Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Dr. Christina Christopher Mnzava

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipatia nafasi na mimi kuweza kuchangia katika hoja ambazo zimewasilishwa, nitakwenda kujikita kuchangia katika hoja iliyowasilishwa na Kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma. Tumeona katika taarifa iliyotolewa kuna baadhi ya changamoto ambazo zinakabili haya Mashirika ya Umma ambayo yamewekeza. Katika changamoto mojawapo ni Taasisi kutofanya kazi kwa pamoja kumekuwa na sintofahamu ya Taasisi mbili za Serikali, ambazo moja imewekeza lakini moja inasaidia nyingine kuweza kufanya kazi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano kuna Shirika la TANESCO pamoja na STAMICO. STAMICO tunajua kwamba ni Shirika la Serikali na limewekeza zaidi ya asilimia 99 ya mtaji na katika ndani ya Shirika la STAMICO, kuna Stamigold ambao wana kiwanda cha madini Biharamulo. Tatizo ambalo linatokea ni kwamba Stamigold ili kuendesha shughuli zake linahitaji umeme mkubwa sana karibia unit 1,300,000. Lakini tatizo lililopo ni kwamba Stamigold hawajaunganishwa na grid ya Taifa wanajikuta kwa mwezi, gharama ya kuendesha mitambo na gharama ya uchimbaji na uchenjuaji inatumia zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kununua mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama TANESCO wangeweza kuwaunganishia umeme grid ya Taifa, wangeweza kuokoa takribani shilingi bilioni 8 kwa mwaka kwa gharama ya mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyojua kwa sasa hivi lita ya mafuta ya dizeli ni Shilingi 2,500/= Stamigold wanatumia zaidi ya lita 600,000, kwa mwezi kwa ajili ya kuendesha mitambo na kwa ajili ya kufua umeme ili waweze kufanya kazi zao. Sasa basi, kama kunakuwa kuna mahusiano mazuri ya Taasisi mbili za Serikali ambazo zina lengo moja kuhakikisha kwamba, Tanzania yetu inakuwa na uchumi imara TANESCO wangefanya juhudi za makusudi kuhakikisha kwamba wamewaunganishia umeme kwa grid ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati imeshafuatilia sana lakini hata STAMICO wameshafuatilia sana suala hili. Mkienda maeneo ya tukio mkienda kwenye ule mgodi wakisikia Kamati inakwenda ndio mnakuta TANESCO, wameanza kuweka vifaa vyao wamechimba kama futi 2 tu mkiondoka shughuli inasimama sasa tatizo ni nini? Kwa sababu, Mashirika mawili ya Umma yanapofanya kazi pamoja tija na ufanisi vinaonekana dhahiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana Taasisi za Serikali ambazo zinategemeana kwa namna moja ama nyingine zihakikishe kwamba, kunapokuwa kuna uhitaji wa Shirika la STAMICO/Stamigold wanahitaji TANESCO ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi basi; ni vizuri Taasisi/mamlaka ambazo zinahusika kuhakikisha kwamba wanasaidia/wanawezesha Shirika moja kufanya kazi zao kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kabisa kwamba kunapokuwa na gharama kubwa za uendeshaji faida inakuwa kidogo. Kwa mwaka 2019/2020 STAMICO iliweza kutoa gawio la shilingi bilioni 1.1 kwa maana hiyo basi kama uendeshaji utapungua kwa kuwa na umeme wa uhakika, kutoka kwenye grid ya Taifa ni dhahiri kwamba hata gawio la Serikali litaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama STAMICO/ Stamigold wanatumia gharama kubwa au Shirika lingine lolote lile linatumia gharama kubwa kwenye uendeshaji, ni dhahiri kwamba lazima itapata hasara. Kwa sababu matumizi ya uendeshaji yanakuwa juu sana kwa hiyo, niwaombe sana sana sana Taasisi kutimiza wajibu wake kurahisisha utekelezaji wa Mashirika mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja nashukuru sana. (Makofi)