Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii muhimu. Nianze kwa kusema naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Ezra kuhusiana na watoto wetu ambao wanakosa mikopo.

Mheshimiwa Spika, kama muda wa saa moja tu uliopita nilikuwa naongea na Mheshimiwa Venant wa Jimbo la Igalula. Juzi jumapili nilikuwa natoka Tabora nimepita pale nikasimama, kuna mgahawa fulani nikasimama. Nikakutana na suala kama hili hili ambalo tunajadili hapa, kuna mtoto amefaulu vizuri pale anakwenda Mzumbe. Sasa nilikuwa namsimulia na michango iliyopita pale nami ni mmoja wa waliochanga pamoja ya kwamba nilikuwa on transit. Ni mtoto wa kike ambaye na yeye amekosa mkopo na hajui kama atapata mkopo na amefaulu viuzuri sana.

Mheshimiwa Spika, huwa najiuliza kuna ile wanasema unauziwa mbuzi kwenye gunia. Hii Bodi ya Mikopo imekuwa ikitoa takwimu nyingi sana za namna wanavyokopesha wanafunzi mbalimbali. Vilevile tukienda kwenye uhalisia hasa vijijini wanafunzi wengi waliofaulu vizuri wanakosa mikopo hiyo. Sasa sijui huu utoaji wao wanaangalia vigezo gani? Sawa wanasema ufaulu na vitu kama hivyo, lakini hawa wanaofaulu wengi wanakosa mikopo.

Mheshimiwa Spika, hii inakatisha tamaa sana. Tume-promote sana watu kusoma, kuna shule mpaka kwenye kata sasa zimekuwa promoted watu wanasoma kwenye kata. Watoto wakike na hasa vijijini, vijiji kama vya kule kwetu kanda ya ziwa ambako watoto wengi wa kike walikuwa wanaolewa kabla ya umri wao, kwa sabbu walikuwa hawaendi shule. Sasa tumewa-promote wasome na kweli wanasoma na wanafaulu kweli, lakini hawapati mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni nini maana yake? Tunaanza kuwajengea tena ile tabia ya kuanza kurudi kulekule ambako sasa wazee watakuwa wanasema sasa hiyo shule yenyewe ina faida gani kwa sababu hata sasa mwanangu ukifaulu uwezi kwenda kokote? Kwa hiyo tunaanza tena kuwakatisha tamaa sisi wenyewe kwa kukosa utaratibu mzuri wa kuwapa mikopo. Hizi takwimu za juzi ambazo tayari sensa inaonyesha akinamama wako wengi zaidi, akinababa tuko wachache. Kwa maana nyingine muda sio mrefu nadhani akinababa watakuwa bidhaa adimu sana, kwa mujibu wa takwimu za sensa.

Mheshimiwa Spika, sasa watoto wa kike hawa ndio watakuwa wengi, ambao tunatakiwa tuwalinde vizuri kwa sababu huko mbele kwa data hizi, wapo watoto wa kike ambao watakosa hata kuolewa, lakini sasa wakose hata kazi au wakose elimu? Bora sasa hata wakipata elimu, elimu hiyo itawasaidia hata kama atakosa mwenza wake huko mbele, lakini ana kazi yake nzuri, huyu mtoto wa kike atakuwa yupo protected. Kwa hali hii tunayokwenda nayo sasa hivi si nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna malalamiko na hasa vijijini kwamba wamekuwa wakipewa upendeleo zaidi watu ambao wapo mijini, watoto ambao wapo mijini na ambao pengine ndugu zao wana uwezo ndiyo wamekuwa wakipata mikopo, malalamiko haya yapo. Sasa Bodi ya Mikopo wanapotoa taarifa zao, basi ikiwezekana watupe na za vijijini kwamba vijijini ni watoto wangapi ambao walikuwa wana-qualify mikopo, wameweza kupewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nazungumza hivyo kwa sababu malalamiko haya ya kwamba mijini na wale ambao wana uwezo watoto wao ndio wanapewa mikopo, itatusaidia sana kama Bodi ya Mikopo itakuja na data za wale wa vijijini, watoto wa mtu masikini kabisa ambao wameweza kupata hiyo mikopo ili tuendelee kuwa-promote watoto wetu waendelee kujua kwamba wakisoma watapata mikopo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nirudie tena kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Ezra, kwamba Bodi ya Mikopo iangalie kwamba kweli hicho kinachosemwa ndicho kinachofanyika? Malalamiko ni mengi na yanakatisha tamaa kwamba watoto wengi bado hawafaidiki na mikopo hiyo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hiyo, ahsante sana (Makofi)