Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Sita na Mkutano wa Saba wa Bunge pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa kwenye Mkutano wa Tatu na Mkutano wa Nne wa Bunge

Hon. Dr. Eliezer Mbuki Feleshi

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Sita na Mkutano wa Saba wa Bunge pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa kwenye Mkutano wa Tatu na Mkutano wa Nne wa Bunge

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nikushukuru wewe kwa kunipatia fursa hii, pia napenda sana kuishukuru na kuipongeza Kamati ya Sheria Ndogo ikiongozwa na Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapongeza sana uchambuzi ambao umefanywa na Kamati pamoja na maazimio ambayo yametolewa. Sisi tunafarijika kwamba katika sheria mama nyingi tulizonazo takribani 446 na sheria ndogo zaidi ya 40,000; dosari ambazo zimeendelea kujitokeza zinaendelea kupungua kadri ya hatua mbalimbali zinavyozidi kuchukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kwa ushahidi ambao Kamati inapochambua inakutana nayo, inatufanya sisi Serikali/Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuona bado tunao wajibu wa kuhakikisha kwamba sheria zetu zinazotungwa kwa mujibu wa Katiba yetu na sheria zetu zinakidhi yale matakwa na malengo ambayo pale zimetungwa. Kwa hiyo, tutaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba dosari ambazo zimetajwa, zinaendelea kupungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Chamuriho katika mchango wake amedhihirisha hii kwa kueleza kwamba wamepitia sheria ndogo nyingi lakini dosari zikawa chache. Kwa hiyo, kati ya mambo ambayo Serikali inayafanya kwa sasa mojawapo ya Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inakamilisha mwongozo ambao utatumika kuongoza mamlaka zinazotunga sheria ndogo katika ngazi ya halmashauri, Mawizara na mamlaka zingine kwa wote ambao walio na dhamana tunaamini mwongozo huu pamoja tunaamini mwongozo huu pamoja na mambo mengine utajaribu kutoa maelekezo kwa mambo yale ya msingi ambayo kwayo wote walioko na dhamana wanatakiwa kuyazingatia, hili nafikiri mwongozo ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili utaendana na jitihada za Serikali za kuona jinsi ambavyo tutaendelea kutoa elimu kwa wote ambao walio na dhamana ya kutunga sheria ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaelewa kwamba sheria yoyote sheria mama nyingi mchakato wake unahusisha tafiti na mawasilisho katika hatua mbalimbali kitu ambacho ni tofauti kidogo na sheria ndogo, kwa hiyo tunaona upo umuhimu kama Waheshimiwa Wabunge walivyochangia kuona kwamba umuhimu wa kutoa elimu, lakini na hata kutafuta utafiti ni jambo ambalo litahitaji kuachwa nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ofisi yangu kwa sasa na Waheshimiwa Wabunge inamalizia kufanya usajili wa wanasheria wote walio kwenye huduma ya umma na mpaka kufikia sasa tuna wanasheria 2,550 na hawa wamo pamoja na hizi waliomo kwenye halmashauri na mwezi huu tutazindua Public Bar Association (Chama cha Mawakili wa Umma Tanzania). Lengo lake moja wapo ni kuhakikisha kwamba wanasheria wote tulionao kwenye huduma umma wanakuwa na kiwango kwa maana ya kuwa na elimu na kuongeza stadi zao za kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kupitia hatua tunazozichukua tunaamini tutaendelea kujitathimini jinsi ambavyo hatua tunazozichukua kwa kuhakikisha wanasheria walioko kwenye Halmashauri, walioko kwenye Mamlaka za Mikoa na walioko kwenye Mawizara pamoja na hata zile taasisi kubwa, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (Solicitor General) na Ofisi yangu kwa pamoja tuhakikishe kwamba kila mmoja wetu anatimiza wajibu wa kuhakikisha kwamba sheria zinazotungwa na Bunge hili basi ziwe zile zile na zenye ubora lakini na sheria ndogo zinazotungwa ziwe zinaendana na masharti mama yaliyo kwenye sheria kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda pia nitoe rai ofisini kwangu kuna mfumo wa kieletroniki ambao ukiingia kuna sehemu ya mrejesho, ningefikiri hili ni eneo mojawapo la kusaidiana kwa wale wote ambao wanahusika na kazi za kisheria na huduma za kisheria na changamoto za kisheria mambo mengine si ya kusubiri yakaenda na urasimu mrefu, haihitaji kuweka neno la siri yaani password kuingia kwenye ile fomu ya mrejesho na sehemu ya mwisho ya ile fomu ofisi yetu inapenda kujulishwa jambo lolote na maoni yoyote ambayo mtu anaweza akaandika na akapata mrejesho.

Kwa hiyo, hizi ni njia ambazo naamini nazo tutajaribu kuona, tunaamini sisi kwamba tukizitumia vizuri zitaongeza thamani ya huduma ambayo inatolewa na Serikali upande wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna jambo lingine ambalo nifikiri halijazoeleka sana kwa hizi sheria ndogo; kwa sheria mama mara nyingi mnaona Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge tunakuja na sheria na miswada ya sheria mbalimbali. Kwa sheria ndogo marekebisho mengi au kufuta sheria ndogo zilizokwisha kutungwa ni zile nyingi tulizopokea hasa kwenye Mawizara, naona kutoka halmashauri ni mara chache sana, basi ningetoa rai tu kwamba tusisubiri na kuelezea sana maumivu yanayotokana na dosari zile za msingi ziko kwenye sheria ndogo taratibu zingine za kufahamisha ofisi yangu, Wizara ya Katiba na Sheria na mamlaka zingine nafikiri zichukuliwe haraka kama walivyo madaktari wowote wanaotibu binadamu tusisubiri ugonjwa mpaka unakuwa mkubwa au kuna kuwa na madhara haki za watu kupotea bila kuchukua hatua ambazo kumbe tungepata taarifa tungechukua hatua ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naishukuru na kuipongeza Kamati kwa mapendekezo yake na mimi kama sehemu muhimu katika utekelezaji wa maazimio haya upande wa Serikali nitashirikiana na wenzangu wote wa Serikalini kuhakikisha huo muda walioutoa tutafanya linalowezekana kupunguza dosari zilizojitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)