Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Afya. Nina maeneo manne kama muda ukiniruhusu kwa ajili ya kuboresha na kuhakikisha kwamba tunaimarisha huduma za afya katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya kazi za mwanzo kabisa ambazo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Magufuli alizifanya ni kwenye sekta ya afya. Tulimwona alikwenda Muhimbili na kutoa maagizo na tuliona Mawaziri na watendaji wa Wizara wakihangaika kutekeleza maagizo yale. Kwa hiyo, watu wengi tulitarajia kwamba afya ingekuwa ni kipaumbele kikubwa sana kwa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuona bajeti ya Wizara ya Afya utaona kwamba, kimsingi licha ya kwamba bajeti ya mwaka huu imeongezeka kutoka bajeti ya mwaka jana, ambapo bajeti ya mwaka jana ilikuwa shilingi bilioni 446 na bajeti ya mwaka huu ni takribani shilingi bilioni 870 lakini bado bajeti ni asilimia tatu tu ya bajeti nzima ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu ina commitments kwa Abuja Declaration ya asilimia 15 ya bajeti kwenda kwenye afya lakini ukichukua shilingi bilioni 870 ukagawa kwa shilingi trilioni 29.5 unapata asilimia tatu tu ya bajeti ndiyo imeelekezwa kwenye afya. Ukienda ndani zaidi utaona kwa mfano, Serikali imepanga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa madawa, bajeti kwa ajili ya MSD shilingi bilioni 251, lakini katika fedha hizo shilingi bilioni 131 ni za kulipa madeni ya nyuma ya MSD. Kwa hiyo, kimsingi bajeti ya madawa iliyopangwa kwa mwaka huu ni shilingi bilioni 120 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi Serikali humu Bungeni ilitamka kwamba madeni yote ya MSD yamechukuliwa na Wizara ya Fedha. Serikali ilitamka hivyo mwaka juzi wakimjibu Mheshimiwa Margaret Sitta alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati. Serikali ikasema hivyo mwaka jana kwenye hotuba ya Serikali ya mwaka jana. Mwaka huu madeni yale yote yamerundikwa ndani ya Wizara ya Afya. Matokeo yake ni kwamba, bajeti ya Wizara ya Afya inaonekana ni kubwa lakini sehemu kubwa hasa kwenye madawa inakwenda kulipa madeni ya zamani ya MSD, kwa hiyo, kimsingi bajeti haijaongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza tuangalie uwezekano wa kuongeza bajeti ya Wizara ya Afya angalau ifikie asilimia tano ya bajeti nzima ya Serikali ambayo ni shilingi trilioni 1.4. Hiyo, ndiyo rai ambayo naitoa kwa Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kutokana na ufinyu huu wa bajeti kuna baadhi ya huduma ambazo Serikali imekuwa ikizitoa kwa msaada wa wafadhili hazifanyiki tena. Masuala ya damu salama yana tatizo kubwa sana sasa hivi kwa sababu wafadhili wamejitoa na Serikali haijaelekeza bajeti kwenye damu salama. Vilevile utafiti uliokuwa unafanyika pale Muhimbili kwa ajili ya watoto wanaozaliwa na sickle cell nao umeguswa kutokana na tatizo hili la bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ni ya nne duniani kwa watoto wenye sickle cell baada ya Nigeria, Congo, India, Tanzania. Tuna watoto 12,000 nchini ambao wana sickle cell. Kwa kipindi cha miaka kumi kumekuwa kuna taasisi inaitwa Welcome Trust ya Uingereza ambayo ilikuwa inafadhili huduma hizi na utafiti wa sickle cell pale Muhimbili. Watu wale wameondoa ufadhili wao na Muhimbili hapa tunapozungumza wamesimamisha huduma za sickle cell. Huduma ambazo zilikuwa zinaendeshwa na daktari wa Kitanzania, msomi ambaye amepata Awards kubwa duniani kwa ajili ya utafiti wake kwenye sickle cell.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunavyozungumza huduma ile imefungwa na yule ameambiwa aondoke pale Muhimbili kufanya huduma hiyo. Toka huduma hiyo imefungwa mpaka leo, kwa takriban mwezi na nusu tu watoto watatu wenye sickle cell wameshafariki kwa sababu nchi yetu haina clinic nyingine yoyote ya sickle cell hapa nchini. Kwa hiyo, leo watoto wakifika Muhimbili wanaambiwa nendeni Amana, Mwanyamala, Temeke wa mikoani wabaki mikoani lakini kule mikoani hakuna huduma hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilipanga fedha za utafiti one percent ya pato la Taifa ambayo inaenda takribani shilingi bilioni 50 hivi, Wizara ya Afya na Muhimbili