Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Sita na Mkutano wa Saba wa Bunge pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa kwenye Mkutano wa Tatu na Mkutano wa Nne wa Bunge

Hon. Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Sita na Mkutano wa Saba wa Bunge pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa kwenye Mkutano wa Tatu na Mkutano wa Nne wa Bunge

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru na mimi kunipatia nafasi ya kuweza kutoa mchango wangu kuhusiana na suala zima la hizi sheria ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze Kamati ya Sheria Ndogo kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kwa niaba ya Bunge ama kwa niaba ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria ndogo imetueleza vizuri kwamba lengo la madhumuni ya kuwepo kwa hizi sheria ndogo. Tunapokwenda kutunga sheria kwa mfano sisi Wabunge, sisi Wabunge humu ndani wote si wanasheria, lakini Ofisi ya Spika imeamua kuwa na utaratibu kunapokuwa na Muswada, kunapokuwa na jambo lolote linalohusu sheria Kamati inayohusika either ya sheria inayotungwa kwenye Wizara yoyote ile Kamati kupatiwa fursa ya kupewa uelewa wa pamoja ili Bunge linapokwenda kufanya maamuzi ya sheria husika Wabunge wote waweze kuwa na uelewa wa sheria hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye halmashauri zetu Madiwani wetu ndiyo wanaopitisha ama ndiyo wanaotunga hizi sheria ndogo, lakini Madiwani wetu hawapati fursa ya kupitishwa ili waweze kupata uelewa wa hiyo sheria inayokwenda kutungwa ina madhara gani kwenye halmashauri hiyo, ama ina madhara gani kwa wananchi wa eneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, cha kwanza niiombe Wizara inayohusika na suala zima la halmashauri iweze kuona ni namna gani inakuwa inawapa semina Madiwani wetu ama inawapa elimu elekezi ya kwanza kabla hawajaanza kutunga hiyo sheria ili Madiwani wetu waweze kupata uelewa wa pamoja na wanapokwenda kutunga hiyo sheria iweze kuwasaidia wananchi na si kuwakwaza na kuwakandamiza wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna wanasheria pia wa halmashauri. Wanasheria wetu wa halmashauri pia kutokana na wingi na shughuli nyingi zilizopo ndani ya halmashauri na wao pia wamekuwa nyuma kwenye suala zima la utungaji wa sheria. Lakini pili, wamekuwa hawapati semina ambazo zinawasaidia kuendelea kuwaongezea uwezo ili waweze kulishauri Baraza vizuri na kwenda kutunga hizo sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pia niishauri Serikali kwamba waweze kuona sasa ni wakati umefika wa kuweza kuwapatia semina wanasheria wetu ndani ya halmashauri ili waweze kuendelea kuongeza uwezo na kuweza kuwasaidia Madiwani wetu kwenda kupitisha hizo sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na kanuni nyingi sana ambazo zinatungwa na halmashauri na kanuni hizi zinatofautiana kwa kila halmashauri na kwenye kila halmashauri inategemea Halmashauri za Mijini, Halmashauri za Majiji, Halmashauri za Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye Halmashauri za vijijini; waliopo wengi vijijini ni wakulima na wafugaji. Kwenye halmashauri zetu kuna kanuni ambazo zinatungwa suala zima la ukusanyaji wa mapato ambalo na wewe umetoka kulizungumza asubuhi ya leo. Mkulima amelima hajapewa mbegu na Serikali, hajapewa jembe na Serikali, mvua ya kutegemea Mwenyezi Mungu, hana chochote ambacho amewezeshwa, amelima ndani ya halmashauri yake, anatoa mazao yake shambani mkulima anaenda kukutana na geti limewekwa barabarani eti alipe ushuru wa mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatujakataa kuchangia maendeleo ya Taifa letu, lakini je, tunachangia kwa utaratibu upi? Mkulima aliyelima kwa jasho lake anatozwa ushuru anayekuja kununua mazao kwa mkulima anachajiwa ushuru mdogo sana, kwa mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba. Mkulima shambani anatozwa gunia shilingi 1,500 huko mashambani, lakini huyu mnunuzi ambaye amekuja kununua mazao anaambiwa yeye anapewa kibali cha kununua mazao jumla analipa shilingi 750. Sasa hivi vitu sheria zinakuwa kwa namna gani yaani mkulima aliyelima yeye ndiye anayezalisha kwenye eneo husika kanuni zetu ambazo Madiwani wetu huku wanazozitunga zinakwenda kumkandamiza huyu mwananchi wa chini halafu zinam-fever huyu mtu wa juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukija kwenye suala zima la mifugo kwenye halmashauri za vijijini tuna minada ya mifugo, hii minada ya mifugo inamtaka mfugaji anapotaka kwenda kuuza mfugo wake siyo maeneo kata zote zenye minada anapotoka kwenye Kata A kwenda Kata B kuuza mfugo wake ni lazima awe na kibali na kile kibali ni cha kumtambulisha yeye aweze kutambulika kwamba ule mfugo ni wa kwake na anahitaji kwenda