Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Nami niungane na Mheshimiwa Ezra Chiwelesa kwa hii hoja aliyoitoa.

Mheshimiwa Spika, sisi katika Kamati yetu tumeshauri katika bajeti ya mwaka huu na katika bajeti iliyopita. Tumeyaona na tumeyasikia malalamiko ya vijana wanaoomba mikopo kwa ajili ya kujiunga na elimu ya chuo kikuu. Ni kweli kabisa, sisi tumewaita watu wa Bodi ya Mikopo, tumekaa nao, tumeongea nao, tumeangalia vigezo wanavyovitumia katika kutoa mikopo. Inachanganya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanasema wanatoa mikopo kwa watoto waliofaulu vizuri, sawa, tunakubaliana nayo. Lakini wanatoa mikopo kwa watoto ambao wazazi wamefariki, yaani Watoto yatima. Kuna watu wengine wamepata mikopo wazazi wapo, kuna watoto wengine ni yatima hawapati mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kibaya asilimia 62 ya mikopo iliyotoka wamekwenda kuwakopesha vijana wanaosoma masomo ya arts. Ukiwapa watoto wanaosoma masomo ya arts wanapofaulu wengi wamekwenda mtaani kutafuta kazi hawana ajira. Kwa hiyo unakuta watoto asilimia 62 hawana ajira, maana yake ni nini, hawarudishi mikopo. Asilimia iliyobaki ni kama 20, wamewapa watoto wanaosoma masomo ya sayansi, asilimia tano ni wale ambao hawakuomba mkopo.

Mheshimiwa Spika, tumeshauri hivi, na mimi nilizungumza humu kwa niaba ya Kamati, kwamba watueleze ni shilingi ngapi inahitajika kwa mwaka kuwapa mikopo wanafunzi wote Tanzania wanaostahili kuingia chuo kikuu. Wakatuambia fedha wanayopata ni bilioni 570, lakini wakipata bilioni 800 watatoa mikopo kwa wanafunzi wote Tanzania.

Mheshimiwa Spika, tukaomba Serikali itafute hiyo bilioni 800, mtu yeyote anayehitaji kuingia chuo kikuu ana shida ya kifedha, no matter ni mtoto yatima au ana wazazi, kwa sababu kuna wazazi wengine hawana uwezo, wapewe mikopo watu wote waingie chuo kikuu wasome. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, elimu iende kutolewa, kwamba mzazi mwenye uwezo kumkopesha mtoto wako kuingia kuchukua mikopo, kumbuka kwamba akiingia kazini atakuwa na jukumu la kulipa mkopo ule. Kama hiyo elimu ikitolewa mzazi kwenda kuchukua mkopo iwe ni last resort, kwamba umekwama ndipo mtoto wako umuingize akachukue mkopo kwa sababu ule mkopo siyo wa mzazi, mkopo ni wa mtoto ambaye akishaingia kazini atastahili aulipe.

Mheshimiwa Spika, na la mwisho tukasema kwamba Bodi ya Mikopo kwa sababu ilianzishwa kwa ajili ya kusaidia wanafunzi kwenda kusoma ibadilishwe iwe commercial, wawe na utaratibu na mfumo mzuri wa kufuatilia ulipaji wa mikopo. Kwa sababu unafika sehemu wanakwama kukusanya madeni kwa hiyo wawe na utaratibu mzuri, ianzishwe kama ni benki ambayo itasaidiwa na Serikali kupewa ruzuku ili iweze kutoa mikopo kwa wanafunzi wote.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naungana na Mheshimiwa Ezra. Hali ni mbaya, inabidi Serikali iliangalie hili na mrudi kwenye maoni ya Kamati muweze kuhakikisha tunatafuta hiyo fedha. Kama ni Bunge kupitisha tutafute hiyo fedha ili wanafunzi wote Tanzania wapewe mikopo waende wakasome. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)