Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata fursa hii kuchangia. Awali ya yote naipongeza sana Serikali kwa hatua ambayo wamefikia sasa kutuletea itifaki hii kwa ajili ya kuiridhia. Kipekee pia nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Sheria pamoja na timu yake kwa kazi nzuri ambayo wameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hii tunalolijadili leo lina umuhimu mkubwa sana katika kuhakikisha kwamba Jumuiya hii ya Afrika Mashariki inaendelea na haitakutana tena na madhila kama yale yaliyoipata ile iliyotangulia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia historia utakuta kwamba suala la umoja wa forodha katika nchi hizi ya Afrika Mashariki, lilianza hata kabla nchi hizi hazijapata uhuru; lilianza wakati wa mkoloni, likianza na Kenya na Uganda na baadaye Tanzania. Kwa hiyo, hata Jumuiya ya Afrika Mashariki ilipoundwa mara ya kwanza mwaka 1967 jambo kubwa ambalo lilikuwa linazingatiwa ni hapo kwenye masuala ya forodha, lakini baada ya miaka 10 ile jumuiya ikawa imeshindwa kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma sababu za kuanguka kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa miaka ile, zinatajwa nyingi, lakini mojawapo wanazungumzia habari za tofauti za mifumo ya kiuchumi katika nchi wanachama. Sasa mimi ukiniuliza nitasema, katika ushirikiano wa aina yoyote ile, tofauti na mifumo ya kiuchumi au kisiasa hazipaswi kuwa sababu ya kuanguka kwa jumuiya. Kuanguka kwa jumuiya kunatokana na kukosekana kwa mikakati ya kuweza kuzisawazisha zile tofauti ili nchi zikaenda kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ndicho tunachokizungumza hapa kwamba kwa kuwa madhumuni makubwa ya hizi jumuiya ni uchumi; tunazungumzia sawa siasa, jamii na nini, lakini kama jumuiya yoyote, hizi Reginal Integration, kama hai-address suala la uchumi lazima itaanguka. Kwa hiyo, masuala haya ya uchumi yasipowekewa mfumo mzuri wa kuyaendesha na kuyadhibiti, basi lazima anguko lake litakuwa karibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana utakuta mwaka 1999 tulipounda tena jumuiya mpya kama walivyoeleza waliotangulia kwamba hatua ya kwanza ikawa ni masuala ya Umoja wa Forodha mwaka 2005, ni suala la uchumi hilo; ikaja Soko Huria 2010, ni uchumi sasa tunaangalia mambo ya Sarafu ya Pamoja, ni uchumi pia, ndiyo sasa tuanze kuota hiyo ndoto ya Political Federation huko baadaye, lakini mpaka haya yakae stable kwanza ndiyo unaweza kufikiria hilo la kisiasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chombo ambacho kina-balance au kina- harmonize haya mambo huwa ni Mahakama. Mahali popote pale ukitaka mambo yaende bila migogoro, lazima uwe na Mahakama, kwa sababu vinginevyo basi unaachia watu waamue kwa kutumia mapanga. Sasa Mahakama tuliyonayo sasa hivi ambayo inaundwa na Ibara ya 23 na 27 ya Mkataba huu wa Afrika wa Mashariki, inashughulikia zaidi mambo ya tafsiri ya mkataba waliovunjwa ule mkataba; iwe ni nchi au ni watu binafsi, mamlaka hiyo iko ndani ya Mahakama hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, mamlaka hii haiendi katika kutoa maamuzi ambayo yana nguvu ya kisheria, ni binding kwa lugha ya kisheria, ni maamuzi ambayo ni matamko (declamatory) au ni ya kushauri tu (advisory). Sasa haya yanaweza yakaendelea kwenye upande wa siasa na jamii na haki za binadamu na kadhalika; lakini ukija kwenye uchumi, lazima kuwe na maamuzi ambayo ni binding, yaani yanaweza yakafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ibara ya 27 inaruhusu kwamba mahakama ile itakuja kuongezewa mamlaka kama ambavyo council itaamua na nadhani ndiyo kinachofanyika hapa. Kwa hiyo tunachokifanya hapa kiko ndani kabisa ya ule Mkataba wa East Africa kwamba mahakama sasa iongezewe uwezo katika mambo haya ya kiuchumi; Umoja wa Forodha, umoja wa hii mambo ya fedha ili kuweza kutoa maamuzi ambayo yanaweza kutiliwa nguvu ya kisheria yakafanyika. Kwa hiyo, nadhani kuridhia hili ni jambo la muhimu sana katika kufanya jumuiya hii isikubwe tena na madhila ya kuyumba au kuanguka kama hapo nyuma ilivyotokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hakuna jambo jema ambalo halina changamoto zake au halina tahadhari za kujiandaa. Naona hili ni jambo jema sana, lakini sisi kama nchi tunahitaji kutia nguvu zaidi kwenye uzalendo wetu. Unapoingia kwenye mambo ya mashirikiano na watu wengine suala la uzalendo linatakiwa liwe na kipaumbele sana. Kwa hiyo moja, tunahitaji sana kujenga nguvu kubwa zaidi ya uchumi wetu, yaani tujenge nguvu ya ushindani kwenye uchumi ili hata tunaposema Umoja wa Forodha na sisi tuwe na mambo ya kwenda kufanya kule kwa wenzetu. Isije ikawa ni Umoja wa Forodha wenzetu wakawa wanakuja kufanya kwetu, sisi hatuna access ya kwenda kule. Siyo access kwa sababu ya sheria, ila access kwa sababu ya uwezo, kwa hiyo tuwajengee wafanyabiashara wetu uwezo wa kushiriki katika uchumi katika biashara zinazokwenda nje ya mipaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuwajengea uwezo Watanzania kujua fursa zilizopo katika nchi za wenzetu. Ni kweli tunatakiwa kufanya jitihada sana wawekezaji waje kwetu, lakini pia na sisi tunahitaji kwenda kuwekeza kwenye nchi za wenzetu. Sasa hapa tunahitaji kuwajengea uwezo Watanzania, vijana wanaoinukia kwenye biashara ili wawekeze hapa na watoke pia nje wawekeze. Ni mabenki mangapi ya Tanzania ambayo yamefungua matawi nje ya nchi. Pengine wala siyo uwezo, baadhi ya benki zetu zinao, lakini ile kuona iko fursa pale inaweza ikawa ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunakwenda kwenye mahakama, mahakama ni sehemu muhimu sana ya biashara, kwa hiyo mtu akipata kesi yake anataka akawakilishwe na mtu ambaye atashinda, whether ana kosa au hana, anachotaka yeye ni kushinda kesi. Kwa hiyo uwezo pia wa Wanasheria wetu na Mawakili wetu ni jambo muhimu sana. Hili ni eneo maalum, siyo kesi za kawaida zile ambazo tumezoea kufanya, kwa hiyo Chama cha Wanasheria Tanganyika na hasa hasa Wizara ya Katiba na Sheria iratibu mafunzo na kuwajengea uwezo Wanasheria wetu ili waweze kushiriki katika mahakama hii, vinginevyo watatokea wafanyabiasha wataenda kutafuta Wanasheria nje, kwa sababu mfanyabiashara anachotaka yeye ni kushinda kesi, siyo mambo mengine ya wema wema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi nishukuru kwa kupata nafasi hii, kama nilivyosema nitachangia kwa ufupi, naunga mkono hoja kwa tahadhari hizo ambazo nimejaribu kuzitoa. Nashukuru sana. (Makofi)