Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia taarifa hizi kwanza nawapongeza Wenyeviti wote wawili wamewasilisha vizuri. Lakini mchango wangu utajielekeza kwenye Kamati yetu ya Bajeti naunga mkono hoja, nampongeza Mwenyekiti na yote ambayo yamezungumzwa ndani ya taarifa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu jioni ya leo utajielekeza kwenye tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa kipindi cha miezi sita Julai mpaka Disemba, 2021. Kupitia tathmini hii naomba nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa kuweza kukusanya mapato ya zaidi ya shilingi trilioni 18.11 ikiwa ni asilimia 49.6. na; katika muktadha huu nichukue fursa hii kuipongeza sana Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kukusanya mapato ya zaidi ya shilingi trilioni 11 ikiwa ni asilimia 98. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kipekee kwa mwezi wa 12 kukusanya na kusajili kiwango kipya cha makusanyo ya shilingi trilioni 2.5 ambacho ni kiwango kipya, tangu Mamlaka hii imeanzishwa mwaka 1995 ni mapato ya juu kabisa kukusanywa tangu imeanzishwa miaka 26 iliyopita. Kwa hiyo, naipongeza sana TRA na Wizara ya Fedha kwa juhudi kubwa lakini pia nampongeza sana Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan, kwa maelekezo yake kwa Mamlaka hii ya Mapato TRA kukusanya mapato kwa ueledi, uadilifu na uwajibikaji. Lakini sambamba na hilo yapo mapato ambayo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliwasilisha kwenye Kamati yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ambazo ni za eneo hili la mapato ambazo hazijafungwa zaidi ya shilingi trilioni 356. Kwa maana hiyo Serikali yetu kupitia TRA na Wizara ya Fedha inayo nafasi ya kuvunja rekodi yake kila wakati, endapo itajielekeza kuhakikisha Wizara zinakusanya shilingi bilioni 546 ambazo hawajakusanya. Mamlaka za Serikali za Mitaa shilingi bilioni 113 Taasisi za Kiserikali shilingi bilioni 6 lakini pia hata zile kesi ambazo zipo kwenye Mahakama ya juu ya Rufani za Kodi. Endapo Serikali itaiwezesha ina uwezo wa kukusanya mapato zaidi na kuiwezesha Serikali, kila wakati hii Awamu ya Sita kuvunja rekodi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kupitia Mamlaka hii ya TRA naomba niiombe Serikali kwa kuwa imeonyesha jitihada kubwa, za kukusanya mapato ikamilishe zoezi la ajira za wafanyakazi 1,000. Kama Balozi wa Kodi naishukuru TRA na Wizara ya Fedha tumetembelea Mikoa, ya Kanda ya Kaskazini tumetembelea mipaka yetu Tarakea, Holili lakini na Namanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali kwa kuwa makusanyo ya mapato zaidi ya asilimia 45 yanatokana na ushuru wa forodha; na kwa kuwa chanzo hiki kinafanya kazi vizuri niiombe Serikali iboreshe miundombinu. Kwa mfano katika mpaka wa Tarakea Rombo unayo nafasi ya kuchangia mapato kiwango cha kutosha, lakini kwa kweli miundombinu haitoshelezi ikiwemo majengo, uhaba wa watumishi na uhaba wa vitendea kazi. Lakini sambamba na hilo niendelee kuiomba Serikali kuimarisha mifumo ya kukusanya kodi kupitia TEHAMA. Natambua jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika eneo hili la TEHAMA, lakini itawezesha wananchi na walipakodi kulipa kodi kwa ueledi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo tulipokea salamu za walipakodi wa Mkoa wa Arusha wakimpongeza Rais mama Samia pamoja na Mamlaka ya TRA. Kwa namna ambavyo kwa sasa hivi TRA imekuwa facilitator wanakaa pamoja wanazungumza, wanawezesha shughuli za kiuchumi ziendelee lakini wakati huo huo shughuli za kulipa kodi ziendelee. Kwa hiyo, nampongeza sana Kamishina wa TRA nampongeza sana Waziri wa Fedha na watendaji wote kwa kuwezesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niwaombe watanzania tuendelee kulipa kodi kwa hiyari tuendelee kudai risiti na wale wafanyabiashara waendelee kutoa risiti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuendelee kubainisha vitendo ambavyo vinapelekea kukwepa kodi kwa manufaa ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho niipongeze sana Serikali na Mheshimiwa Rais mahususi, kwa namna ambavyo mkopo wa shilingi trilioni 1.3 ulivyofanya kazi nzuri katika maeneo yetu. Kwa Mkoa wa Pwani tulipokea shilingi bilioni 17 tumepata madarasa 530 sasa hivi tumejielekeza kwenye miradi ya sekta ya afya, sekta ya maji. Kwa hivyo, kwa kweli na kama Kamati ilivyosema namna ambavyo mkopo huu ulisimamiwa kila mmoja, kwa nafasi yake tunayo nafasi ya mikopo mingine nayo kutoa tija nzuri na masuala mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)