Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kidogo kwenye Wizara hii ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kuwapongeza Mawaziri; nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu kwa kazi kubwa anayofanya, anavyojituma kufanya kazi kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata hii huduma ya afya vizuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Naibu Waziri wake, naye ni jembe, anafanya kazi vizuri sana, tunaomba mwendelee hivyo hivyo, katika kuhakikisha kwamba tunaboresha huduma ya afya hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia yangu machache niseme kidogo juu ya huduma ya afya hasa kwenye maeneo ya vijijini. Nafikiri wote tunatambua kwamba Watanzania wengi wanaishi vijijini na ndiko huko Watanzania hawa wanapata matatizo makubwa sana ya huduma za afya. Kwa hiyo, tunapotaka kuboresha ni lazima tuwafikie hasa Watanzania walio wengi wanaoishi maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sera yetu imekaa vizuri kwamba kila kwenye kijiji tuwe na Zzhanati na kila kwenye Kkta lazima pawe na kituo cha afya na angalau kwenye Halmashauri kuwe na huduma ya hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niende kwenye Jimbo langu. Jimbo langu lina vijiji 45, lakini zaidi ya asilimia 70 kuna zahanati. Tukija kwenye vituo vya afya, tuna viwili tu. Kimoja kipo Lupembe, kilometa takriban 80 kutoka Njombe Mjini au toka kwenye Hospitali ya Wilaya ambayo ipo Halmashauri ya Mji na kingine kipo maeneo ya Kichiwa karibu kilometa 50 toka mjini. Kwa hiyo, unaweza ukaona jinsi gani wananchi wa maeneo haya wanavyopata shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa kwangu kule, kuna baadhi ya watu wanatembea zaidi ya kilomita 47 ili kupata huduma ya zahanati. Mgonjwa anatembea kilomita saba ili aweze kupata angalau huduma ya zahanati. Akikosa hapo anatembea umbali mwingine zaidi ya kilomita 25; angalau kukutana na kituo cha afya, halafu akitoka hapo akishindwa kupata huduma, anatakiwa kutembea takriban umbali wa kilomita 80 kwenda kwenye Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema kwamba kwenye Jimbo langu hakuna Hospitali ya Wilaya wala ya Serikali hata tu zile za binafsi, hazipo. Kwa hiyo, tuombe Wizara katika mipango yenu ya uboreshaji, angalau muwafikirie wananchi hao walio wengi wanaoishi vijijini. Hasa sehemu kubwa wanaoathirika hapa ni akinamama na akinamama wajawazito. Kule kwangu kwa sababu ya ubovu wa njia, hospitali kuwa mbali na vituo vya afya kuwa mbali, wengi wao wamekuwa wakijifungulia njiani, wakipoteza maisha wakiwa njiani kwenda kwenye Hospitali ya Wilaya kwa ajili ya kupata huduma ya upasuaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika mipango ya Wizara pia kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI angalau tuhakikishe kwamba vituo vya afya vilivyoko vijijini, viwe na huduma ya upasuaji ili tuweze kuokoa maisha ya akinamama wengi wa Tanzania wanaopoteza maisha yao wakati wanapotimiza haki yao ya msingi ya kuongeza watu hapa duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kama walivyosema wenzangu juu ya huduma ya CHF (Community Health Fund), inawasaidia wananchi wengi hasa wa vijijini na wengi wao wanaifurahia huduma hii. Lipo tatizo moja, kwamba wakishakatiwa hii CHF, haitumiki kwenye kata nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri ziweze kuunganishwa na Hospitali za Wilaya. Wakishakatiwa hii CHF basi waweze kuitumia hata kwenye Hospitali ya Wilaya au kwenye hospitali iliyo katika kata nyingine, ili kama anakosa matibabu, huduma au dawa hazipo