Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, na mimi nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia mjadala huu wa Kamati ya Sheria Ndogo, lakini kabla sijaenda mbele na mimi pamoja na kwamba ulishakataza kuendelea kukupongeza, basi nichukue nafasi hii kukupongeza wewe pamoja na Naibu Spika kwa ushindi ambao mliupata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niipongeze Kamati nzima lakini kipekee nimpongeze sana Katibu wetu wa Kamati ambaye amekuwa, akitengeneza majedwali ambayo yanatusaidia sana katika uchambuaji wa Sheria hizi Ndogo. Niwapongeze Serikali haswa Mawaziri na Naibu Mawaziri ambao walikuja mbele ya Kamati pamoja na watendaji wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakwenda moja kwa moja kwenye maeneo machache; nianze na la wadau. Ni muhimu sana kwa upande wa Serikali wanapokuwa wanaanza huu mchakato wawashirikishe kwa karibu wadau. Wadau hawa ambao wako field wanakuwa na uzoefu mkubwa na wamejawa maarifa ya kile ambacho kinaweza kufanyika kule kwenye field. Naweza kutoa mifano michache ilipokuja Tume ya Taaluma kwa Walimu (Teachers Professional Board), tuligundua kuna wadau wa muhimu sana ambao walikuwa hawajashirikishwa. Wengine ni wale walioko on the ground, lakini wengine ni Taasisi, ambazo zinawasaidia sana waalimu kama vile HakiElimu na nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini umuhimu wa wadau uliendelea kuonekana wakati tunapitisha sheria na kanuni za wavuvi ilionekana kwamba sheria iliyochukua usawia katika maeneo yote kuna tofauti kubwa sana kutekeleza sheria hiyo katika water bodies zetu. Kwa mfano, sheria iliyokuwa inataja urefu ambao aina fulani ya samaki wavuliwe ilionekana inafaa Ziwa Victoria, lakini Ziwa Tanganyika lenye kina kirefu katika urefu huo hupati hata samaki hao. Kwa hiyo, ni muhimu kuwashirikisha wadau kwa upana wao ili waweze kuleta ule utaalam na uzoefu wao pale uweze kuleta tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna wakati wadau ni Wizara nyingine na wakati Wizara moja inatunga sheria hizi au kanuni hailazimiki kuwasiliana na Wizara nyingine. Mfano, wakati Bodi ya Filamu wanaleta tozo zao kwa ajili ya maeneo ambayo yanaonyeshwa filamu kwa sababu tulikuwa tumeshapitisha sheria za Halmashauri mbalimbali ambazo nazo zilikuwa zimeweka tozo hizo tuliwashauri Wizara hizi mbili kukutana ili kuleta uwiano, kwa sababu mwisho wa siku mzigo mzito ulikuwa unakwenda kumdondokea yule mwananchi wa chini, lakini vilevile tumeelezea suala la umuhimu wa kuangalia uzoefu au uwezekano wa utekelezaji wa sheria.

Mheshimiwa Spika, zipo Halmashauri zilileta Sheria ya kuwatoza kwa mfano ma-mc kwenye sherehe na wanatoza kwa tukio. Tulipoangalia sheria kama hizi tukaona ni vigumu kwa watekelezaji wa sheria hii kuzunguka usiku kwenye kumbi za starehe/sherehe kuhakikisha kwamba ma-mc hao wamelipa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, badala yake tukaishauri waweze kufanya tozo moja kwa mwaka inakusanyika na haimlazimishi kwenda kuzunguka usiku kwenye kumbi za sherehe na pengine watu wanaweza wakawa wanafurahi wakawaletea matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la utekelezaji wa makubaliano tunayokuwa tumekubaliana na urejeshaji wa kilichofanyika. Wizara nyingi zimekuwa zikichelewa kuleta utekelezaji, nyingine kutokuleta kabisa lakini nyingine kuchelewa. Ikumbukwe baadhi ya sheria unakuta zimeshaanza kutumika kabla hazijaletwa kwenye Kamati yetu. Sasa tunapotoa maoni na yanachelewa kuletewa marejesho au kufanyika na mengine kutokufanyika kabisa yanaleta matatizo makubwa sana katika utekelezaji wa sheria hizi ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nikomee hapo na ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)