Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia na mimi fursa niweze kuchangia katika hoja hii muhimu ambayo ipo mbele yetu. Nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kuwa uwasilishaji mzuri na pia hata Mwenyekiti wetu wa Kamati, Mheshimiwa Kawawa, naye amewasilisha vizuri na kimsingi taarifa hiyo imesheheni na mawazo yaliyopo kwenye taarifa ile kwakweli hata sisi kama Kamati tuliyajadili na tumeyaafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninasimama hapa kutoa mchango wa ziada kuhusu hoja hii ya Azimio la kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika ya Kuzuia na Kupambana na Tatizo la Ugaidi Duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo mimi nataka kulisema, la kwanza kabisa ni umuhimu wa maisha, umuhimu wa uhai ambao Mwenyezi Mungu ametuzawadia. Hatupaswi kabisa ku-compromise na uhai ambao ni zawadi pekee tuliyopewa na Mwenyezi Mungu. Sasa tunapoona mtu anacheza au anafanya utani au anachezea maisha ya mwanadamu asiyekuwa na hatia hakuna mtu hata mmoja atakayefurahi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, Azimio hili ama Itifaki hii lengo lake ni kwenda kuhakikisha linalinda uhai wa mwanadamu. Na hasa sisi watanzania ambao tumekuwa ni nchi ya amani kwa kipindi kirefu, kisiwa cha amani, sasa yanapokuja matukio kama haya ya ugaidi yanaondoa kabisa ile heshima ya uhali ambayo Mwenyezi Mungu amempatia mwanadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwanza niwaombe Wabunge wenzangu waunge mkono hoja hii, waunge mkono Itifaki hii iweze kuridhiwa ili sasa nchi yetu iweze kuhakikisha inanufaika na zile faida ambazo wenzangu wanazisema zinazotokana na Itifaki hii. Na kimsingi Itifaki hii imeshasainiwa na nchi nyingi. Nchi zipatazo 45 zimesaini ikiwemo Tanzania na nchi 21 zimeridhia. Kwa hiyo, sisi sasa tunaenda kuwa nchi zaidi ya 22 ambazo tayari zimesharidhia- adopt hii Itifaki kwa lengo la kuhakikisha tunabadilishana uzoefu, tunabadilishana taarifa kama ambavyo wenzangu wamesema katika kupambana na tatizo hili la ugaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tunavyofahamu panapokosekana amani hata shughuli za kibinadamu za kiuchumi hazifanyiki. Huwezi Kwenda kufanya kazi huku ukiwa na mashaka ukiwa huna uhakika na uzima na usalama wa mazingira uliyonayo. Ndiyo maana kuna watu hapa akiona mende ana mashaka hawezi tena hata kutoka, anakuwa na wasiwasi sasa hapa tunazungumzia suala la ugaidi adui ambaye humuoni, hujui ni wakati gani atatekeleza tukio. Kwa hiyo, ni muhimu sana tuhakikishe tunaliridhia azimio hili ili tuweze kunufaika na faida zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kwenda kuridhia Itifaki hii itaisaidia nchi yetu kuhakikisha inachukua hatua za lazima za haki za msingi za binadamu dhidi ya vitendo hivi vya kigaidi. Vilevile itasaidia kuhakikisha nchi yetu inazuia uingiaji na utoaji wa mafunzo kwa vitendo vya kigaidi ama vikundi vya kigaidi vinavyojihusisha na haya masuala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo inaenda kuipa nchi yetu sasa nguvu, tena kwa kushirikiana na nchi zingine, kupambana na vikundi mbalimbali vinavyojihusisha na matendo ya kigaidi. Pia itasaidia kuainisha, kutambua na kuzuia ama kukamata fedha na mali zinazotumika katika masuala haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ugaidi, kama tunavyofahamu, mwenzangu mmoja amesema ni organized crime. Ni watu ambao wameungana. Kwa hiyo, inawezekana nchi ziko sehemu nyingine, Ulaya na