Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

Hon. Amb. Dr. Pindi Hazara Chana

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa kwanza kuunga mkono Itifaki hii ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya mwaka 2004.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maliasili na Utalii ni mdau mkubwa sana katika masuala haya. Ninampongeza sana kaka yangu Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri lakini pia niishukuru Serikali kwa kutuletea Itifaki hii. Itifaki hii haijachelewa imekuja wakati muafaka, kwa kawaida kabla ya kuridhia huwa tunakuwa na mambo mengi sana ya kuangalia na kujiridhisha kwa hiyo, niseme tu kwamba imekuja muda muafaka na muda muafaka ni sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumepata watalii wengi sana, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan Amiri Jeshi Mkuu kwa kutuongoza vyema na amani ndani ya nchi hadi sasa tunapata watalii wengi. Nimekuwa nikisema kwamba watalii hawa wanakuja Tanzania siyo tu kwa kuwa tupo kwenye ramani ya dunia lakini kabla ya watalii kufika wanaangalia vigezo vingi. Kuna suala la uongozi bora, siasa safi na political stability ni miongoni mwa vigezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo nchi zingetamani sana kupata watalii lakini watalii kabla ya kwenda wakiona nchi labda ina vita, ina machafuko wanasema huko hatuwezi kuenda. Sisi tumeingia kwenye rekodi ya dunia kama kisiwa cha amani, tuko kama kisiwa cha amani kutokana na uongozi bora wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ndiyo maana hivi leo unakuta watalii wanaingia kupitia mipaka yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Iwe ni mipaka ya nchi kavu wengine wanatumia njia mbalimbali za ndege na kadhalika lakini tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na uzinduzi wa ile program ya Tanzania (The Royal Tour) na sasa tutakwenda awamu ya pili ya uzinduzi wa (The Hidden Tanzania) tunamshukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Itifaki hii yako maeneo ya kubadilishana taarifa, yako maeneo ya mashirikiano imeeleza vizuri sana Itifaki hii. Inasema kwamba we are determined to ensure Africa active participation, corporation and coordination with the international community in its determine efforts, combat and to eradicate masuala ya ugaidi. Haya ni masuala muhimu sana na niombe Bunge hili turidhie kwa kauli moja kwamba, Itifaki hii ya kupambana na kuzuia ugaidi ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepewa dhamana pia ya kulinda na kuendeleza misitu, lazima tuwahakikishie Watanzania wasiopungua takribani Milioni 55 tunasubiri takwimu za sensa, kwamba misitu yetu iko salama. Katika Itifaki hii imesema tutaendelea kubadilishana taarifa. Iko misitu ambayo inafanana na kushirikiana katika nchi zetu za SADC. Kwa mfano kuna misitu inaitwa Miombo hii ni misitu ambayo iko maeneo yetu ya Nyanda za Juu Kusini na inakwenda hadi nchi za SADC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo mengi sana ya misitu tunapakana na nchi mbalimbali, hasa misitu hii kama jinsi ambavyo misitu yetu ndani ya Jamhuri ya Muungano iko salama ni lazima tubadilishane taarifa, kwamba hii misitu ya nchi jirani na kwenyewe kuko salama au kuna changamoto? Kwa hiyo, Itifaki hii inapokuja itatusaidia kutoa mashirikiano kati ya nchi zetu, nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, nchi za SADC kuona kwamba maeneo yetu ya maliasili na utalii yapo salama. Kwa hiyo, Itifaki hii ni muhimu, kupitia Itifaki hii itatusaidia kwanza kukabiliana na masuala ya ugaidi, kukabiliana na masuala yote ya machafuko lakini kikubwa kama nilivyosema hapo awali ni suala zima la kubadilishana uzoefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ugaidi kwa kawaida unakuwa ni planned and organized, sasa tukiweza nchi za Afrika kuja pamoja kuelimishana, kukumbushana namna bora ya kudhibiti masuala haya ya ugaidi itatusaidia sana. Kwa hiyo, nimesimama hapa kuunga mkono hoja hii, kuunga mkono Itifaki hii na niombe kwamba Itifaki hii imekuja wakati muafaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa utalii unachangia takribani asilimia 17 ya Pato la Taifa. Utalii unatoa ajira takribani milioni 1.5 na fedha za nje takribani asilimia 25, nusu ya eneo letu la Jamhuri ya Muungano ni misitu. Maeneo haya ya misitu mazingira ya utalii, lazima tuwahakikishie umma na Jumuiya ya Kimataifa kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo salama karibuni katika masuala yote ya utalii. Iwe ni utalii katika fukwe, utalii katika hifadhi mbalimbali katika mapori yetu na Ikolojia zote kwamba Tanzania tuko salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha jambo hilo hivi sasa tumekuwa na mikutano mingi sana na haya ni mazao mapya ya utalii, mwezi wa Oktoba tutakuwa na mkutano wa United Nations World Tourism Organization, huu ni mkutano ambao utaleta wadau wasiopungua 600. Miongoni mwa checklist ambazo wanakuwa nazo ni kujiridhisha kwamba huko tunakokwenda wako salama? Kwa hiyo, kwanza wameshajiridhisha tuko salama lakini Itifaki hii itakuwa ni moja ya silaha ya vitendea kazi ambavyo tutaweza kulinda na kuendeleza usalama wetu ambao tunao. Kwanza, kwa kuwaelekeza nchi nyingine ni namna gani unaweza kufanya kudhibiti masuala haya ya uhalifu na wao wawe salama kama Tanzania tukitambulika kama ni kisiwa cha amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Tanzania tumekuwa mfano wakati wa kupigania uhuru katika nchi za Kusini mwa Afrika, kupitia Baba wa Taifa Mheshimiwa Nyerere alikuwa akitoa maelekezo kwa nchi zote za Kusini na hapa tulikuwa tunaweka makambi ya usalama. Kwa hiyo, suala hili la ugaidi kukabiliana nalo tumekuwa tukilidhibiti tangu wakati wa uhuru Tanzania imekuwa ni sample ndani ya Afrika, Tanzania imekuwa ni mfano bora. Kwa hiyo, leo tunapopitisha Itifaki hii ni wakati muafaka na ninaomba nichukue nafasi hii kwa kweli kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja hii. Ahsante sana. (Makofi)