Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki

Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi pia na mimi ya kuchangia Protocol au Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa uzima na kuwepo asubuhi ya leo katika Bunge lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki ina historia ndefu kidogo ambayo imetoka mbali. Ilianzishwa na Waasisi waliotangulia mbele ya haki na sisi leo tunaendelea kuiboresha zaidi kama ambavyo tumepata fursa hii siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jumuiya ya Afrika Mashariki ilianza mwaka 1917 ikiwa na nchi mbili ya Kenya na Uganda. Baadae mwaka 1927 Tanzania ilijiunga katika Jumuiya hiyo ikiwa na jina jingine kwa maana ya Tanganyika. Lakini Jumuiya hii ilikuja tena kuanzishwa rasmi kwa hizo nchi tatu ikitambulika kama Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1967 ambapo baadae iliendelea kushamiri na kunawiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1977 Jumuiya hii iliweza kuanguka. Sababu za kuanguka kwa jumuiya hii zilikuwa ni nchi wanachama ikiwemo Kenya kudai sehemu kubwa ya maamuzi. Pia jambo lingine la pili ilikuwa ni nchi ya Uganda kwa maana ya Dikteta Idd Amin kuvamia Tanzania, kuchukia kuona kama Tanzania inaingilia uhuru wa Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na historia hiyo yote, jumuiya hii tena ilianzishwa mwaka 1999 baada ya Wakuu wa Nchi kukaa na kuona kwamba kuna haja tena ya kuendelea kunyanyua jumuiya hii. Jumuiya hii iliendelea kwa wananchi wake kushirikiana kwa nchi tatu na baadaye nchi nyingine mbalimbali ziliongeza kama Burundi, Rwanda mpaka baadaye na Kongo juzi imejiunga. Hayo yote yanafanya jumuiya hii iweze kusaidia wananchi wake kuingia katika nchi yoyote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kufanya biashara, kazi, na pia ule ushirikiano wa kindugu, kisiasa kijamii na kiuchumi nao umeendelea kushika kasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kwamba jumuiya hii inaendelea kusonga mbele, Wakuu wa Nchi tarehe 2/3/2004 waliweza kusaini Itifaki ya Soko la Pamoja, lakini pia tarehe 30/11/2013 ilisaniwa pia Itifaki ya Sarafu ya Pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini naendelea kusema hivyo? Ni kuonesha kwamba sisi leo kuletewa itifaki kuisaini, siyo kwamba ni jambo la kwanza, bali hasa katika itifaki hii tumechelewa kufanya hivyo. Nadhani ni kwa sababu Tanzania ni nchi makini, ambayo watu wake wanafanya utafiti wa kina katika masuala mbalimbali, ndiyo maana tumechelewa kwa kiwango hicho, lakini bado tuko kwenye jumuiya na tumekuwa ndio wabeba jumuiya kwa sehemu kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunatakiwa kuongezea Jumuiya ya Afrika Mashariki nguvu kwa maana ya mamlaka? Tunatakiwa kufanya hivyo kwa sababu kwanza mkataba wenyewe unatutaka kufanya hivyo. Katika kifungu cha 27 kifungu kidogo cha (2) cha Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa ruhusa yako naomba kunukuu: “the Court shall have such other origina,l appellate, human rights and other jurisdiction as will be determined by the Council at a suitable subsequent date. To this end, the partner states shall conclude a protocol to operationalize the extended jurisdiction.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifungu hicho tunapewa mamlaka hayo ya kuweza kuongezea Mahakama hii mamlaka ili iweze kuamua haki kwa wanachama wote kwa maana ya nchi wanachama, kwa wananchi wetu; na kwa maana nyingine kwamba lazima wawekezaji wetu waweze kuamini nchi yetu kwamba imesaini mkataba kikamilifu katika kuhakikisha kwamba tunapata wawekezaji wengi zaidi na wananchi wetu wanaweza kupata haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hiyo tu, kabla ya hapo, suala la migogoro ya biashara ilikuwa inafanywa na nchi wanachama kwa maana ya Mahakama za ndani ya nchi wanachama. Sasa suala hili wakati mwingine linaleta changamoto kwa sababu inakuwa ni mgogoro wa maslahi (conflict of interest) katika Mahakama za ndani. Labda tuna kesi Uganda na nchi nyingine au mwananchi wetu wa Tanzania, obviously tutaanza kufikiri kwamba kama yule mtu wa Uganda atapewa haki, ina maana tutasema Mahamaka ya Uganda imetuonea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kuridhia itifaki hii ni faida kubwa sana kwetu kama nchi na wananchi wetu pale ambako tutakuwa na mashauri ambayo yanafanyiwa maamuzi. Kwa sababu tukienda mbali zaidi, utakuta shauri ambalo limefanyika Uganda linaweza likatolewa maamuzi tofauti, baadaye ikija Tanzania maamuzi tofauti, ikienda Rwanda maamuzi tofauti. Kwa hiyo, kama tutaiongezea Mahakama hii ya Afrika Mashariki suala la mamlaka kamili, itakuwa inatoa maamuzi ambayo ni moja tu katika Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kulikuwepo pia na wasiwasi ndani ya nchi yetu kwa maana ya wananchi wa Tanzania kwamba sisi kuridhia itifaki hizi inaweza kuchukuwa ardhi yetu. Hiyo ilikuwa ni mitizamo ya wananchi wetu wa Tanzania, lakini tunahakikishiwa ndani ya itifaki katika Ibara ile ya 15 ya Soko la Pamoja kwamba ardhi haitahusika katika itifaki hii ambayo inaridhiwa na Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaondoa kabisa wasiwasi kwa Watanzania kwamba ardhi itakuwa ni miongoni mwa maamuzi. Ardhi itabaki katika kuamuliwa na Mahakama za ndani za Tanzania, kama ambavyo imesemwa ndani ya itifaki yenyewe. Kwa hiyo, wasiwasi huo kwa wananchi wetu na Bunge lako Tukufu tuondokana nalo kabisa kwa sababu haitakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ya kuridhia itifaki hii ni kubwa sana na ninaamini kwamba Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wataridhia. Kwa sababu tukiridhia, wananchi wetu watakuwa na uhuru wa kuingia katika nchi yoyote kwenye Jamhuri hizi za Afrika Mashariki, kuingia na kutoka na kufanya biashara mbalimbali, watakuwa na uhuru wa kufanya kazi kama ambavyo hata sasa wanafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia watakuwa na uhuru wa kupata huduma mbalimbali katika Jamhuri hizo za nchi za Afrika Mashariki, kuwekeza mitaji mbalimbali. Kama walivyosema, tutakapokuwa tumesaini itifaki hii, wawekezaji wetu watakuwa na imani kubwa ya kuja kuwekeza Tanzania na katika nchi za Afrika Mashariki kwa sababu sasa wana kitu ambacho wanaamini kwamba Mahakama ya Afrika Mashariki itatoa haki kwa pande zote bila upendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nasisitiza kwamba tukumbuke kwamba Wimbo wa Jumuiya wa Afrika Mashariki ni kielelezo dhahiri shahiri, inatueleza kwamba tuilinde Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki. Maudhui ya wimbo huo yanaeleza kabisa kwamba tuna wajibu mkubwa wa kulinda Jumuiya ya Afrika Mashariki na kupitisha itifaki hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba Waheshimiwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wapitishe itifaki hii bila wasiwasi wala tashwishi kwa sababu sisi Kamati tumepitisha na tumechambua kwa kina, na tumeuliza maswali kadha wa kadha ili kujiridhisha kwamba tuna maslahi gani ndani ya itifaki hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)