Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niwe miongoni mwa watakaochangia katika uwakilishi wa Kamati hizi mbili; ya Miundombinu na Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mimi nianze kwa kuwapongeza viongozi wote na Kamati zote mbili kwa kufanya kazi kubwa, hasa Wizara yetu ya Nishati na Madini, nina mambo mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza; Serikali Awamu ya Kwanza ilikuja hapa ikatuambia tuna upungufu wa mabwawa hayajajaa maji kwa hiyo tutakuwa na tatizo la umeme. Mwenyezi Mungu akashusha neema mvua zikaanza kunyesha. Wakati mvua zinanyesha wakabadilisha gia hewani wanafanya service ya mitambo siku kumi. Siku kumi zimekwisha lakini tatizo la upatikanaji wa umeme katika maeoneo yetu bado ni changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hayo kwa sababu watu tuliwapelekea umeme wakatoa zile mashine ambazo zilikuwa zinawasaidia kukoboa kwa njia ya mafuta. Unapokata umeme kwa wiki mbili au tatu unasababisha disaster kubwa sana katika maeneo yetu. Kwa hiyo mimi niiombe Serikali, kwenye hili hebu itusaidie. Wabunge wengi wametoa changamoto zao ikiwemo kuangalia namna bora ya kutatua hizi changamoto za ukatikaji wa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninavyokwambia katika kata zangu zaidi ya sita katika jimbo langu hazina umeme, kila siku umeme unakatika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ulitupa matumaini kuwa kazi inafanyika na tunaiona, lakini ongeza spidi utusaidie hili tatizo la ukatikaji wa umeme lisiwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmetuletea hapa bei ambazo Mheshimiwa Rais na Waziri naye ameanza kuzishughulikia, na wametuletea mwongozo kule ni vitu gani ambavyo vitasababisha wengine walipe 27,000 na wengine walipe 320,000. Mimi niiombe Serikali; wananchi wanaotumia umeme huu ni watu wa maisha ya chini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapompelekea umeme wa 320,000 wakati hata zile huduma za kuvuta umeme, yaani kununua vifaa vya wiring vya 200,000 vinawashinda, leo kweli tunakwenda kuwasaidia kwa kuwaongezea huduma ya kulipia nishati ya umeme ya 320,000? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhumuni la Serikali kwanza ni kutoa huduma kwa wananchi, siyo kufanya biashara kwa wananchi. Kwenye Kamati kule wametuletea TANESCO imepata faida. Sasa kama imeweza kupata faida kwa nini inashindwa kujiendesha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, hebu wakati wanaangalia changamoto ni nini ya kushindwa kujiendesha na waangalie watu gani ambao wanaweza kuwabana. Hatujakataa kwenye miji yetu mpandishe hizo tozo, lakini kwenye vijiji kule hali yetu ni mbaya. Kwa hiyo, mnatukataza watu wasijenge sekondari, mnatukataza watu wasijenge vituo vya afya, mnatukataza tusiwe na masoko wala huduma ambazo ni muhimu sana kwa maisha ya binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali ni kukusanya mapato baadhi ya maeneo, lakini kwenye hili hebu wajaribu kuliangalia. Hamuwezi kwenda kutuongezea gharama ya kulipa umeme. Wiring tu zenyewe wananchi zinawashinda. Maeneo mengi tumepeleka umeme kwenye vijiji, nyumba zilizounganishwa hazifiki hata asilimia 50, leo mnakwenda kuongeza gharama. Kwenye hili mimi niiombe Serikali ije na njia nyingine ya kuona namna gani tunaweza kuongeza huduma hii ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapeleka umeme wa REA kwenye vijiji. Tumejipanga na hii taharuki ambayo itakuja kujitokeza? Lazima tuwe na mbinu nyingine. Leo unapeleka kilometa 200 kutoka Makao Makuu ya TANESCO; je, ikitokea hitilafu ya umeme kule kuna mafundi, kuna wataalam? Sasa kuliko kupeleka umeme kule ikatokea shoti mnashindwa kuitafuta shoti imetokea wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo lengo la Serikali ni kupeleka umeme kwa kila kijiji lakini iangalie namna gani ya kusaidia isije ikatokea giza siku moja kwenye hii nchi kwa sababu ya ukosefu wa miundombinu kuwa bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikushukuru sana, niunge mkono hoja za Kamati. Nakushukuru sana kwa nafasi; ahsante.