Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie sekunde hii moja kukupongeza kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika wetu wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 42, lipo jambo linazungumzwa na Kamati juu ya Daraja la Tanzanite. Daraja hili ni furaha ya Tanzania kupata mkopo wa dola milioni 121, shilingi za Kitanzania kama bilioni 243. Hili ni daraja zuri lakini tunatambua umuhimu wa daraja lile limekuwa ni mbadala wa daraja lililokuwepo siku zote pale ambalo limekuwa likisaidia wananchi, lakini vilevile palikuwa na foleni kubwa.

Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba hili siyo daraja la kwanza kupatikana kwenye nchi yetu. Dar es Salaam lipo daraja lingine zuri Kigamboni ambapo mwaka 2015 lilijengwa chini ya Shirika letu la NSSF kwa shilingi bilioni 214 tofauti ya bilioni kama 30 tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wamesema wengine waliotangulia kusema leo kwamba tunaendelea kuwa na mshangao juu ya faida zote ambazo zinaonekana juu ya daraja lile. Daraja la Kigamboni toka limejengwa kama mbadala wa wananchi wa kule tayari limewekewa tozo, wananchi wale upande mmoja walikuwa wakilipa tozo za kawaida vilevile daraja lilipokuja kuwa mbadala wakaendelea kulipa tozo. Sababu kubwa ilikuwa ni fedha zetu wenyewe kutoka katika Shirika letu la NSSF ambalo limewekeza pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, daraja la sasa hivi ni mkopo ambao tunajua bilioni 243 linaenda kuwa deni la Serikali, deni ambalo kila Mtanzania ana nafasi ya kulilipia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia sababu kama mbili tu au tatu za kutofautisha watu wa Kigamboni na lile daraja la pale na wale watu wanaopita, kuna hali kama mbili. Moja, ni umasikini. Ukiangalia upande wa Kigamboni, viashiria vyote vya kimasikini vipo kule. Hali ya umasikini, hata matumizi ya kaya kwa siku, utaweza kutofautisha na watu wa Oysterbay, Masaki na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama waliotangulia walivyosema na kushauri, ni vizuri. Mimi nishauri katika eneo hili; kama Kigamboni katika nyanja zote hizo mbili, madaraja yote mawili, wanalipa tozo, basi na huku walipe tozo. Option ya pili, kama ni lazima sana, au sisi ambao hatujui kwa huku hawalipi na kule wanalipa, basi wananchi wa upande wa kule kwenye kaya nyingi za masikini wasilipe tozo katika upande mmoja; na upande wa daraja waendelee kulipa yale magari yanayopita. Inaweza ikawa ni njia nzuri ya kusaidia malalamiko makubwa ya watu wa Dar es Salaam na wananchi wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze sana kwenye upande wa TARURA. Wakati wa nyuma hapa kidogo katika kutafuta mapato kwa ajili ya barabara zetu vijijini na mijini chini ya TARURA, tuliingiza tozo ya mafuta (petroli na dizeli) shilingi 100/=, tukatarajia kupata shilingi bilioni 322. Ni kweli katika fedha hizo mpaka sasa zimeshatumika, zimetolewa takribani 43%, jambo zuri na ninampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi fedha hazitoshi. Mpaka juzi hapa, Bunge letu hapa likatoa kauli, TARURA waje na tathmini ya nchi nzima kwa kuokoa hali ya barabara zilizoharibika. Tathmini imekuja na Kamati imeeleza, takribani shilingi bilioni 119 wanazihitaji, lakini shilingi bilioni 119 wanazitoa wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 wamepangiwa shilingi bilioni saba na nyongeza ya shilingi bilioni moja ambayo wametoa katika reallocation ya ndani ambayo kwa kuongezea wamefikia shilingi bilioni nane. Hii ndiyo dharura kwenye bajeti ambayo tunaendelea nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukaona hali ya hatari ambayo tunayo kwenye barabara zetu. Sasa Kamati inaeleza, ongezeko ni shilingi bilioni 111, zinatoka wapi? Maana yake nini? Zinaenda kudhuru bajeti iliyopitishwa na Bunge hili. Shilingi bilioni 111 ni fedha nyingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, kwa sababu hatuwezi kuendelea hivi kudhuru bajeti ambazo tunakaa kama Taifa tunapitisha, lakini leo tukafanye reallocation between votes, tukanyang’anye katika mafungu mengine ya Wizara ili tuweze kufanya jambo la dharura katika hili. Sasa, nini cha kufanya? Kuna mambo mawili: Moja, katika eneo hili ni vizuri tupeleke fedha zaidi ya shilingi bilioni 100 kwenye bajeti yetu inayokuja 2022/2023 kama dharura; eneo la pili kwa sentensi moja, ni kutafuta vyanzo vingine. Dar es Salaam kule tunahitaji GN…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Malizia malizia.

MHE. ISSA J. MTEMVU: …ije haraka ili tuweze kutatua barabara za ndani kama ilivyo miji 45 katika mikoa mingine ambavyo wametatuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)