Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuanzia Januari, 2021 hadi Februari, 2022 pamoja na Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuanzia Januari, 2021 hadi Februari, 2022 pamoja na Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie suala la Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili ni la muda mrefu na kama ripoti ya Kamati ilivyooneshwa hatujaridhishwa kabisa Wanakamati na taarifa tunazozipata kuhusu mwelekeo na muendelezo wa mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu tunachoambiwa ni kwamba uko kwenye majadiliano. Majadiliano haya ambayo hayaishi tunashindwa kuelewa ni majadiliano gani. Tuna uhakika kabisa wataalam wetu wana uwezo wa kufanya majadiliano na tumewaamini na tuna hakika pengine wanapigania maslahi makubwa ya nchi yetu ili tupate mkataba mzuri, lakini miaka 11 toka mkataba umesainiwa mpaka leo hatujaweza kukamilisha jambo hili? Hivi hatujui na hatuoni umuhimu wa chuma katika maendeleo ya nchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kusema wote tunafahamu majadiliano siku zote sio lazima ushinde kila kitu, lakini majadiliano yanataka compromise, ufike mahali ukubaliane na hasa kama unajua lengo lako ni nini. Sasa sisi tunaelewa chuma tunahitaji, tunaelewa mradi huu ni mkubwa, mradi huu utabadili maisha ya watu, mradi huu tunaouita mradi wa kielelezo, mradi huu tunauita upo katika mpango wa kwanza ulioishia 2021, upo kwenye mpango wa pili unaoishia 2026, upo kwenye kila bajeti ya kila mwaka, upo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Ndugu zangu, hivi tunataka nini? Tunafahamu kabisa kwamba tunapoteza kwa kutoendelea na uwekezaji kwenye mradi huu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi napenda kupendeza; nafahamu Waheshimiwa Wabunge kwamba Kamati yetu inajaribu ku-negotiate ili tupate better terms, lakini nitoe ushauri hebu wajaribu kuangalia maslahi mapana ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, unajua approach ikiwa ni kuangalia negotiations kama kama kihasibu, unaangalia tu faida kwamba, tutapata faida, hatupati mpaka mwisho unapiga hesabu unasema hapa hatupati faida, nadhani hiyo approach sio nzuri. Waende na approach ya kiuchumi ya kuangalia multiplier effect kwenye mradi huu; mradi huu ajira 5,000 za moja kwa moja, mradi huu ajira 33,000 ambazo hazitakuwa moja kwa moja. Ndani ya mradi huu…

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mchango mzuri sana wa Mheshimiwa Mbunge, Mradi huu wa Liganga na Mchuchuma, sio tu kwamba utasaidia kuzalisha chuma ambacho tungeweza kutumia katika maendeleo mengine, lakini ni mradi ambao ni unganishi kwa kuendeleza pia Makaa ya Mchuchuma na chuma cha Liganga,

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa maana hiyo, kulikuwa na mpango sahihi kabisa wa kuzalisha megawati 600 ambazo nyingine zingetumika kuchenjua chuma na megawati nyingine 400 zingeingizwa katika njia ya msongo wa kilovoti 400 pale Makambako ili uweze kuingia kwenye Gridi ya Taifa kwa hiyo, ni mradi muhimu kwa ustawi na maendeleo ya nchi.

NAIBU SPIKA: Ahsante, Mheshimiwa Mwanyika, Taarifa hiyo.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana kaka yangu kwa kuendelea kunifilisi nilichotaka kuongea, lakini niseme mradi huu ni special. Mradi huu ukiuangalia kwa haraka upande mmoja ni mradi wa kiuchumi, lakini ni mradi wa kiundombinu; tunaongelea ujenzi mkubwa wa reli katika mradi huu ambao utaiunganisha Bandari ya Mtwara, inakuja mpaka Manda inapata mchepuko inakuja kwenye huu mradi. Kwa hiyo, ajira ngapi zitazalishwa katika hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuangalie kitu kingine, tunatumia fedha nyingi sana nnchi hii katika masuala ya chuma; ujenzi wa maghorofa, ujenzi wa madaraja, ujenzi wa SGR, ujenzi wa towers. Mheshimiwa Naibu Waziri hapa ameongea kwamba hatuna towers, nchi hii ina towers za simu zaidi ya 10,000; hivi hiyo miradi yote hiyo ya towers ni chuma na sisi chuma tunacho hapa na tunalialia kwamba, hakuna towers za kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia ni mengi, miradi hii itapunguza gharama nyingi sana ya vitu vingi. Kwa mfano, tunaongelea uzalishaji wa gesi, nani anafahamu?

Mheshimiwa Naibu Spika, kifungashio cha gesi unachokiona, unakiita cylinder, asilimia karibu 50 ya ile gesi, gharama…

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kumpa Taarifa kaka yangu Mheshimiwa Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini kuhusu suala la Liganga- Mchuchuma sio tu itasaidia hayo anayoyasema, lakini pia itasaidia kuanzisha viwanda vya magari katika nchi yetu. Kwa hiyo, itaongeza na kukuza uchumi kwa zaidi ya asilimia 100. Ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Haya, ahsante. Taarifa hiyo.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubali taarifa na mambo ni mengi ni mengi sana ambayo chuma kingetusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kumalizia kwa kusema wenzetu Serikalini watusaidie. Mheshimiwa Engineer Chiwelesa amesema huyu mwekezaji kama hawezi basi aondolewe, lakini tunachoambiwa ni kwamba kuna tatizo la tax incentives au vivutio.

Sasa mimi nimeangalia vivutio vinavyoongelewa, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, hivi vivutio vinavyoongelewa kwa mradi mkubwa wa aina hii tuangalie maslahi makubwa kwamba tukijenga hii infrastructure ambayo ni Liganga – Mchuchuma, power na steel, tukajenga na hizi reli, uchumi mkubwa wa eneo zima la Kusini utasisimka na tunaweza tukapata hii kodi ambayo tunaweza tukaisamehe hapa mwanzoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata ukiziangalia hizi kodi zinazoongelewa hapa tuliuliza swali hivi tunazipata leo? Kwa hii chuma kuwa bado hazijachimbwa? Tunazipata hizo kodi? Hatuzipati.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Kwa hiyo, tuliangalie kwa karibu nashukuru muda ni mfupi lakini naunga mkono hoja. (Makofi)