kuuza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye halmashauri zetu wametunga sheria ya hizo kanuni za kum-charge mfugaji fedha ya kupeleka ng’ombe wake ama kuku wake ama mbuzi wake kwenda kuuza mnadani, halafu yule anayenunua kule hawam-charge, mfugaji yeye anakuwa charged, lakini mnunuzi akinunua yule ng’ombe anachukua ile risiti ya mfugaji ndiyo anatembea nayo barabarani na kwenye magari mpaka anafika anakowapeleka. Kwa hiyo, ukiangalia hizi sheria bado Madiwani wetu hawajawa na uelewa mzuri wa namna bora ya kuweza kutunga hizo sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna kanuni pia za Mawaziri, naomba nizungumzie Wizara ya Afya ni kweli kwamba wakina mama wajawazito wanatakiwa waweze kufika kliniki lakini pia waweze kujifungulia kwenye kliniki zetu, lakini ni ukweli usiofichika kwamba kwenye maeneo yetu yaliyo mengi bado hatujawa na zahanati za kutosha kwenye maeneo yetu, hatuna vituo vya afya vya kutosha kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mama huyu akitoka zaidi ya kilometa 20 ama 30 kwenda kutafuta hicho kituo cha afya ama zahanati ni mbali, wakati mwingine uchungu unapokuja anakuwa bado hajajiandaa wala hajui ni saa ngapi uchungu utafika, akijifungua anapotoka nyumbani anaenda anampeleka mtoto wake kliniki anapigwa faini na mimi kwangu halmashauri ya Wilaya ya Chemba mwaka 2020 nilikutana na hicho kitu wakati wa kampeni, ilikuwa mtoto mwanamke akijifungua mtoto wa kiume anakuwa- chaeged faini akijifungulia nyumbani akienda kliniki anakuwa charged faini mtoto wa kiume shilingi 30,000, mtoto wa kike shilingi 50,000 wakiuliza hizi ni kanuni tumeletewa, hii ndiyo sheria tunayo tekeleza sisi tumeletewa ili tuweze kutekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, muone kwamba wakati mwingine hivi vitu either inaweza hata haikupelekwa, lakini kwa kuwa wananchi wetu hawana uelewa wanakwenda kujificha watumishi wetu watekelezaji wa hizi kanuni na sheria wanaenda kuwaumiza wananchi wetu kwenye maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TAMISEMI suala zima la watoto wetu kupata chakula shuleni; hatukatai ni jambo jema sana ili kumpunguzia mtoto umbali ule mrefu wa kwenda na kurudi apate chakula shuleni ili aweze kuendelea na masomo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mzazi ana watoto wanne wako shuleni, shule imeamua kujipangia utaratibu na mbaya zaidi hawashirikishi kabisa wazazi wanakaa Kamati ya Shule kule, inapanga, inaanza kupeleka migambo huko chini kwamba mzazi ana watoto wanne anapangiwa kila mtoto apeleke gunia la mahindi kwa muhula, debe la maharage. Mzazi huyu anakuwa hana uwezo wa kuweza kuwahudumia hawa watoto wote apeleke magunia manne na debe nne za mahindi anaanza kulipa kwa awamu kidogo kidogo let say huyu wa kwanza kamlipia, wa pili hivyo ili aweze kupunguza huo mzigo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kusikitisha wazazi hawa wamekuwa wakifanyiwa vitu vya ajabu, mzazi anaenda anakamatwa na mgambo kwa nini hajalipa chakula cha mtoto, okay akikamatwa na mgambo hela ya mgambo anatakiwa alipe yeye 30,000 anaenda kwenye Baraza la Kata anaambiwa alipe fedha ya Baraza, akitoka hapo anatakiwa kupigwa faini na Kamati ya Shule eti ameshindwa kulipa chakula kwa ajili ya watoto kwenda kupata chakula shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hizi kanuni bado tuone ni kwa namna gani zinakwenda kufanyiwa utafiti ili tuweze kukidhi mahitaji ya wananchi wetu huko chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine hizi kanuni zote na sheria zote zinatungwa ili ziweze kuwasaidia wananchi wetu wasiweze kupotoka kwenye maeneo mbalimbali, lakini zitungwe sheria ambazo ni rafiki na kabla ya kutungwa tuwashirikishe watu husika ambao wanatekeleza hiyo sheria tusitunge sheria halafu mwisho wa siku watekelezaji inakuja kukutana nalo barabarani halafu mwisho wa siku inakuja kutuletea shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni kuhusiana na suala zima pia ya hizi sheria zetu na Kamati pia wamelisema, sheria zinatungwa wakishatunga kabla hazijatangazwa kwenye Gazeti la Serikali sheria zinaanza kutumika matokeo yake zinaleta hasara kubwa sana kwenye halmashauri zetu kwa sababu zikianza kutumika mtu anaamua kwenda kushtaki, akishtaki halmashauri ikipelekwa kule kesi tunaenda tunashindwa kwa sababu sheria kwanza haijatangazwa kwenye Gazeti la Serikali haikuwa tayari kwa matumizi. Kwa hiyo, mwisho wa siku tunaingiza halmashauri kwenye madeni makubwa ya kulipa gharama mbalimbali ambazo hazikuwa na sababu. Kwa hiyo. Mimi niwashauri pia Serikali waweze kuona kuelekeza halmashauri zetu zinapotungwa sheria hizi ndogo ndogo zihakikishwe zinaanza kutumika baada ya kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na ahsante. (Makofi)