Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Niseme kwanza naunga mkono hoja za Kamati zote mbili ambazo zimewasilishwa kwenye Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu kwa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia kwa namna ambavyo ametupatia pesa nyingi kwenye Majimbo yetu na wananchi wamenufaika, wanashukuru sana. Pamoja na pongezi hizo naomba nami nitoe mchango wangu kwenye maeneo mawili kama siyo matatu kama muda utakuwa rafiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza kabisa nataka kuongelea kuhusiana na TASAF. Kwenye majimbo ambayo ni ya kijijini haifanyi vizuri sana kama ambavyo Serikali ina picha halisi. Wanufaika wengi wa TASAF kule Vijijini kiukweli siyo wale ambao walipaswa waingie kwenye Mfuko wa TASAF. Watu wengi ambao ni wazee na wengine ni walemavu hawana hata uwezo wa kukopeshwa kwenye ile asilimia mbili yao ambayo inapatika asilimia kumi kwenye Halmashauri wameachwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine niwaombe sana Viongozi wa Serikali, Mawaziri pamoja na Naibu Mawaziri wakubali tufanye ziara za kushtukiza twende kule ili wajionee uhalisia namna gani ambavyo wananchi wanalalamika. Tumeona wakati mwingine wakitembelea kwenye maeneo yetu wanapata ule msururu wanazongwazongwa hawapati picha halisi. Wakati mwingine wanapewa taarifa ambazo siyo sahihi kulingana na uhalisia ambao upo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TASAF wananchi wengi ambao wanapaswa kunufaika ambao kweli hawapati mlo na wengine hawawezi kujiendeleza kabisa hawajapata na wengine ambao ni watendaji hawafiki kwenye yale maeneo ili kuchukua takwimu halisi, wanawaachia Wenyeviti wa Vijiji, wanawaachia Wenyeviti wa Mitaa na wengine pia ni binadamu wanaingia kwenye tamaa wanawaingiza ndugu zao ilihali hawakuwa wanufaika na TASAF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia kwenye TASAF, sehemu nyingine nyingi ambazo tumeona kwenye TASAF, ile miradi ya maendeleo ambayo imeubuliwa imeisaidia jamii kwa ujumla hata ambao hawakupaswa kunufaika na TASAF. Zipo baadhi ya halmashauri za vijijini watalaam wake hawana utalaam wa namna gani ya kuandaa haya maandiko ili wayalete TASAF Makao Makuu waweze kunufaika na miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni kuhusiana na TARURA. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu tena kwa namna ambavyo alimpatia kila Mbunge wa Jimbo bilioni 1.5 ili ziweze kwenda kumsaidia kwenye miundombinu. Kwa upande wangu kwenye Jimbo langu tumeanza kuona mwanga kutoka kwenye bilioni 1.5 hii. Ombi langu na ushauri kwa Serikali, wakati natoa ombi nisisahau kumpongeza Chief wa TARURA Injinia Seif kwa kweli amekuwa ni mtu mwema sana anawasaidia Wabunge wengi na nimesikia watu wengine wakimsemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la TARURA tunaiomba Serikali kupitia Wizara yenye dhamana wawapunguzie TARURA mambo mengi wanapokuwa wamepata hela, kuwawekea vitu vingi mara sijui zabuni, vitu gani, inafika wakati wanaanza kutekeleza miradi hii wakati mvua zimekuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano sasa hivi kuna mafuriko, mkandarasi ameanza kulima barabara mwezi wa Pili, tarehe Mosi, leo tunavyoongea tarehe 14 Februari, barabara zote zimekwishasombwa na maji. Kwa hiyo, tunaomba pesa zinapotoka immediately watu wa TARURA waanze kufanya kazi mapema iwezekanavyo ili wafanye kipindi ambacho ni cha kiangazi, itatusaidia barabara zile zinapopitiwa na magari, zinapopitiwa na watu zinajishindilia lakini sasa hivi barabara zinaanza kutengenezwa mwezi wa Kumi na Mbili unapowauliza ni corrugations nyingi ambapo taratibu nyingi zinafanya hata zile pesa ambazo tumepewa na Mheshimiwa Rais zimepoteza thamani yake kwa sababu pale walipolima maji yamechukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, tunashukuru Serikali kwa kutujengea madarasa mengi lakini pia na watoto wakapata madawati. Walimu walisahaulika kwenye eneo hili, Walimu hawajapata fenicha, wamepata ofisi lakini hawana mahali pa kukaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na upungufu wa Walimu kwenye madarasa ambayo tumeyapata, naiomba Serikali, kama Serikali Kuu imekubali kwamba itawalipa Madiwani posho zao, tunaomba zile halmashauri ambazo hazina uwezo kwa sababu sisi wengine tunatoka kwenye halmashauri ambazo hazina uwezo, kwa hiyo hawataweza kuwaajiri watoto wao kupitia mapato yao ya ndani, tuombe hii iwe replaced na Madiwani kama watapata posho kutoka Serikali Kuu, kile ambacho walikuwa wanapata Madiwani basi wale vijana wenzetu ambao wako mtaani wamekaa zaidi ya miaka minne hadi mitano na watoto wamekaa bila kusoma basi tunawaomba vija hao wakachukue hizo nafasi hata wakilipwa shilingi laki nne ninaamini zitawasaidia sana. Ahsante sana. (Makofi)