Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote niungane na Wabunge wenzangu kukupongeza wewe pamoja Naibu Spika kwa kuchaguliwa kwa asilimia 100, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Wenyeviti wa Kamati hizi mbili ambao kwa kweli, wamefanya kazi nzuri sana katika kuwasilisha taarifa, lakini pia kamati zimechambua kwa kina sana mambo mbalimbali ambayo yanaonekana na haya ndio machache ambayo yameweza kuja ambayo mimi naamini kwamba, yana vitu vya msingi ambavyo Serikali inatakiwa iende ikavifanyie kazi.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote tuunge mkono maazimio yaliyoko katika taarifa hizi, ili Serikali iende ikayafanyie kazi. Na ikiyafanyia kazi ituletee mrejesho namna ilivyotekeleza haya maazimio. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama taarifa zilivyobainisha, yapo maeneo ambayo yamekuwa yana matumizi yasiyoridhisha. Maeneo ni mengi, lakini katika Serikali ukichukua Wizara, ukachukua mashirika, ukachukua idara zinazojitegemea, ukachukua wakala, maeneo mbalimbali yanaonekana kuwa na viashiria vya matumizi yasiyoridhisha. Na maeneo hayo ni pamoja na maeneo ya utengenezaji wa mifumo.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi mifumo mingi imekuwa ni kichaka ambacho kinatumika katika matumizi mabaya ya hela za umma. Kwa hiyo, nitaliomba Bunge lije liangalie katika taasisi zote mifumo yote ambayo tumeitengeneza kwa muda wa miaka mitano au kumi mpaka tulipofika tumetumia fedha kiasi gani? Na hiyo mifumo imeleta nini kwenye Taifa hili? Hilo ni eneo la kwanza.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo limekuwa ni shida ni kwenye eneo la manunuzi na usimamizi wa mikataba. Kwa sababu ya muda, sitaweza kuyazungumza kwa undani. Lakini katika hili eneo ndio maana tumeona kwa mfano bandari peke yake, hiyo tumeweka ni mfano tu, bandari peke yake mifumo bilioni 17 na kitu zimetumika, lakini mifumo ile haina tija. Sasa hivi wameondokana na mifumo hiyo, mifumo haionani, sasa wanakuja na mfumo mwingine, tena zinahitajika hela nyingine, sasa hii kwa kweli haikubaliki. Na taasisi nyingine nyingi ambazo mimi kwa sababu ya muda sitaweza kuzisema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hebu tuje kwenye hali halisi, TRA wanaonekana kwenye makusanyo wana trilioni 360 ambazo ziko kwenye Bodi ya Rufaa ya Kodi. Hivi ni sura gani inayoonekana kwenye Serikali?

Mheshimiwa Spika, yani tunaposema Serikali inadai hizo hela, nimeliangalia hili deni mwaka 2015 mpaka 2016 deni lilikuwa ni 1.3 trillion. Mwaka 2017 deni lika-shoot mpaka trilioni 360; nazungumzia trilioni ambazo ukizigawa ni bajeti ya nchi hii ya miaka 10 hizo hela kama zingekusanywa, lakini hebu tujiulize hivi hili deni lina uhalisia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeangalia kwenye vitabu vyote vya TRA, vitabu vya Serikali, vitabu vya kiuhasibu, hili deni halipo. Na hili deni linatokana kwa kiwango kikubwa na makinikia, lile deni la makinikia. Sasa kama tumefanya majadiliano na zile kampuni zinazohusika tumemaliza, hili deni nashauri Serikali iangalie uwezekano ilifute linachafua taswira nzuri ya Serikali. Kwa hiyo, nafikiri hili lazima waliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili; yapo mashirika mengi ambayo yanaonekana yana upungufu mkubwa, yana shida ya fedha. Nianze kwa mfano Shirika la Ndege linaonekana lina upungufu mkubwa, lina madeni bilioni 246 ambazo tunafikiri Serikali iangalie uwezekano wa kuiongezea ili mizania ya hesabu ikae vizuri, lakini kuna TANESCO. TANESCO kuna bilioni 493.6, lakini TANESCO hiyo inadai kwa wateja bilioni 422, sasa mizania yake haijakaa vizuri. Ukienda TPDC wanaidai TANESCO fedha nyingi sana, lakini kwenye TPDC pia kuna deni la ujenzi wa bomba la mafuta ambalo Serikali inalipa tayari, lakini kwenye vitabu halifutiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nafikiri Serikali, haya yanachafua. Ni vizuri mkaangalia namna ya kusafisha vitabu vikae vizuri, mizania zile zikae vizuri, kuliko hali iliyoko sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, waliunganisha kweli benki wakaamua kuunganisha, hivi Serikali unapochukua benki inayofanya vizuri unaunganisha na benki isiyofanya vizuri, lengo linakuwa ni nini? Halafu unawachukua wale wafanyakazi walioshindwa kuiendeleza benki, walioharibu, unawaleta kwenye benki inayofanya vizuri. Hii haijakaa vizuri kabisa. Halafu unachukua madeni chechefu yaliyoshindikana kulipwa huko, unayaleta kwenye benki inayofanya vizuri, maana yake sasa mizania ya benki inayofanya vizuri sasa inaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafikiri hili siyo lengo, lengo la Serikali inawezekana lilikuwa zuri, zile benki zenye madeni chechefu waziundie kampuni yao huko zinazofanya vizuri waziache zifanye vizuri. Hiyo itasaidia sana na naona kuna hizo sitaki kuzitaja kwa sababu ya muda, naona mambo karibu yamekwisha, lakini nataka niseme moja kwa dakika moja.

Mheshimiwa Spika, kuna benki zinazodaiwa, kuna Serikali inadaiwa trilioni 1.1 na NSSF, lakini Rais wetu amefanya kazi nzuri. Toka miaka nenda rudi tunadai ule Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Serikali zaidi ya trilioni mbili na kitu, ametoa non cash bond kwenye hiyo, amenusuru.

Mheshimiwa Spika, sasa tunamwomba na NSSF aangalie na haya mashirika mengine nayo aangalie, lakini hii tume ya madini ya bilioni 156 wafanye …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa sasa hapo tena muda umetuacha kidogo.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, naomba wafanye reconciliation.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja zote na Mungu awabariki. Ahsante sana. (Makofi)