kwenye hospitali ya Serikali au kwenye Kituo cha Afya cha Serikali, basi aweze angalau kwenda kwenye Hospitali ya Wilaya na akapata matibabu; kuliko ilivyo sasa hivi, wagonjwa hawa au wananchi wetu wakikosa kwenye kituo cha afya pale hawezi kwenda sehemu nyingine akatumia CHF. Kwa kuwa tumesema kwamba sasa matibabu yatakuwa yanatumika pia na TEHAMA, kwa kuwa jina litakuwa lipo kwenye database basi aweze kutibiwa sehemu nyingine kwa kutumia hii huduma ya CHF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo juu ya matibabu kwa wazee kama walivyoongelea wenzangu. Wazee wetu wanapata shida na tumesema kwenye ilani kwamba sasa tutaboresha huduma hasa kuhakikisha kwamba wazee wetu walio na umri unaozidi miaka 60 waweze kutibiwa bure. Bado kuna changamoto kubwa, kwa kuwa hospitali nyingi au zahanati na vituo vya afya vingi havina dawa za kutosha, hawa wazee wetu wamekuwa wakikosa matibabu. Tukumbuke kwamba wazee wetu hawa hawana uwezo wa kuzalisha, kwa hiyo, hawana uchumi mzuri, hawana fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri kwamba ni vizuri sasa badala ya kuwapa CHF, wapewe Bima ya Afya. Kwa kuwa ni wachache, basi Serikali ione umuhimu ya kuwapangia bajeti maalum wazee wote waliofikisha miaka 60 na wakapewa Bima ya Afya ili waweze kwenda kutibiwa kwenye hospitali zozote zilizoko hapa nchini kama ilivyo kwa wanufaika wengine wa Bima za Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo lingine juu ya miundombinu. Hospitali zetu na vituo vya afya vingi miundombinu yake bado siyo mizuri kwa maana ya huduma kama vile za umeme na maji. Utakwenda hospitali nyingi, utakuta zimejengwa vizuri, au kituo kimejengwa vizuri lakini hakuna maji. Naomba katika sera, katika mpango kwamba kila panapojengwa kituo cha afya au hospitali na maji pia yaweze kupelekwa katika maeneo hayo ili kuwepo na huduma bora. Wagonjwa wanaokwenda kwenye vituo hivi vya afya au hospitali basi wapate na huduma ya maji safi, kuliko ilivyo hivi sasa ambapo utakuta kuna hospitali nzuri, lakini inapofika kwenye huduma ya maji, haipo. Kwa hiyo, wanachota sehemu nyingine mtoni. Sasa hii ni hatari kwa mgonjwa kama kutakuwa na hospitali ambayo haina maji ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni umeme. Tumeona kwenye hospitali nyingi sana hasa zilizoko vijijini, hazina hata umeme! Tupeleke umeme! Kama siyo kupeleka umeme ule wa REA basi tuwe na mipango ya kupeleka umeme wa solar, unaweza ukasaidia. Kwa hiyo, kila tunapojenga hospitali au tunapopeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ni lazima tufikirie pia na umeme, tuanze kufikiria na power itakayotumika kwenye kijiji, kituo cha afya au hospitali, ili wananchi waweze kupata umeme kwenye hizi hospitali zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho niseme kama walivyosema wenzangu juu ya unyanyasaji wa kijinsia. Tunaomba tuweke mipango rasmi kabisa ya kuhakikisha kwamba unyanyasaji wa kijinsia nchini kwetu unatokomezwa. Mpaka sasa hivi kuna maeneo mengine, akinamama ambao wamefiwa na waume zao, wanalazimishwa kwenda kuolewa na wadogo wa wenzi wao waliofariki. Bado kuna maeneo mengine wanalazimishwa kugawanya mali. Maana ndugu wanachukua mali za huyu marehemu aliyefariki, eti kwa sababu ya kulelea familia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tujaribu kujitahidi kuhakikisha kwamba akinamama wanaopoteza wenzi wao wajane hawa, wanatetewa na mali zao zinabaki kwa ajili ya kuendelea kuhudumia familia zao kuliko ilivyo sasa hivi kwa baadhi ya maeneo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na naunga mkono hoja.