Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Nyongeza ya Bajeti ya Mwaka 2021/2022

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Nyongeza ya Bajeti ya Mwaka 2021/2022

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. nakushukuru sana kwa nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninaomba sana niunge mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha ya kuliomba Bunge liidhinishe shilingi trilioni 1.3 kwenye nyongeza ya bajeti yetu ya mwaka huu 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, waswahili walisema, usione vyaelea vimeundwa na mimi natumia nafasi hii kumsifu sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi yake na jitihada yake aliyoifanya hadi tukapata huu mkopo wa shilingi trilioni 1.3 ambao umekuwa na faida kubwa sana kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jimboni kwangu peke yake nimepata madarasa 98, nimepata mashine ya x-ray, nimepata jengo la huduma za dharura na nyumba ya watumishi, na kwenye maji nimepata shilingi milioni 500. Hiyo kwa kweli ni boost kubwa sana kwa Watanzania na ni jambo ambalo linaonekana wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze sana Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha na hata Waziri Mheshimiwa Masauni ambaye amewasilisha hapa, na watendaji wote wa Serikali waliohusika na hoja hii. Lakini nimpongeze Mwenyekiti wetu wa Kamati, Mheshimiwa Sillo na Makamu wake, Mheshimiwa Kigua, na Wajumbe wote wa Kamati ya Bajeti kwa jinsi ambavyo wameichakata hoja hii kwa kina ndani ya vikao vya Kamati wakishirikiana na Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpango huu wa kukabiliana na athari za UVIKO Tanzania ulikuwa unahitaji shilingi trilioni 3.6, lakini zilizopatikana ni shilingi trilioni 1.3, kwa jinsi ambavyo hizo shilingi trilioni 1.3 zimekuwa na faida kwa Watanzania sipati picha tungepata hizo shilingi trilioni 3.6 hali ingekuaje. Kwa hiyo, naomba sana juhudi kama hizi ziendelee kwa sababu zina faida kubwa kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiuangalia mgawanyo wa fedha hizi ambazo zinaombewa nyongeza nimeona kwamba shilingi bilioni 975.1 au asilimia 90 zimekwenda kwenye huduma muhimu za afya, elimu na maji ambayo lengo lake ni kuwakinga Watanzania wasipate maambukizi ya UVIKO. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuwakinga kwa namna gani; mtu akielimika vizuri, atajikinga vizuri zaidi dhidi ya hatari za UVIKO. Kuongeza madarasa maana yake ni kupunguza msongamano kwenye madarasa ambayo hiyo ni kupunguza kitisho cha maambukizi dhidi ya UVIKO. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye afya, kuboresha hizi huduma za dharura, huduma za wagonjwa mahututi, huduma za vifaatiba na vifaa vingine maana yake ni kumhudumia kwa haraka mgonjwa ili apate nafuu au apone kwa haraka. Hiyo ni kuwakinga wananchi na maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na maji hivyo hivyo; tunaambiwa kwamba ili mtu ajikinge vizuri na UVIKO anawe mikono kwa maji tiririka, sasa kama mtu hana maji atanawaje maji tiririka; maana yake ni kwamba kupeleka shilingi zote hizo kwenye maji inasaidia sana kupunguza hatari ya UVIKO. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hizi shilingi bilioni 693 ambazo zinaongezwa kama mkopo kwenye SGR. Ni faraja kubwa sana kwa Watanzania kwani sasa tuna uhakika kwamba SGR inakwenda kukamilika. Kujengwa kwa kipande kutoka Makutupora mpaka Tabora ni dalili kwamba kumbe hata vipande vingine vya kutoka Tabora kwenda Mwanza, kutoka Isaka kwenda Keza, kutoka Tabora kwenda Kigoma, kutoka Uvinza mpaka Msongati, kutoka Tabora kwenda Mpanda mpaka Karema, vyote hivyo sasa hii ni dalilikwamba vinakwenda kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na hii ni faida kubwa sana kwa nchi, na ninaomba sana Serikali iendelee kuhakikisha kwamba fedha zinatafutwa ili vipande vyote hivi vijengwe. Lego na faida ni nini; ya kwanza ni kusisimua ujenzi wa viwanda kwenye maeneo yote ya karibu na reli, lakini kushusha gharama za usafiri na usafirishaji, lakini tatu ni kupunguza kasi ya uharibifu wa barabara zetu; nne ni kusafirisha tani 10,000 kwa mkupuo mmoja. Hizi ni faida kubwa sana kwa uchumi wa nchi yetu. Kwa hiyo naomba sana Mheshimiwa Rais na wasaidizi wake wote endeleeni kutafuta kila namna ili nchi hii iweze kupata maendeleo.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. naunga mkono hoja. (Makofi)