Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki

Hon. Abdullah Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mahonda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naomba kutoa shukrani ya dhati kwa kunijaalia wasaa huu kuleta mchango wangu juu ya Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzo kabisa napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza wawasilishaji, Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Khadija Shaaban Taya ambaye amewasilisha report kwa niaba ya Kamati, kwa hakika uwasilishaji ulikuwa mahiri sana na wameeleweka. Tutajitahidi na sisi kuchangia vema ili tuende na mlolongo wao waliouanzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika tumechelewa kuipitisha hii Itifaki. Itifaki hii ina umuhimu mkubwa sana katika ustawi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ili nieleweke inabidi niweke kwa muhtasari Jumuiya ya Afrika Mashariki ni nini na mihimili yake ili watu watuelewe na kwa nini Itifaki hii ni muhimu sana iridhiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jumuiya ya Afrika Mashariki ina mihimili Minne. Mhimili wa kwanza ni Umoja wa Forodha (Customs Union), mhimili wa pili ni Soko Huria (Common Market), mhimili wa tatu ni Sarafu Moja (Monitory Union) na mhimili wa nne ni Umoja wa Kisiasa (Political Federation) lakini kwa sasa hivi tunazungumzia Political Confederation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua wasaa kidogo nigusie kwa muhtasari haya. Customs Union (Umoja wa Forodha), hivi Umoja wa Forodha maana yake nini? Haya maneno yanazungumzwa sana lakini bila kuyatambua na kuyafahamu ni vigumu kwa Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako Tukufu kujadili vema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Umoja wa Forodha ni jambo jepesi sana. Umoja wa Forodha ni mfumo ambao ndani ya hizi nchi Tano au Sita za Jumuiya ya Afrika Mashariki tukafanya tukawa na kitu kinaitwa common external tariff. Common external tariff ni nini? Kila nchi ikiagizia vitu kutoka nje ya nchi kuna vipengele vya kulipia kodi, Tanzania tuna vipengele vitatu. Chochote utakachoagiziwa nje ama utalipa zero percent ya kodi au asilimia 25 au asilimia 35. Vitu vyote vya nje vikiingia ndani lazima vilipiwe ushuru kwa vigezo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa common external tariff baina ya zile nchi tano, hivi vigezo vyote vinakuwa sawia katika hizo nchi zote tano. Yaani ukiagiza kishikwambi chako kutoka China au Mkenya akiagiza kishikwambi chake kutoka China au Mganda au Mnyarwanda au Mkongo kodi itakayolipwa ni ileile. Sasa common external tariff inatengeneza single customs territory. Eneo zima lile linakuwa na umoja wa forodha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mgogoro ukitokea nani awe msuluhishi? Ndiyo hoja tunayoizungumzia hapa. Msuluhishi hapa tunasema iwe East African Court of Justice wale ndiyo wataalam ambao wanaelewa taratibu na sheria na itifaki kwa undani ili wao ndiyo warekebishe, hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kila nchi kupitia Mahakama zake za nchi wanachama kuna uwezekano mkubwa sana tukapata maamuzi tofauti. High Court ya Tanzania ikaamua vyake, High Court ya Kenya ikaamua vyake, High Court ya Rwanda ikaamua vyake, kwa kweli kwa uhakika tutajivuruga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mhilimi wa pili, Common Market (Soko Huria) watu wanapenda kusema soko la pamoja, Hapana ni soko huria (free market). Ndani ya Jumuiya hii ya Afrika Mashariki soko liko wazi. Tumekubaliana sisi Itifaki hii ya mwaka 2004, vitu vitakavyotengenezwa ndani ya Jumuiya vikihama kutoka sehemu moja kwenda nyingine havina kodi. Utakachokitengeneza Tanzania ukakipeleka Kenya, Uganda, Rwanda hakuna kodi. Hali kadhalika utakachokitengeneza Rwanda, DRC, South Sudan ukikileta Tanzania hakina kodi, soko huria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa soko huria linatoa haki fulanifulani na hizo ni muhimu tuzielewe. Soko huria linatoa haki ya kwanza ya free movement of goods (bidhaa ziko huru), free movement of person maana yake nini? Maana yake uhuru wa wananchi kwenda popote ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Haki ya tatu, haki ya kuishi. Mwanaafrika Mashariki ana haki ya kuishi kokote ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki maadamu ana shughuli ya msingi ya kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhuru wa kufanya kazi sehemu yoyote, uhuru wa kusafirisha mitaji na uwekezaji sehemu yoyote, uhuru wa kufanya biashara ya huduma. Sasa, kukiwa na mkanganyiko baina ya nchi moja au nyingine juu ya uhuru au huru hizo, nani ahukumu? Itifaki hii inatuambia The East African Court of Justice ambao Majaji wake wanatoka kila nchi mwanachama, Watanzania wapo, Wakenya wapo, Majaji ambao wanazo sifa na uwelewa wa kuhukumu masuala hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mhimili wa tatu, Monitoring Union. Monitoring Union kidogo ina utaalam na ni kitu kikubwa kidogo. Monitoring Union ili tuwe tuna sarafu moja, chumi za hizi nchi Sita kwa pamoja lazima ziunganishwe ziwe moja (marketing integration). Unafanyaje chumi hizi kutoka kuwa sita iwe moja? Kuna vigezo tumejiwekea. Vigezo hivyo vinaitwaje? Maneno complicated lakini ni simple. Inaitwa macroeconomic convergence criteria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo vitu ni vitu gani? vitu vichache ni kama vifuatavyo: -


(i) Kila nchi mwanachama lazima inflation rate yao wai-control isizidi asilimia nane. Kiwango cha juu cha mfumuko wa bei usizidi eight percent.

(ii) Nakisi ya bajeti baada ya kujumuisha misaada isizidi asilimia tatu ya GDP ya Pato la Taifa.

(iii) Deni la Taifa lisilozidi asilimia 50 ya Pato la Taifa.

(iv) Akiba ya fedha za kigeni isiyopungua mahitaji ya miezi minne na nusu.

(v) Nchi wanachama lazima waweze kuweka hivi vigezo kwa miaka mitatu mfululizo ili waweze kuingia kwenye sarafu moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo ndiyo tutapata marketing integration. Eneo lote lile likawa kama sehemu moja na tukaweza kuwa na sarafu moja. Sasa, mtazamaji ni nani wa kusema bwana nchi fulani kidogo hapa imelegalega? Lazima kuwe na taasisi moja ya kuhakikisha haya yote yako sawa. Kama kuna mgogoro lazima taasisi hiyo moja ya katikati itatue huo mgogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika Jumuiya ya Afrika Mashariki ni jambo nyeti sana. tunalichukulia poa lakini siyo poa. Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa upana wake ina dhamira ya kutufanya sisi, chini Kusini mwa Jangwa la Afrika kuna chumi kuu mbili, wengine wote wadandiaji tuu. Chumi kuu mbili, Nigeria in West Africa na South Africa Kusini kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Jumuiya ya Afrika Mashariki mawanda yake mapana ni kutengeneza chumi kuu Tatu. Nigeria na wenzake ECOWAS kule, South Afrika na wenzake Kusini, Tanzania na Afrika Mashariki. Major geopolitical purpose tunataka kuwa katika miongoni mwa nchi Kusini mwa jangwa la Afrika ambao tuna chumi kubwa kuendeleza maendeleo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo kuyagusia, mwisho kabisa napenda sana kuunga mkono hii hoja na napenda kuwaomba Wabunge wenzangu waiunge mkono hii hoja bila ukakasi wa aina yoyote, kwa sababu ya maslahi mapana ya Tanzania ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)