waangalie utaratibu, wazungumze na COSTECH tupate sehemu ya fedha hizi kuendeleza utafiti wa sickle cell na huduma ya sickle cell na huduma hiyo itolewe bure kwa watu wenye sickle cell, vinginevyo tutaendelea kupoteza maisha ya watoto wetu ambao wanazaliwa wakiwa na sickle cell. Kwa hiyo, jambo hili naomba Wizara ilitazame kwa umakini sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hilohilo kwenye damu salama tuna tatizo wafadhili wamejitoa. Pia sasa hivi kuna mradi ambao unaendelea ambao unaendeshwa na Dkt. Othman kwa ufadhili wa mfuko wa GSM kwa ajili ya watoto wenye kuzaliwa na vichwa vikubwa. Mradi huu unafadhiliwa na wafadhili, mfadhili akiondoka na wenyewe utakuwa kwenye the same problem. Kwa hiyo, naomba Wizara ya Afya ijaribu kuona namna gani ambavyo tutaweza kushughulika na mambo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine kubwa ambalo tumekutana nalo kwenye Kamati na limeelezwa kwenye taarifa yetu ya Kamati na Mwenyekiti wetu, ni suala la watumishi wa afya. Tuna tatizo kubwa la watumishi wa afya. Takwimu zinatisha kuhusu watumishi wa afya na hasa watumishi wa afya kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali za vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunavyozungumza wahudumu wa afya vijijini asilimia 93 ni uhaba, Madaktari kwenye hospitali za wilaya takribani asilimia 70 ni uhaba, hawapo. Mwaka huu Wizara haijaajiri, ruhusa ya kuajiri imetolewa lakini mpaka sasa Wizara ya Afya haijaajiri. Kwa hiyo, naomba Wizara ya Afya ijaribu kuangalia ni namna gani itashughulikia jambo hili maana tunaoathirika sana ni watu ambao tunatoka mikoa ya pembeni na pembezoni ambapo Madaktari wakipangwa hawaji na matokeo yake inakuwa ni tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni pendekezo kwa Wizara ya Afya kuhusiana na bodi ya kitaalam ya watu wanaofanya huduma za physiotherapy. Bodi hii itaweza ku-regulate license zao na shughuli wanazofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ni bima ya afya. Nchi yetu hivi sasa ina Mfuko wa Bima ya Afya na baadhi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ina mafao ya bima ya afya. Nadhani imefikia wakati, nitatoa mchango huu kwa maandishi ili Wizara iweze kunielewa zaidi, tuunganishe ili pasiwe na Mfuko ambao wenyewe moja kwa moja unaendesha fao lile la afya. Mifuko yote ambayo wanachama wake wanafaidika na bima ya afya tuiunganishe wa-limit fedha zao NHIF ili tuwe na one unity, one composite ambayo ina-deal na bima ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taratibu za ILO ukichangia kwenye hifadhi ya jamii percent fulani inapaswa kuwa ni fao la afya. Kwa hiyo, leo kuna baadhi ya wafanyakazi wa Serikali kwa mfano, wafanyakazi wanaochangia PSPF, wanachangia PSPF twenty percent inakwenda mchango wa mwajiri na mchango wa mfanyakazi lakini at the same time wanachangia NHIF three percent yake, three percent ya mwajiri. Kwa hiyo, unakuta mfanyakazi anatoa michango mingi sana wakati uleule mchango uliokwenda PSPF ilitakiwa percent yake iende bima ya afya kwa ajili ya huduma za bima za afya na kwa kufanya hivyo tutakuwa tumepanua sana bima ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Afya waje Kigomba na Ruangwa, tuna mradi ambao tunafanya kwa kushirikiana na World Bank ambapo ndani ya miaka miwili tutakuwa na universal coverage health insurance. Hii itaweza kuwapa somo la namna ya kufanya katika nchi nzima kwa sababu ni lazima ifikie wakati nchi yetu watu wote wawe na bima ya afya. Kwa sababu matatizo ambayo tunayapata sasa hivi, allocation za madawa na kadhalika ni kwa sababu hatuna mfumo madhubuti wa bima ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, reforms ambazo tumependekeza na nitawaletea zingine kwa maandishi mziangalie. Najua Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla aliunda timu ya wachumi na madaktari kwa ajili ya kuangalia possibility ya kuunganisha mfumo wa bima ya afya katika nchi yetu na kupata afya ya jumla, nitaweza kuangalia namna gani tutaweza kusaidiana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishie hapo maana muda wenyewe ndiyo hivyo tena umekwisha au unaniongezea muda kidogo?