kadhalika, zinakuja huku kwa njia zisizofaa, kuja kutumika kigaidi. Kwa hiyo, hii itifaki inakwenda kusaidia katika kuzuia fedha haramu za namna hiyo ambazo zinakuja kuhatarisha maisha yetu huku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naendelea kusisitiza na kuwaomba Wabunge wenzangu, tuone umuhimu wa itifaki hii na kuhakikisha tunaungana kwa pamoja, tunairidhia ili iende kusaidia nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, itasaidia kuanzisha pia vituo vya Kitaifa ndani ya nchi yetu kwa ajili ya kubadilishana na kupeana taarifa za makundi ya kigaidi kwa wakati na shughuli za kigaidi katika ngazi za kikanda na hata Kimataifa. Kwa hiyo, tufahamu kwamba inawezekana kuna taarifa zimepatikana nchi fulani au eneo fulani, sisi hatuna, lakini taarifa hizo zinataka kuathiri nchi yetu, kwa hiyo, sasa tunakwenda kupata uhuru ule ama uwezekano rahisi wa kupata taarifa kutoka sehemu nyingine ambazo zingekuja kutuathiri sisi huku nchini mwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo hili in a nutshell ukizungumzia faida mahususi za itifaki hii, kwanza ni kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na kijamii kutokana na kuwepo kwa amani na usalama. Kama ambavyo tumesema kule mwanzo kwamba jambo la kwanza ni amani na usalama katika nchi yetu. Sasa panapokuwa na usalama, ndipo shughuli za kibiashara na za kiuchumi zitafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna uwekezaji tunaoweza kupata kama nchi yetu ina viashiria vya ugaidi ambavyo tulishawahi kuona hata huko nyuma. Watalii hawawezi kuja. Kukishakuwa tu na taarifa zozote kuhusiana na masuala ya ugaidi, watalii hawawezi tena kuja. Kwa hiyo, hii sasa inakwenda kutuwekea uhakika wa utalii na hata wageni na wawekezaji wa sekta mbalimbali katika nchi yetu katika kuhakikisha tunaimarisha uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia ushirikiano, itaipa nchi yetu uwezo wa kushirikiana na nchi wanachama katika kulinda amani na usalama. Hii ndiyo ambayo tunasema inaenda kuhakikisha uhai ama kulinda mali za watu pamoja na maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nalo ni la muhimu ni kuhakikisha tunakwenda kubadilishana utaalam na masuala ya misaada ya kiufundi. Sisi tuna limitation, kuna wenzetu wengine ambao wame-advance, kwa hiyo, tunaporidhia hili, ina maana tunaenda kushirikiana na wenzetu wengine ambao wame-advance, wana utaalam na pia ufundi uliopo ili tuweze kushirikiana, tuutumie katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa nasema hii inaenda kuisaidia nchi yetu; kama unavyofahamu, kumekuwa na taarifa nyingi kwamba kuna watu wanasema watuhumiwa wengi wa ugaidi wanakamatwa, wanakaa muda mrefu magerezani, wanashikiliwa, wanateswa. Kwa hiyo, hii pia inakwenda kutusaidia, na nchi inakwenda kupata namna ya ku-deal na zile kesi za watuhumiwa wa masuala ya ugaidi kwa urahisi. Badala ya kukaa muda mrefu magerezani, hii inakwenda kutusaidia pia katika kuhakikisha hatua zinachukuliwa. Pia hata kuwarudisha wale walioko nje, walioko Tanzania wa nchi nyingine waende kwenye nchi zao, Watanzania walioko nje warudishwe kwa ajili ya kufuata taratibu za kisheria ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niendelee kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kuridhia itifaki hii kwa pamoja ili kuhakikisha nchi yetu inakuwa salama na inaepukana na masuala haya ya kuishi kwa hofu na mashaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. Ahsante sana. (Makofi)