Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nami kama Mjumbe wa Kamati ya LAAC naunga mkono Taarifa ya Kamati kwa asilimia mia moja. Nasi kama Wabunge wa Bunge hili la kwanza tunaendelea kujifunza kwa Mwenyekiti wetu na Katibu wetu wa Kamati ya LAAC Bwana Bisile, mambo mazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama walivyosema wenzangu, nami nakupongeza wewe na Mheshimiwa Naibu Spika kwa kuchaguliwa; na siku ile tumekuchagua tukakutana na Waandishi wa Habari, wakaniuliza kwa mic mdomoni ghafla: “Unafikiri Dkt. Tulia atakuwa Spika wa namna gani?” Basi mimi nikasema atakuwa Spika wa STK; kwa maana ya Sheria, Taratibu na Kanuni. Tumeshaanza kuona humu sasa, sheria, taratibu na kanuni zikishughulikiwa vya kutosha. Uzuri wa hiyo STK ni kwamba inatujali sisi manjuka, haitubani sana. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuendelea kuchangia kama walivyochangia wenzangu kwa haraka nikijumuisha vipengele vinne ama vitano ambavyo Mwenyekiti amevisema katika taarifa yake. Uutagundua kwamba karibu tunazungumzia upotevu au watu kuchezea karibu shilingi bilioni 64.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika taarifa yake, matumizi ya fedha mbichi, anazungumzia shilingi bilioni 18.7; kufutwa kwa miamala ni shilingi bilioni 4.5; kurekebishwa kwa miamala ni shilingi bilioni 4.8; na mawakala fedha ambazo wamezikusanya, hawajazipeleka katika Hazina za Halmashauri ni shilingi bilioni 35. Hii ni karibu shilingi bilioni 64, ukiigawanya shilingi milioni 500 kwa Vituo vya Afya, ni karibu Vituo vya Afya 13.

Mheshimiwa Spika, katika kuzunguka na Kamati ya LAAC kwenye Halmashauri mbalimbali nimejifunza vitu vingi sana. Kutokana na ufinyu wa muda, ukweli ni kwamba kama tunataka maendeleo ya nchi hii, ni lazima kutazama Halmashauri zetu vizuri. Vinginevyo fedha zitakuwa zinatafutwa na Mheshimiwa Rais Samia duniani kote, zinaletwa, tunapeleka Idara za Kilimo, Elimu, lakini watu wanazichezea fedha hizo. Ni jambo la hatari sana. Nasi kama Wabunge siku hizi tunalalamika hapa.

Mheshimiwa Spika, Mwenyekiti amesema, kwa miaka mitatu trends zinaonesha bajeti yako katika Bunge hili haipelekwi karibu kwa fifty percent. Amesema tunaidhinisha shilingi bilioni 977 inapelekwa shilingi bilioni 497 kwa sababu ya fedha hizi kutokukusanywa vizuri na fedha zile ambazo tunatakiwa tupate kama mapato, hazikusanywi. Wabunge wamesema kuhusu POS na kadha wa kadha.

Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza, ni lazima tuishauri Serikali yetu, nami mwisho nitashauri. Nimeona juzi Mheshimiwa Rais Samia amechukua hatua tu, amepeleka fedha za madarasa, watu wamecheza nazo, akaondoka na Wakurugenzi Wanne. Tumeona Mkuu wa Mkoa wa Mara alivyozungumza kuhusu Wakuu wa Idara na changamoto katika Halmashauri. Lile siyo tatizo la Mara peke yake, ni karibu tatizo la nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, ushauri wetu, hivi katika yote haya yanayozungumzwa na Waheshimiwa Wabunge katika malalamiko, kweli tuko serious katika nchi hii, kuna Halmashauri haina Mkuu wa Idara ya Ununuzi? Kweli kabisa! Yaani, tunazungumza hapa, fedha zinaenda mabilioni na mamilioni ya fedha kwenye Halmashauri; Halmashauri Mweka Hazina anakaimu. Serious! Tunazungumza fedha zinaliwa, unaenda unakutana na Afisa Mipango anakaimu; au unakuta mtu anayelalamikiwa ni Mkuu wa Idara miaka 20, ana malalamiko yake mpaka wananchi wanajua upungufu wake na miradi anayoifanya katika Halmashauri ile, anaachwa.

Mheshimiwa Spika, hatuwezi hata kidogo kuendelea. Kupanga ni kuchagua. La kwanza, ni muhimu sana kujaza Ikama ya Watumishi muhimu. Tunajua Serikali haiwezi kuajiri watu wote, Serikali ya nchi hii inashindwa kuajiri Wakuu wa Idara wa kila Halmashauri wakapatikana watu smart, wenye sifa walio-perform, wakasimamia fedha zetu katika Idara! Haiwezekani hata kidogo. Tupange, tuchague tuhakikishe tunapata watumishi wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuwezesha kitengo cha Ukaguzi wa Ndani. Sisi katika taarifa ya CAG, tunayopata kwenye Kamati, kwenye Halmashauri zote kuna Wakaguzi wa Ndani; na Wakaguzi wa Ndani ni kama indicator kwa Mkurugenzi.

Mheshimiwa Spika, kwa sisi ambao tulikuwa ma-DAS, anamwambia, Mama utaratibu huu wa kufanya manunuzi hapa haujafuatwa; utaratibu upo hivi, na hivi na hivi. Mkurugenzi asiyesikia, unamkuta kwenye taarifa ya CAG.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, hivi huyu Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani katika Halmashauri, gari yake mbovu, anaazima gari kwa Mkurugenzi; akitaka kwenda kwenye ukaguzi wa miradi anachukua mafuta kwa Mkurugenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili suala linasemwa. Nimeangalia video, Youtube ya hotuba za Mabunge ya miaka kumi nyuma, wanalalamikia hili jambo. Hivi mtu unayemkagua na kumshauri halafu unaenda kumwomba mafuta, atazingatia ushauri wako? Akiona unamsumbua, anakukanyagia tu, mafuta hakupi. Ndiyo malalamiko kila sehemu ukienda Wakaguzi wa Ndani wameshindwa kwenda kukagua miradi.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, naomba kuwasilisha. Ahsante sana. (Makofi)