Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimpongeze sana Mwenyekiti kwa wasilisho lake zuri, lakini pia niipongeze Serikali kwa maana ya Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya, hasa hasa Waziri wa TAMISEMI kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache ya kuchangia ambayo yamejikita kwanza kwenye upungufu wa wafanyakazi. Kwanza tuipongeze Serikali kwa kazi kubwa ambayo imeifanya ya kujenga vituo vya afya lakini pia kuongeza ujenzi wa madarasa katika sehemu mbalimbali za nchi hii. Hata hivyo, changamoto kubwa ambayo tumekuwa nayo ambayo tunaipata hadi sasa hivi ni wimbi kubwa la vijana kukosa ajira ambapo mimi kama Mbunge ningependa kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na watu wengi kustaafu, lakini pili kumekuwa na wenzetu ambao wanafariki na kutangulia mbele ya haki. Hawa wote tungetamani nafasi zao ziwe zinajazwa kwa wakati, kwa sababu wanakuwa wako kwenye payroll ya Serikali. Hii ingeweza kusaidia kuendelea kupunguza gaps lililopo la watumishi kwenye nchi yetu ambalo limekuwa ni kubwa. Kuna watu ambao wamemaliza toka miaka 2012, 2013, 2014 hawajaajiriwa hadi wanakuwa wazee, wamekosa ajira. Kwa hiyo, tungeiomba Serikali na ningeishauri Serikali ijitahidi kutoa vibali mapema kwa hizi gaps ambazo zinakuwa zipo za watu ambao wamestaafu na wangine wametangulia mbele ya haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine, ni kwenye suala la fedha za miradi. Kwanza tuipongeze sana Serikali, mama yetu anaupiga mwingi sana. Mama Samia anaupiga mwingi sana kwenye ujenzi wa miradi kwenye nchi hii. Unaweza ukaangalia kwa asilimia 100 kama siyo 90 na kitu halmashauri zote nchini zimepata fedha za maendeleo za bajeti ambazo walikuwa wameomba, ni kitu ambacho hakijawahi kutokea kwa miaka mingi toka tumepata uhuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ambayo tunaipata, kwenye uwiano wa kugawa fedha hizi. Watu walioko Makete, Kiteto, Nyamagana kule Mwanza, Musoma, Mbinga na watu waliopo maeneo mbalimbali anapewa milioni 20 ajenge darasa, wakati huo huo hiyo milioni 20 anapewa mtu aliyopo Dar es Salaam ajenge darasa. Halafu tunategemea hawa watu wote wawe na darasa sawa la Dar es Salaam na la Makete kule Ipepo, na la Makete kule Matamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto inayokuja kujitokeza, watu waliopo kule mikoa ya mbali kama Kigoma, Makete Wilayani wanahangaika kuhakikisha wana-meet kile kiwango ambacho Serikali imetaka darasa likamilike, lakini si kwa zile fedha ambazo muda mwingine zimetolewa na Serikali, wanakwenda kuingia hadi mifukoni mwao kuhakikisha wanatekeleza lile jambo ambalo Serikali inataka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungetumia mfumo ambao EWURA wanavyofanya kwenye kugawa mafuta. Bei ya mafuta Dar es Salaam ni tofauti na bei ya mafuta iliyoko Mwanza. Ndivyo ambavyo tunatakiwa tufanye hivyo hata kwenye miradi hii ya Serikali, angalau tungetambua kwamba Zone hii ya Mwanza au Lake Zone au Zone ya Mbeya, ujenzi wa madarasa siyo milioni 20 kwa darasa moja, ni milioni 25. Wangefanya hivi ingeweza kusaidia kwa watumishi na wafanyakazi wetu waliopo kule chini, kwa sababu wana- suffocate, wanapata wakati mgumu, kuhakikisha kwamba wana-meet kile ambacho Serikali inataka, lakini usawa huu ungeondolewa ili kuweza kuwasaidia ndugu zetu ambao wapo huko wanahangaika na kutekeleza miradi ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ningeomba sana watumishi walizingatie, wanateseka sana Watendaji wa Kata, wanabanana sana na Wakurugenzi kuhakikisha kwamba hii miradi inakamilika kwa uwiano wa kugawa fedha kwenye majimbo yote nchini, wangetenga kwa zone ingetusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho, ni kwenye suala la Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma. Hii Sekretarieti imeanzishwa kwa sheria, ibara ya 132 kwenye Katiba yetu, ndiyo ilianzisha hii Sekretarieti ya Maadili ya Umma. Changamoto ambayo tunaipata kwenye hii Sekretarieti ya Maadili ya Umma. Tumekuwa na changamoto ya Viongozi wengi na watumishi wengi wa Serikali kutokuwa na maadili ya umma kama ambavyo tunatoka kwenye sheria, lakini hii Sekretarieti imekuwa kimya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya majukumu yake wanasema, kuna mojawapo wanasema, Sekretarieti ya Maadili ya Umma inasema to conduct investigation into allegations or complex against any public leader. Sasa tumeanza kushangaa kwamba hadi anakwenda Rais anasema hadharani kwamba kiongozi huku amefanya moja, mbili, tatu, nne, tano au hadi watu waweke bango barabarani kwamba kiongozi huyu ana moja, mbili, tatu, nne, tano, lakini hii Sekretarieti ya Maadili ya Umma ilikuwa na kazi hiyo ya kufanya investigation kujua viongozi wapi wanafanya moja, mbili tatu ili achukuliwe hatua za haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna vijana ambao wanahangaika mahakamani kwa kesi mbalimbali, lakini kuna mambo yalikuwa wanayafanya hadharani na hii Sekretarieti ilikuwa kimya, lakini leo hao viongozi wanahangaika kwenye hayo mambo.

Kwa hiyo, nasema Serikali ione umuhimu wa kuhakikisha kwamba Sekretarieti ya Maadili ya Watumishi wa Umma inafanya kazi kwelikweli kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa Wakurugenzi na wateuliwa wengine wa Rais ambao wamekuwa wakikiuka maadili na tunawaona wapo kimya na hii Sekretarieti ya Maadili ya Umma ipo kimya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ingefanya kazi vizuri, ingewasaidia hata vijana ambao wanakua wajue kuna chombo ambacho kinafanya kazi kabla ya Mheshimiwa Rais kuchukua hatua. Hiki chombo ambacho kiliundwa na Sheria na ni chombo huru, kina uwezo wa kufanya kazi hadharani na watu tukaona tukajua nchi yetu ukikosea hiki unachukuliwa hatua hii, lakini sasa tumeona kwamba kumekuwa na ukimya huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti baada ya kusema hayo nikushukuru sana na naunga mkono hoja.