Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Liganga na Mchuchuma limeongelewa tangu Bunge la Nane, tuko Bunge la Kumi na Mbili. Waheshimiwa Wabunge wenzangu, kwa maslahi ya Taifa letu tusikubali tukakamilisha kipindi chetu cha Ubunge bila Mradi wa Liganga na Mchuchuma kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya Viwanda na Biashara ilieleza vizuri, Kamati yetu tumeeleza vizuri, huu mradi ni wa muda mrefu, leo tunaambiwa kuna Kamati inaangalia ni namna gani labda waachane na Mwekezaji au kupitia mkataba mpya. Huyu Mwekezaji ameshindwa kuwekeza hana mtaji wa dola za Kimarekani bilioni 2.9, hana! Tunabembelezana naye kwa nini? Mpaka sasa hivi tunavyozungumza alitakiwa amalize kujenga kiwanda cha chuma, alitakiwa amalize kujenga miundombinu ya umeme, alitakiwa alipe fidia ya wananchi watakaopisha ule mradi, ameshindwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Madini ipo wazi Kifungu Na. 47(1), twendeni ukurasa wa 123 unasema wazi kwamba mtu akipewa leseni ya uchimbaji anatakiwa ndani ya miezi 18 awe ameshachimba na kuendeleza, niwaulize Waheshimiwa Wabunge wenzangu, ni miezi 18 mingapi imepita tangu Bunge la Nane? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu sijawa Mbunge enzi ya Mama Mary Nagu tunazungumza Liganga na Mchuchuma! Mungu atupe nini? Leo hii tunaagiza chuma nje wakati chuma kipo kimelala pale, bado tunafikiria kuendelea na Mwekezaji huyu, sheria zetu za nchi zinatulinda na kwenye taarifa yetu tumesema, lazima Serikali muwe makini na kuangalia mitaji ya wawekezaji wanaokuja kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunazungumzia Kamati inaangalia! Tunamlinda nani? Hivi kweli kwenye uwekezaji mkubwa wa namna hii wenye maslahi ya Taifa letu hatujui uwezo wa mwekezaji? Zaidi ya miaka kumi inapita hana dola za Kimarekani bilioni 2.9! Wananchi kule wa Ludewa wamekaa wanashindwa kuendeleza maeneo yao. Tunaomba Bunge la Kumi na Mbili lisiingie kwenye historia zingine, twendeni tulitendee haki Taifa letu, twendeni tukaweke historia kwamba kulikuwa kuna Bunge la Kumi na Mbili lilifanya maamuzi ya kuhakikisha uchumi wa nchi yetu unakua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yetu tumezungumzia kuhusiana na kampuni ya uagizaji wa matrekta, hii ilikuwa tangu Awamu ya Nne, matrekta 2400 kutoka Poland, tangu enzi za Waziri Mkuu Mheshimiwa Pinda. Hata hivyo, mpaka leo yamekuja matrekta 800, matrekta 1,774, mabilioni ya shilingi pesa za walipakodi hayajafika. Ni aibu nikisema hapa tumeuliza kwenye Kamati wanasema, eti Kampuni imefilisika, yaani imefilisika kabla haijamaliza kuleta matrekta yetu? Tuna uwezo gani wa kugundua uwezo wa watu tunaoingia nao mikataba? Yaani ameleta matrekta 800 kampuni imefilisika, matrekta ya Watanzania ambayo yangesaidia wakulima wa nchi hii 1,774 hayajaingia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili, Kamati yetu ya uwekezaji tuliopewa jukumu la kusimamia pesa za walipakodi katika uwekezaji vitu kama hivi hatutaruhusu. Tunaitaka Serikali ije na majibu ya kina, matrekta ya Watanzania 1774 yatakuja lini? Haituingii akilini, watu wameingia tenda, wamesaini mikataba baada ya kuleta matrekta 800, baadaye kampuni ikafilisika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la EPZ. Tulipiga kampeni sana na tukatoa maeneo mbalimbali, tukatenga maeneo ya uwekezaji, leo hii EPZ ingefanya vizuri tatizo la ajira nchi hii ingekuwa historia. Hivi ninavyoongea kati ya Kanda 15 ni Kanda tatu tu zimeweza kuwekezwa, Kanda 12 wananchi wametoa maeneo yao hawajalipwa fidia na tumeambiwa EPZA iko kwenye ukwasi, ni kwa sababu Serikali haipeleki pesa za kutosha kwa ajili ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wetu wamesimama hawaendelezi maeneo yao. Kwa nini tunatafuta ugomvi na wananchi? Kwa nini tusiende kuchukua maeneo tunayoweza kuwekeza? Kanda 12 wananchi wamechukuliwa maeneo yao uwekezaji haujaanza halafu tunaimba ajira kwa vijana wa nchi hii wakati tunajua ni maeneo gani tunaweza tukafanya vizuri na tatizo la ajira nchi hii likapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mheshimiwa Vuma amezungumzia kwenye suala la uwekezaji, naomba nizungumzie ni namna gani Serikali hawalipi madeni, hawapeleki michango ya wanachama.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyozungumza ATCL tangu mwaka 2008 mpaka 2016 haijapeleka michango ya wanachama, inadaiwa bilioni 16 hawajapeleka PSSF. Hizi ni pesa za watumishi wa nchi hii, walikatwa kwa ajili ya maisha yao baada ya utumishi wa nchi yao wanayoipenda sana. Nimesikia habari kwamba hawajalipa hizo pesa eti wanafanya mazungumzo wasilipe riba, come on! Pesa za watu walizochanga, ile siyo benki, ni pesa za wafanyakazi wa nchi hii waadilifu, wamekatwa zaidi ya miaka kadhaa ili waweze kupata manufaa baada ya kustaafu. Hapa kuna watu wamestaafu hawajalipwa pesa zao kwa sababu michango haijapelekwa, bilioni 16! Kuna watu wamekufa, kuna watu bado wanaendelea na kazi kwa uadilifu na uaminifu lakini michango yao haijapelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema hili suala kwenye vyombo vya habari, nilisema hili suala kwenye maeneo mengine, tunaomba pesa za wastaafu ziende.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua kwamba tathmini ya Mifuko imefanywa na iko Serikalini huu mwezi wa Tisa hamtaki kusema status ya mifuko ikoje na nimepata taarifa mmeanza kupunguza madeni ya Mifuko…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)