Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuunga hoja iliyopo mezani. Wakati naanza kuchangia mchango wangu naomba nirejee maneno ya Baba wa Taifa, Taifa la Afrika ya Kusini, ambaye ameshawahi kusema hapo, “Education is a most powerful weapon which, you can use to change the world.” Akimaanisha kwamba, elimu ndio silaha peke yake ambayo unaweza ukaitumia kuibadilisha dunia. Kwa muktadha wake huu ni nini?

Mheshimiwa Spika, sisi pia Watanzania pamoja na vizazi vyetu na hawa watoto ambao tunatarajia kuwasomesha, tunatarajia ya kwamba elimu ndio silaha mojawapo ambayo wao wanaweza wakaitumia kuibadilisha jamii yetu, lakini pia kuwa washindani kwenye soko la dunia huko tuliko. Tukiangalia hapa kwenye takwimu za sensa ambazo tumepewa jana pale na Mheshimiwa Rais, Milioni 61 ya Watanzania na hiyo Laki Saba, ukiangalia kwa uhalisia utagundua idadi kubwa ya Watanzania ni Watanzania ambao wana kipato cha kawaida kabisa. Maana yake asilimia kubwa ni wakulima, asilimia kubwa wanafanya shughuli ndogondogo kwa ajili ya kuendesha maisha yao ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ikiwa Watanzania hawa ni wa kawaida kabisa ambapo mtoto huyu hapati mkopo kabisa wa Chuo Kikuu, anapata mkopo chini ya kiwango au anaenda inafika hatua ameshadahiliwa kuanza masomo mpaka sasa hivi vyuo vimefunguliwa ni wiki ya pili, watoto bado hawajapata mikopo. Unajiuliza mzazi huyu ambae alikuwa akimsomesha mtoto wake kwa kuungaunga kwenye shule hizi za Kata kwa maisha magumu, sasa hivi ni wiki ya pili, mtoto labda amechaguliwa Dar-es-Salaam anatoka Mwanza Vijijini, mtoto amechaguliwa kwenda kusoma vyuo vilivyoko Mwanza ametoka huko Momba Vijijini, amefika na nini? Atalipia malazi nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wamemtaka atoe hela ya udahili ili aanze masomo. Mtoto huyu ambae Serikali imefuta ada kutoka O-Level mpaka sasa hivi A-Level, mzazi anapata wapi hela ya kumsaidia mtoto huyu kumdahili? Ada ni zaidi ya Milioni Mbili, mzazi ni mkulima wa kawaida ambaye analima magunia mawili au anachoma mahindi barabarani, anafanya usafi Mama ni house girl, Baba anaranda, anapata wapi ameachwa kwenye mkopo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninao ushauri katika jambo hili. Kwanza tunaomba Bodi ya Mikopo (HESLB) ivunjwe na ipitiwe tena. Ipo haja ya HESLB inapaswa kuchunguzwa kwanza, yapo malalamishi mengi sana ambayo wanufaika wa mikopo huko nyuma bado wanayalalamikia.

Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge hili Tukufu naomba niseme wazi ninaishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi, mimi ni mnufaika ambaye nilikopeshwa mkopo na kupitia Bunge hili mwezi wa Kumi uliopita nimemaliza mkopo wangu. Kwa hiyo, tafsiri yake kile changu ambacho mimi Serikali iliniwezesha, mtoto wa mkulima wa kawaida kutoka Momba, nikasoma na niko hapa na inawezekana isingekuwa mkopo ningekuwa nimeshaolewa saa hizi nina wajukuu hata Wanne kwa hiyo, tafsiri yake inawezekana hata watoto wengine sasa hivi wakikosa mkopo wataingia kwenye mazingira magumu, wataendelea kuteseka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, HESLB ivunjwe, ichunguzwe, ipitiwe upya tena, lakini yale marejesho ambayo watu wengine ambao wanarejesha wanaonekana wanabambikiziwa yapitiwe tena pia, tuweze kuangalia Je, yale marejesho yanayorejeshwa hayawezi kuwasaidia watoto wapya ambao wanaingia? Je, hiki kiwango ambacho tulikipitisha hapa Bungeni hakiwasaidii watoto wapya ambao wanatakiwa kunufaika na mkopo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu mwingine ni kuwa, wako watoto wengi ambao wanafika chuo mwaka wa pili na wa tatu, wanashindwa kufanya mitihani yao kwa kukosa ada. Ninaomba Wizara ifungue dirisha, Wabunge tukiwaletea watoto hawa na sisi wakati mwingine ni binadamu, tunasaidia misiba, tunasaidia wagonjwa, inafika wakati tunashindwa. Mtoto yuko mwaka wa tatu, ameshindwa kufanya mtihani, ameomba mkopo zaidi ya mara tatu ameshindwa, mwaka wa tatu mtoto anaacha masomo?

Mheshimiwa Spika, tu-assume labda wewe mwaka wa tatu ungeachishwa masomo sasa hivi tungekuwa hatuna Spika hapo ulipokaa. Mwaka wa tatu ungeachishwa masomo tungekuwa hatuna Waziri Mkuu hapa ndani. Tunawaomba Bodi ya Mikopo mfungue dirisha, mtoto anapokuwa mwaka wa tatu ameshindwa kufanya mtihani wake kwa ajili ya kukosa ada laki nne, laki tano, tunaomba jamani watoto hawa muwape nafasi waweze kumaliza mitihani yao, waweze kufanya mitihani waende wakahangaike huko barabarani. Tuje hapa tujadili mambo mengine kwamba ajira ni changamoto, lakini kama tunasema education is the best weapon in the world, let us give them the weapon, acha tuwape silaha wakapambane huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunawaomba sana watoto wasiache kufanya mitihani eti kwa sababu amekosa Laki Tano, amekosa Laki Sita. Hata sisi ni Wabunge wakati mwingine tunashindwa, siwezi mtoto afanye…

SPIKA: Ahsante sana dakika zako zimeisha Mheshimiwa.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Naunga mkono hoja iliyoko mezani.