Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nami naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Eng. Ezra na imenifanya kufikiri sana. Hivi huu ni msaada, mkopo, huruma au upendeleo? Kwa sababu unashindwa kuelewa uiweke kwenye position gani?

Mheshimiwa Spika, mimi ninao watoto zaidi ya 100, acha hao waliosoma Msalato; amehangaika kwenye shule zetu huko vijijini, akafanikiwa kupata Division One. Ameomba mkopo mwaka wa kwanza, amekopa; wa pili amekosa, akija kupata, anapata asilimia 30. Sasa swali langu hapa bado najiuliza, huu ni mkopo ambao mtu ni haki yake kupata? Ni huruma, upendeleo au ni zawadi? Maana yake kama ni mkopo, imani yangu ni kwamba kila mwenye sifa ambaye amekuwa admitted kwenye university, na anaomba mkopo kwa sababu atalipa, ndiyo maana ya mkopo. Otherwise tukubaliane hapa, tubadilishe jina la hili fungu

Mheshimiwa Spika, mtu ambaye anaomba kukopa, atalipa. Halafu anayemkopesha, anasema sikukopeshi, nakupa asilimia 10. Je, huu ni mkopo, huruma, upendeleo au zawadi? Tutafute jina ambalo litafiti kwenye hili fungu, badala ya kulipa jina kubwa halafu kumbe hatuna uwezo wa kulisimamia jambo hili halafu tukakuta watoto wengi wanakosa haki ya kusoma.

Mheshimiwa Spika, kuna vijana kama wanne walikuwa wanasoma UDOM. Mwaka wa kwanza wakaomba mkopo wakakosa. Nikamfuata Naibu Katibu Mkuu nikamwomba anisaidie, naye akaniambia nipe majina. Akapeleka kule kwenye Bodi ya Mikopo naye akakosa. Mwaka wa pili wakaomba, wakakosa, wakaacha shule. Mwaka huu tena nimempelea Naibu Waziri kwenye simu yake.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi niko Bungeni, Mbunge mwenzangu nimemwomba awasaidie hawa Watoto, nawajua ni masikini, akaenda na yeye akaniambia waambie wa-appeal, wakimaliza waniambie. Waka- appeal wakakosa. Sasa najiuliza hii means test, ina-test nini? Kama amejaza fomu, imepitia process zote, ni authentic form, lakini bado sifa za kupata hiyo fedha hana.

Mheshimiwa Spika, na kama kweli Mheshimiwa Naibu Waziri alichukua yale majina akapeleka na amethibitisha kwamba wame-appeal na bado na yeye aliwapeleka wakakosa, sasa nilitaka nikushauri, kwanza turudi kwenye Hansard. Tulishauri hapa wakati wa bajeti tukasema, inawezekana kweli kwamba tumeweka utaratibu ambao watu tunajikuta tunashindwa kujua nani anahitaji. Mimi hata unaposema tusomeshe watu wa sayansi peke yake, mimi sikubaliani nayo. Nchi hii haiwezi kuongozwa na watu wa sayansi peke yake. Kuna watu wamesoma sheria, wamesoma masomo mengine, wana haki ya kupata mkopo na wana haki ya kuitumikia nchi hii na wana haki ya kuongoza nchi hii, hatuwezi kusema tuwape wanasayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuweke utaratibu ambapo itakuwa ni haki ya kila mtoto aliyesoma. Bado nashawishika kwamba utaratibu wa kupima vigezo vya kuwapa watoto mkopo, hautusaidii kuwapata watu wenye shida. Mtoto wangu akiomba mkopo, najulikana Kanyasu, utaninyima kwa sababu ni Mbunge. Nina Diwani wangu ambaye mtoto wake aliomba mkopo akanyimwa, kwa nini? Eti Diwani. Hivi Diwani ana uwezo wa kusomesha mtoto kwenye ada ya Shilingi milioni nne? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namuunga mkono Mheshimiwa Ezra, nadhani tuna shida ya kuutaza upya mfumo mzima wa ukopeshaji, na pengine inawezekana fedha tunazozitoa tunadhani ni nyingi kumbe siyo nyingi.

Mheshimiwa Spika, wakati wa Bunge lililopita tulipitisha bajeti hapa. Mtoto wangu anasoma Chuo Kikuu cha Mweka, akaniambia baba, hivi mbona ninyi wanasiasa wote ni waongo? Nikamwambia kwa nini? Mmepitisha Shilingi bilioni 500, huwa mnampa nani? Hapa nina watoto karibu 20 hawajapata mkopo. Sasa inaonekana wanasiasa wote waongo.

Mheshimiwa Spika, tufumue upya, tuangalie namna bora ambayo kila mtoto mwenye haki ataweza kusoma.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)