Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Humphrey Herson Polepole

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi nianze kwa kupongeza kazi nzuri sana ya Kamati.

Mheshimiwa Spika, Ibara ya 8(1)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazungumzia lengo kuu la Serikali itakuwa ni ustawi wa wananchi wetu. Katiba inaeleza lengo kuu ni ustawi na lengo hilo linafanyika kwa kutunga sera zinazolenga kuleta ustawi wa watu wetu katika maeneo kadhaa wa kadhaa. Baada ya sera tunatunga sheria ili kuhakikisha kwamba yale ambayo tumeyaweka kwa maana ya ustawi na maendeleo ya watu yanaweza kuwa na nguvu ya kisheria kutekelezwa. Ili sheria ziweze kutekelezwa Katiba inatoa utaratibu wa Bunge ambalo ndilo lina mamlaka ya kuweka utaratibu wa kutekeleza sera na sheria kutunga kanuni.

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 4 cha Sheria ya Tafsiri kinaeleza kwa upana tunapozungumza sheria ndogo maana yake nini, tukasema leo basi kwa kuwa tumepata nafasi kwenye Kamati tulieleze ili tufahamu upana na umuhimu wa sheria ndogo inapokuja kwenye kuhakikisha ustawi wa watu wetu ni halisi.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Tafsiri kifungu cha 4, sheria ndogo inajumlisha amri, viongozi wetu wamepewa mamlaka ya kutoa amri (orders), viongozi wetu wamepewa mamlaka pia ya kutoa matamko (proclamations) na hayo matamko yanaweza yakagusa ustawi wa watu wetu, lakini pia zipo kanuni kwa maana ya rules and regulations, pia zipo notices ambazo pia zinatolewa na mamlaka mbalimbali na viongozi wetu, tunazo pia sheria ndogo kwa maana ya by- laws kwenye Serikali ya Mtaa kama ambavyo wenzangu wametangulia kusema lakini zaidi ya yote zipo hati kwa kiingereza tunasema instruments, zote hizi kwa ujumla ni sheria ndogo na Bunge hili limepewa dhamana ya kusimamia na kuhakikisha ya kwamba hazikinzani na sheria mama, sera zetu na Katiba zetu katika kuleta maendeleo ya watu wetu wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale ambapo tunaziendea ndivyo sivyo shida inaanza kuja, shida inaanzia kwenye Serikali, shida inakwenda Chama cha Mapinduzi na hata Wabunge mmoja mmoja inaweza kuwa mtihani. Rai yangu kwa Serikali, sheria ndogo jambo la msingi kifungu cha 48(1) kinaeleza utaratibu wa namna ambavyo tunapaswa kuziendea sheria ndogo.

Moja, ikitolewa tamko, amri ama ni kanuni zinatakiwa ziletwe hapa katika Mkutano unaofuata ndani ya siku sita. Na mimi ningependa nijielekeze kwamba Serikali izilete na ikizileta tupe nafasi pale kwenye Sheria Ndogo kuna watu wabobezi na mabingwa watazichambua na wataangalia maslahi mapana ya Taifa letu la Tanzania na mimi ningependa niangazie mambo kama matatu hivi: -

Kwanza, tozo kwenye miamala; hii ni kanuni tulipitisha uhalali wa kutoza, Waziri na Serikali wamekwenda kutengeneza kanuni lakini jambo limekuwa kubwa na lina interest kwa umma. Watu ukiwasikiliza hivi wananung’unika na jambo hili, sasa Serikali nafahamu linaweza kuwa ni jambo la kibajeti linagusa pesa za Serikali lakini umesikia hapa pesa imepungua, miamala imepungua liletwe hapa kama siyo kwenye bajeti, kwenye Sheria Ndogo sisi tuwaoneshe namna gani unaweza ukatoza miamala na wananchi wakawa na amani wame-relax vizuri, pesa ikaongezeka na pesa ikiongezeka ndiyo maendeleo ya nchi hii yatakuwa yanakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninashauri jambo hili la tozo ifike pahala, Mheshimiwa Rais alishatoa mwelekeo tufanyie kazi jambo hili, liletwe basi tuweke utaratibu sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni tamko la umeme shilingi 27,000. Hili jambo linaweza likafitinisha watu na Chama chetu cha Mapinduzi, mimi kama mnufaika wa Chama cha Mapinduzi jambo hili limesemwa kipindi hiki liletwe Bungeni, Mkutano unaokuja tuwasaidie wenzetu wa TANESCO maana yake nini kutoza shilingi 27,000 kwa Watanzania ambao wameusubiri umeme kwa miaka mingi sasa umefika huu siyo wakati wa kuwaambia tena shilingi 27,000 inaondoka! Unajua ilikuja kwa sababu kuna mkanganyiko na TANESCO lazima wafahamu, hawatupi umeme bure, tunalipa LUKU tena kwa pesa nyingi.

Mheshimiwa Spika, mwisho…

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Polepole kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Engineer Manyanya.

T A A R I F A

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nadhani unatakiwa kukaa kwanza. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ninapenda kumpa taarifa aliyekuwa anazungumza kwamba jambo hili Kamati imeliangalia kiundani na ilishaongea na Wizara kwamba wao wataweza kuleta ufafanuzi wa bei mbalimbali ambazo zinahitajika ili Kamati kwa pamoja tuweze kuangalia na wenzetu pia kwenye Bunge waweze kupata taarifa.

Kwa hiyo, kimsingi dhamira ilikuwa njema kwamba bei pengine ya umeme sasa imekuwa ni ndogo sana, lakini sisi tumesema tuliangalie kwa mapana ili tuweze kupata namna bora zaidi ya kushughulikia. Ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Humphrey Polepole malizia mchango wako.

MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Engineer Manyanya ni mama yangu na nimepokea taarifa yake lakini kule kwenye Sheria Ndogo hili halijaja bado ndiyo maana ninaiomba Serikali ilete kwenye Mkutano unaokuja kama Sheria ya Tafsiri inavyoelekeza ili sisi kama Bunge na Kamati ya Sheria Ndogo tusaidie kusema watu hawa kwanini tunasema shilingi 27,000, Kijijini na maeneo ya pembezoni kwa maana hiyo na kwa maslahi mapana ya Chama chetu cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho nizungumzie suala la Sheria ya Madawa na Vifaatiba ipo pale tumeipitia. Wanasema ukitaka kufanya majaribio ya kitabibu au clinical trial Mtanzania, mgunduzi kagundua dawa unatakiwa ulipe kule fees and charges dola karibu 3,000. Nani anaweza kutoa dola 3,000 kwa kugundua dawa ya corona, nani anaweza kutoa dola 3,000 kwa kugundua dawa ya kifua kikuu au na mambo kama hayo?

Mheshimiwa Spika, ninaomba vitu hivi viwe katika namna ambayo itakuza ugunduzi katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana ninaunga mkono hoja. (Makofi)