Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini

Hon. Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nami nipongeze hoja iliyotolewa na Mheshimiwa Ezra. Ni kweli kwamba, Serikali kuna sera ya wanafunzi wote wanaostahili kupata mikopo wapate mikopo. Kwanza hiyo ni sera kabisa kwenye elimu, wanastahili kupata mikopo wale wote wanaotimiza vigezo.

Mheshimiwa Spika, niliongea katika Bunge lililopita, nikasema kwamba kama tunashindwa kuwapa wote asilimia 100, basi afadhali wote wapate flat rate. Hivi unampa mtoto mkopo wa asilimia 30 wakati mnajua hawa watoto wanatakiwa kufanya research, wanatakiwa kulipa hiyo tuition, wanatakiwa kula vizuri; asilimia 30 inatosha nini? Nilishauri basi ikiwezekana watoto wote wapate flat rate ili idadi kubwa ya wanafunzi waweze kupata mkopo.

Mheshimiwa Spika, na hii ya kuwabagua watoto wengine wasipate mkopo eti kwa sababu wamesoma private si haki na si sawa. Kwa sababu mtoto anaposoma sekondari mkataba ni kati ya mzazi na shule, kwa hiyo pale mzazi anahitajika alipe ada, ule ni mkataba wa shule na mzazi. Lakini mtoto anapoingia chuo kikuu ni mkataba kati ya yule mwanafunzi wa chuo kikuu na chuo au na Serikali. Kwa hiyo hatuna haja ya kuweka ubaguzi, eti amesoma private asipate mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na watoto wengi walioniletea mimi maombi, eti wananiletea mimi maombi kama mwakilishi, wengi wametoka private, hasa huko KCMC aliposema Mheshimiwa Ezra. Wanaomba mikopo; SAUT wanaomba mikopo, Teofilo Kisanji wanakosa mikopo, na mara nyingi wakati wako karibu na mitihani.

Mheshimiwa Spika, hili jambo nimefurahi sana leo limeingia hapa. Umenisaidia sana Mheshimiwa Ezra; I salute you. Kwa hiyo tuangalie namna gani sasa tutajipanga, na vigezo vile ambavyo havileti haki viondolewe. Tutafute fedha ili sasa hivi watoto wote hao wapate stahiki zao ili waweze kusoma.

Mheshimiwa Spika, leo tunalalamika kwamba watoto wakimaliza vyuo vikuu hawafanyi kazi nzuri kwenye field. Ni kwa sababu sasa hivi watoto hawana hela za kufanya research, kwa hiyo hakuna ubunifu. Hawa watoto wana-copy tu vitu. Tunapata watoto wamemaliza vyuo vikuu lakini hawana ubunifu, ni kwa sababu ya hapa.

Mheshimiwa Spika, tuwekeze fedha kama walivyofanya Thailand, wamewekeza fedha kwenye elimu. Thailand ilikuwa ni nchi ya kawaida, maskini, leo Thailand inatupiga, Singapore inatupiga. Wamewekeza fedha kwenye elimu kuanzia kindergarten. Kwa hiyo tubadilike tuwekeze fedha kwenye elimu ili iwakomboe watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.