Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Namshukuru Mwenyezi Mungu na naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuipongeza Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri; na Mheshimiwa Deo Ndejembi, Naibu Waziri, kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kushughulikia masuala yote ya maslahi kwa ujumla ya wafanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi hiki cha mwaka mmoja na miezi kadhaa tumeona kuna changamoto kubwa ya wafanyakazi na ajira, lakini tumeona takribani watumishi 180,000 wamepandishwa vyeo na kubadilishwa kada, lakini suala zima la madai pamoja na malimbikizo ya mishahara pia Serikali imeendelea kuhakiki pamoja na kulipa. So far mpaka sasa hivi watumishi takribani 37,000 wamelipwa madai yao na malimbikizo jumla ya shilingi trilioni 65 zimetumika, kwa hiyo tumeona nia thabiti ya Serikali kuendelea kushughulikia maslahi ya wafanyakazi, tunawapongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala zima la uhuishaji wa miundo ya maendeleo ya utumishi wa wafanyakazi. Hili suala nimekuwa nikilisema sana kwenye michango yangu, lakini sasa hivi kumekuwa na uhuishwaji wa miundo ya watumishi takribani 22 kwenye Wizara na 47 kwenye Wakala wa Serikali na Mashirika ya Umma. Kwa hiyo, tunaipongeza Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala zima la kutoa vibali. So far wametoa vibali karibu mia tisa kwa ajili ya kutoa ajira kwa nafasi zilizokuwa wazi, pia wametoa vibali karibu mia tano kwa ajili ya nafasi za uongozi, pia wametoa vibali 550 kwa ajili ya ajira ambazo sio za mkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wameshughulikia miundo mbalimbali, kwenye utumishi wa umma kuna miundo mingi, lakini sasa hivi kuna muundo mpya umetoka unasimamia utendaji wa kazi na upimaji wa Mtumishi.

Muundo huu utakuwa na tija sana kwa sababu mtumishi atapimwa, atajiandalia kazi zake na mwisho atapimwa kutokana na kazi zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundo iko mingi lakini kuna suala zima pamoja na pongezi nilizozitoa kuna suala ambalo limekuwa kero ambalo wenzangu pia wamelisemea ni kukaimu kwa muda mrefu. Watumishi wanakaimu kwa muda mrefu, naishauri Serikali sasa inaweza kuandaa kanzidata ili kupata uelewa wa watumishi ambao wana mwelekeo wa uwezo wa kupata hizi nafasi. Kwa hiyo, kuwe na mkakati maalum wa kuandaa hili jambo, limekuwa ni kero kubwa kwa watumishi. Watumishi wamefanya kazi kwa bidii wana uwezo, sasa ifikie sehemu wapate kuajiriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la watumishi Serikali imejitahidi kuajiri sasa, lakini bado kuna changamoto. Naishauri Serikali kama inawezekana kuanzia halmashauri zenye uwezo basi itoe vibali waajiri angalau kwa muda kwenye shule zetu na zahanati zetu, lakini zinapotoka ajira rasmi wale watu walioajiriwa kwa vibali hivi vya muda wapewe kipaumbele ya kuajiriwa kwenye ajira zitakazotoka. Hii itasaidia kuleta huduma njema ambayo sasa hivi inakosekana, japo tumepata hospitali na madarasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)