Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Naungana na wenzangu kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati zetu pamoja na Waheshimiwa Mawaziri, wataalam na wadau wote ambao tumeshirikiana nao kwenye Kamati zote kufanya hii kazi, pia kipekee na kwa upendeleo, wale ambao wanaangukia kwenye Kamati yangu ya Katiba na Sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo ambalo liko wazi kwamba pamoja na majanga yote ya kidunia na nini lakini uchumi wa nchi yetu umeendelea kukua na Mheshimiwa Raisi Mama Samia Suluhu Hassan katika Awamu yake ya Sita amekuja na kauli moja ya kusema kwamba tunaifungua nchi yetu kwa ajili ya kukuza uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli hii sio kauli ndogo, ni kauli kubwa sana; na mimi ninachofurahia juu ya Wizara na wadau wote wanaoingia kwenye Kamati ya Katiba na Sheria ni kwamba wamejitahidi kufanya kazi kubwa sana katika kupata mambo mawili; jambo la kwanza kujenga mazingira katika kuifungamanisha nchi yetu na dunia kwa sababu ndiko teknolojia na mitaji iliko, lakini pili kujenga mazingira ya sisi wenyewe Watanzania kwenda na hiyo hali mpya ya kujifungamanisha na dunia. Kwa sababu unajua unapofungua dirisha hewa iingie hata papasi na panzi huwa wanaingia kwa hiyo lazima pia ndani ujipange, ukishajifungamanisha na dunia yako mengi yanayoingia kwa hiyo lazima ujipange kwenda nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hapa nazungumzia mfano wa taasisi zetu za usalama kazini; OSHA na Workers Compensation pamoja na hifadhi ya jamii (pension). Taasisi hizi zimefanya kazi nzuri na hata ukizipima kwenye vigezo vya blue prints wametekeleza kwa kiwango kikubwa sana na ndio maana kama taasisi ya OSHA imeweza kujifikisha kwenye viwango vya kimataifa kiasi cha kuweza kupata dawati katika mambo ya usalama kazini pale SADC, hii ni hatua kubwa ambayo kwa kweli tunapaswa kuiona kwamba taasisi imetuwakilisha vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, OSHA ikifanya kazi yake vizuri, majanga yakapungua mahali pa kazi, mzigo unapungua Workers Compensation kwenye fidia, kwa sababu kunakuwa hakuna ajali ajali. Mzigo ukipungua kule wale wanapata nafasi ya kuwekeza na kwa ajili ya kukuza uchumi wetu. Hali kadhalika watu wa pension wakifanya kazi zao vizuri inaongeza ufanisi kwenye kazi na inapunguza hata matatizo ya rushwa kwa sababu wakati mwengine ufanisi na mambo ya kudaidai rushwa pia yanatokana na hofu ya kustaafu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anajiuliza fine nafanya kazi leo nna mshahara mzuri lakini nikishaafu kesho itakuwaje. Kwa hiyo kama kuna taasisi hizi za hifadhi za jamii ambazo zipo stable hiyo pia zinatusaidia hata katika mambo kama haya ya kupunguza rushwa na kuongeza ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kweli kwa kipindi hiki cha mwaka mmoja ambapo tumepata fursa ya kuziangalia taasisi hizi, kazi imefanyika vizuri na tunazipongeza na tunadhani kwa viwango vya blue print na viwango vingine wanapaswa kuigwa kwa ufanisi mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sekta wa utoaji haki; Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu pamoja na DPP pia wamefanya kazi nzuri, zipo changamoto za upungufu wa watumishi pamoja na masuala ya kibajeti, hali hiyo sasa ni jukumu letu kushirikiana nao kwamba wakati wa bajeti ikija tuwapitishie bajeti nzuri kwa sababu wameshaonyesha uwezo wa kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata sheria ambazo tumezipitia, tumeangalia jumla ya Miswada sita ambayo inarekebisha sheria 58 almost. Hizi zote zimekaa kimkakati wa kuisaidia nchi yeti katika kupiga hatua za kiuchumi, kwa sababu tuseme yote lakini uchumi ndio kila kitu, hali ya nchi itakuwa nzuri uchumi ukiwa vizuri. Kwa hiyo, zipo sheria kubwa ambazo zimezungumzwa hapa na wenzangu kama mabo yale ya nolle prosequi na mambo mengine ya kukamilisha upelelezi kabla ya kupeleka watu Mahakamani ni mambo mazuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ziko sheria nyengine ambazo sio rahisi kuzi-note lakini bado zina-impact sana katika masuala ya uchumi wa nchi. Kwa mfano marekebisho ya Sheria ya Makampuni ambayo tuliyapitisha. Ooh! Naona kengele imelia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia sentensi yako.

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Basi labda tu niseme kwamba sheria zote ambazo zimepitishwa kwa kweli nimekuwa nimejiandaa kuzitaja zote zimekaa kimkakati kusaidia nchi yetu kuweza kujifungamanisha na dunia na kurahusisha mambo ya biashara za kimataifa, lakini pia kulinda haya mafanikio yanayokuja na kuwalinda Watanzania katika mchakato huu unaokuja wa uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo na kwa ajili ya muda basi nuinge mkono hoja kwa asilimia zote ahsante sana. (Makofi)