Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana nami kupata nafasi ya kuchangia hoja iliyopo Mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja hii ilipita toka mwaka 2004 na nchi yetu ilisaini, lakini leo, miaka 18 baadaye, inaletwa Bungeni kwa ajili ya kuridhia. Ni hoja muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niwaambie Wabunge wenzangu, kama nchi, tunakosea sana tunaposaini mikataba mbalimbali ya Kimataifa, lakini ukifika wakati wa kuridhia na kupitisha Bungeni mnaleta kwa kuchelewa. Mmekosea sana, miaka 18 ni mingi sana. Mheshimiwa Waziri, kwa kweli umelichelewesha Taifa letu kuweza kusimamia nafasi hii ambayo leo tunataka tuifanye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi nimesikia Wabunge wenzangu wakiwaomba Wabunge waweze kuipitisha na kuiridhia. Ilitakiwa tuiridhie miaka 18 iliyopita. Hivyo basi, ninaamini leo, sote kwa umoja wetu, tutaipitisha ili tuweze kuisimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, itifaki hii ni ya muhimu, kama nilivyotangulia kusema, lakini nitaisema kwa upande wa pili. Sisi kama nchi tunapoenda kuiridhia, tunaomba tafadhali sana isimamie haki za binadamu. Kwa sababu itakapopitishwa, isichukue wale ambao ni watu wametuzidi kisiasa, wametuzidi kwa mambo mbalimbali ya kibinafsi wakati mwingine, kiongozi aliye madarakani au chama kilicho madarakani kikaamua kukandamiza watu kwa kupitia itifaki hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba itifaki hii itakapopitishwa, watu wafuatiliwe kiuhalali, wasimamiwe kama ni magaidi wafuatiliwe bila kuwabambikia. Kwa sababu tukiacha wazi watu wengi sana wasiokuwa na hatia wataweza kuhukumiwa, na baada ya miaka mitano, 10, 15, tunakuja kusema hawakuwa magaidi, tunawaachia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa njia hiyo hiyo kuna kipindi cha hapo nyuma watu wamefilisiwa mali zao, wamefungiwa akaunti zao za benki, wameshikiliwa pesa zao zisitumike mpaka uchunguzi uishe. Tunaomba itifaki hii ikasimamie haki za watu kama hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana, Ibara ya 18 ya Katiba inataka uhuru wa kujieleza, uhuru wa kutoa mawazo. Tunaomba itifaki hii isije ikawabana wale watu ambao wanatoa mawazo yao kwa ajili ya nchi yao, wakiwa wanatoa mawazo kwa ajili ya mambo mbalimbali yakiwemo ya kisiasa na ya kijamii, wasihukumiwe kama ni magaidi. Tunaomba ibara hii iwalinde na isimamie haki za hao watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinyume cha kufanya hayo, itifaki hii itaondoa amani na kuweka watu katika makundi, kwamba kuna watu wanaostahili kusema kitu fulani na kuna ambao hawastahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile hii itifaki pia iwashike wenzetu wa Jeshi la Polisi, waisome vizuri na kuiangalia. Kifungu cha tatu cha wajibu wa nchi washirika, kwa maana ya sisi ambao tunaingia itifaki hii, kipendele (a) kinasema hivi: “nchi mwanachama lazima ichukue hatua zote za kulinda haki za msingi za binadamu na kuhakikisha watu wake wanalindwa.” Watu wasipigwe, watu wasiumizwe wakiitwa magaidi wakati bado haijachunguzwa kama kweli hao watu ni magaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba ndugu zetu Polisi, maana yake wao watakuwa karibu sana na sheria hii na ndio watekelezaji kwa asilimia kubwa. Wasimhukumu mtu, hata kumtoa kwenye magazeti kama ni gaidi wakati bado hajathibitika kuwa gaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia habari za haki na umoja wa Watanzania. Tunaomba sana, itifaki ni ya muhimu, na ni vizuri kama walivyosema waliopita, nchi yetu inaingia kwenye uchumi wa kati, na kama inaingia kwenye uchumi wa kati, tunahitaji kuwa na amani na ulinzi, hata wawekezaji wanavyokuja kuwekeza wanajua tunakwenda sehemu salama. Mwisho wa siku tusiitumie vibaya tukafanya vibaya, hasa inagusa wanasiasa kwa sababu wanasiasa watakapoguswa, siasa ni hisia. Unapomkamata kiongozi wa kisiasa au mtu ambaye ameshindwana na ninyi kwenye mambo ya kisiasa mkamsingizia mambo ya ugaidi, amani itatoweka, watu hawatasimamia shughuli za kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba itifaki hii ipite. Nami nawaomba Wabunge wenzangu tuipitishe, lakini Serikali iliyopo madarakani ihakikishe itifaki hii inakwenda kusimama kwa haki kwa magaidi wa kweli na wala siyo magaidi wa kubambikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. (Makofi)