Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Ramadhan Suleiman Ramadhan

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chake Chake

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nami kupata nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mbele yetu ya Kamati ya Sheria Ndogo ambayo imesomwa mbele yetu na Mwenyekiti wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi nichukue fursa kama wachangiaji wengine kukupongeza kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sisi tunaahidi tutashirikiana na wewe.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kwenda kwenye hoja yangu nichukue fursa hii kumpongeza na kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, pesa za UVIKO zimefika Zanzibar na tumeanza kuona matumizi ya pesa hizo na zimeanza kuleta faraja na maendeleo kwa wananchi wetu. Miradi sasa ya maji, miradi ya kumalizia mabanda ya shule inafanywa kwa ufanisi mzuri zikisimamiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikijielekeza kwenye hoja, amemalizia mchangiaji aliyemaliza hapa kaka yangu Tarimo ambaye tupo Kamati moja kwamba kuna ugonjwa mkubwa unaendelea ambao ni ucheleweshaji wa kuyatekeleza mapendekezo yanayopendekezwa na Kamati.

Mheshimiwa Spika, kwenye Bunge lako tarehe 28 Juni, 2021 Bunge lilipitisha Azimio la Kamati hii ya Sheria Ndogo na moja kati ya maazimio yaliyopitishwa na Bunge lako ilikuwa ni kwenda kufanya marekebisho kwenye maeneo ambayo Kamati ilipendekeza na iliona yana dosari, lakini kwa masikitiko makubwa yapo maeneo ambayo toka Mkutano wa Pili, Mkutano wa Tatu bado hayajafanyiwa marekebisho, sasa ni mwaka Serikali hawajafanya marekebisho ya maeneo ambayo Kamati ilipendekeza kwao kufanyiwe marekebisho.

Mheshimiwa Spika, zipo sheria zinaendelea kuumiza watu na Bunge likaziona na likaiambia Serikali wazirekebishe sheria hizo lakini hadi leo wanakuja kwenye Kamati baada ya mwaka sasa kauli ni ile ile ndiyo tunaandaa jedwali la rasimu kupeleka kwa CPD, tunaandaa jedwali la rasimu kwenda kwa mchapaji, kwa tukikaa nao wakija na story hizo hizo inaumiza kwa sababu tunapotoa mapendekezo tunataka wananchi wetu wasiendelee kuumizwa na sheria ndogo ambazo zipo na zinatumika huko kwenye maeneo tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka leo kwa mfano zipo sheria za kwenye Halmashauri yako ya Mbeya za kutoza tozo za bajaji na mpaka leo hazijafanyiwa marekebisho huu ni mwaka sasa na tumesema zifanyiwe marekebisho kwa sababu zilikuwa zimeshaanza kuleta ugomvi kule, lakini hadi leo bado. (Makofi)

Kwa hiyo, bado ninasisitiza na ninaomba na ninaweka msisitizo kwamba yale makabrasha yakishatoka kwenye Kamati yasiende kufungiwa kabatini, yanahitaji kufanyiwa kazi ili tupate weledi mzuri wa jinsi ya kuwasimamia watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ambayo nilitaka kuchangia ni hoja ya ushirikishwaji Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (CPD). Hapakuwa na utamaduni wa Serikali wanapokuja kwenye Kamati kujibu hoja za Kamati kuja na mfanyakazi au ofisa yeyote wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ili kuja kutueleza hatua zilizofikiwa, wakija tu watakuambia kwamba hili lipo kwa CPD, sisi tukawashari kama Kamati sasa mkija kwenye Kamati mje nao Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ili sasa tujue ukweli ni upi kwamba tatizo lipo kwenu au tatizo lipo kwa CPD. (Makofi)

Sasa hivi hili limerekebishika na tunataka kutoa shukrani kwamba sasa wanapokuja kwenye Kamati yetu wanakuja na Ofisi ya CPD sasa hakuna mtu ambae anaweza kumzulia mwenzake kwamba nimepeleka pale kwangu imeshaondoka kwa hiyo kazi inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hayo ndiyo ambayo nilitaka kuchangia kwa leo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)