinaliwa vinaenda tunaangalia kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ya kwangu ndio hayo machache tu. Ahsante. (Makofi/Kicheko)