Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

Hon. David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kwa kunipatia fursa hii kuchangia taarifa za kamati mbili zilizoletwa hususan kamati ya USEMI ambayo ndiyo wasimamizi wakuu wanaotusimamia sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naunga mkono mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati ya USEMI na nikiri wazi kabisa moja ya kamati ambayo imekuwa ikitushauri vyema kabisa sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni Kamati ya USEMI imekuwa karibu nasi nyakati zote na sisi bila kinyongo chochote haya yote waliyoyaandika hapa tumeyapokea na tutayafanyia kazi kama ambavyo yameletwa na kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa na mambo machache sana ya kuchangia kwa maana ya kuongezea tu. Jambo la kwanza ni kwamba kuna hizi fedha za maendeleo 40% kwa 60% zinazotokana na mapato ya ndani katika halmashauri zetu na sasa hivi Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi karibuni alitupatia fedha kupitia fedha za Mradi wa Mapambano Mhidi ya UVIKO-19 na fedha nyingi tulipeleka katika madarasa na inaonyesha kabisa kuna baadhi ya halmashauri kule wanataka kujifichia humu ndani ili miradi ya maendeleo iliyopangwa katika asilimia 40 na 60 waingizie katika hizi fedha za UVIKO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kamati ilivyoagiza na sisi tumeshaziagiza halmashauri zote nchini kuleta taarifa ya fedha za maendeleo ya zile asilimia 40 kwa 60 zinazotokana na mapato ya ndani zisihusishwe na fedha ambazo alizozitoa Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, hilo tulishaliagiza na kabla ya mchakato wa Bunge la Bajeti kuanza taarifa hiyo tutakuwa tunaileta kwako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili suala la 10% ambazo zinatokana na mikopo katika makundi maalum kwa maana ya wanawake, vijana pamoja na watu wenye mahitaji maalum kamati imeomba kwamba tulete marekebisho ya sheria pamoja na kanuni zake kwa sababu hilli tumeliona ni changamoto kwetu sote na Waziri wangu Mheshimiwa Bashungwa ameniambia kwamba tulipokee na kwamba hili tutaleta marekebisho ya sheria kamati itatushauri pamoja na Bunge lako tukufu ili tupate namna bora ambayo hizi fedha kila wakati zitakapokuwa zinatoka ziende zikafanye kazi ama tija ile ambayo imekusudiwa na Serikali pamoja na Mheshimiwa Rais mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ni kuhusu ajira ambalo tayari Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora ameshalizungumzia. Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeomba ajira sasa hivi kama nafasi 10,000 tumeomba kibali ambapo tukishapatiwa maana yake tutazitangaza ili ziende zikaongeze idadi ya walimu katika yale madarasa 15,000 ambayo Mheshimiwa Rais ameyatoa. Kwa hiyo, tusubiri Serikali ipo katika mchakato wake na inafanya kazi kwa kusikilizana litakapokuwa limekamilika Bunge lako Tukufu litapewa hiyo taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni kuhusu TARURA watu wengi wameizungumzia sana na Bunge lilishatuagiza hapa wiki iliyopita kwamba tulete taarifa ya tathmini ambayo tayari taarifa ya awali tumeshapatiwa kwa hiyo sasa hivi tunaandaa taarifa ya kina na tutaleta kwako katika Bunge Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tu niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge moja ya kazi nzuri ambayo amefanya Mheshimiwa Rais ni kupeleka fedha za kutosha kwenda kwenye halmashauri zetu pamoja na Majimbo hizi hela kwa ajili ya ujenzi wa barabara, na mfano mzuri zile shilingi milioni 500 kwenda kwenye Majimbo Mheshimiwa Rais ametoa fedha zote milioni 500 kwenda katika Majimbo 214 sawa sawa na bilioni 107. Kwa hiyo, zile ambazo tulishapitisha ndani ya Bunge kupitia mfuko wa Hazina Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ametimiza ahadi yake na zipo katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kinachofanyika huko tu ni kuhakikisha zifanye ile kazi iliyokusudiwa na Wabunge hawa wanapaswa na wao kutusaidia kuhakikisha kwamba wanazifuatilia hizi fedha zifanye ile kazi ambayo Mheshimiwa Rais amekusudia ifanyike kwa watanzania wote. Tuwaahidi tu kwamba tutakuwa tunatoa taarifa kwa kila Mbunge na sasa hivi tunaandaa mfumo ambao utasaidia sasa kuwa tunatoa taarifa kila fedha ambayo inatoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI iwe ni kama kwenye darasa iwe ni kama kwenye barabara iwe ni kama kwenye zahanati tunataka tutoe taarifa kama unavyopata zile automated mesages za kwenye simu zile tunataka tuwe tunawafikishia Wabunge ili wahakikishe wao wanauwezo wa kufanya hiyo kazi na kufuatilia hizo fedha kwa urahisi. Kwa hiyo nikushukuru sana na ninaunga mkono hoja za kamati zote mbili. (Makofi)