Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kwanza kukushukuru wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kuwa hapa leo na kuweza kuchangia Wizara. Kwanza nianze kumpongeza Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi wanazozifanya, lakini pia kwa kutusaidia katika Majimbo yetu tunapokuwa tuna shida.
Mheshimiwa Spika, lakini umeongelea kwamba tusichangie zahanati na mambo mengine kwa sababu yako TAMISEMI. Tunaomba tuendelee kuchangia kwa sababu tunajua kabisa Wizara ya Afya inasimamia sera. Kwenye Jimbo la Segerea kuna watu 500,000 na katika Jimbo la Segerea kuna kata moja ambayo ni Kata ya Vingunguti ndiyo inayoongoza kuwa na watu wengi Tanzania nzima. Kata hii ya Vingunguti haina zahanati wala haina Kituo cha afya. Juzi Mheshimiwa Naibu Waziri alisema kwamba wanategemea kukipandisha kuwa kituo cha afya hospitali ya Kata ya Segerea na Segerea ni mbali.
Mheshimiwa Spika, pia akazungumzia zahanati ya Plan International ambayo iko Mnyamani. Zahanati hii kwanza imebanwa na nyumba nyingi na hawa watu wameomba kuondoka, lakini mpaka sasa hivi hawajapewa fidia ili waweze kuondoka. Hapa kwenye hii Kata ya Mnyamani, kwanza kuna mabwawa ya maji taka na mlipuko wa magonjwa ukianza tu tunaanza na hii Kata ambayo tayari ina watu wengi, lakini pia kuna mabwawa ambayo yanasababisha watoto kuanzia zero mpaka miaka mitano waweze kuugua kwa wingi.
Mheshimiwa Spika, tumeshafanya research kwenye hii zahanati kwa kupita kwenye hii Kata ya Mnyamani, tumegundua wagonjwa wengi wanaopelekwa kwenye hiyo Plan International ni watoto wadogo wa kuanzia mwaka mmoja mpaka miaka mitano.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaomba pamoja na kwamba tusizungumzie sana suala la zahanati na mambo mengine katika hii Wizara, lakini tunaomba Waziri dada yangu Ummy pamoja na Naibu Waziri msimamie sera inayosema kwamba kila Mtaa uwe na zahanati, lakini kila kata iwe ina kituo cha afya, ambapo Jimbo la Segerea lina mitaa 60 na lina zahanati kumi. Kwa hiyo, unaweza kuona kabisa kwamba Watanzania ambao wanaishi Jimbo la Segerea wanateseka kiasi gani kwa kukosa huduma za afya.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Spika, naomba tu nielezee kidogo kwamba mimi nimekuwa Diwani kuanzia mwaka 2010 mpaka mwaka 2015.
Mheshimiwa Spika, Manispaa ya Ilala ina mambo mengi ambayo yanajitokeza, tunayaita mambo ya zimamoto, kwa hiyo, bajeti nyingi ambazo zinatengwa katika Manispaa ya Ilala zinakwenda kwenye shughuli nyingine ambazo zinakuja, haziko kwenye programu na hii ndiyo imekuwa kila wakati inatufanya sisi tusiweze kujenga zahanati.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2014 tulipanga tujenge zahanati, lakini ikashindikana kwa sababu pesa tulizopanga kujenga zahanati Serikali ilielekeza tukajenge maabara na ndiyo maana tumeshindwa kujenga zahanati mpaka sasa hivi. Sasa hivi nimekuwa Mbunge, nimeona haya matatizo tuliyokuwa nayo kama Diwani niyalete kwenye Bunge ili Mheshimiwa Waziri aweze kuyatatua.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo Mheshimiwa Waziri ameongelea udhibiti wa ukatili wa kijinsia…
SPIKA: Suala moja tu la eneo, mmeshatenga eneo pia?
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Spika, eneo lipo lakini kila mwaka Manispaa ya Ilala inaweka kwenye programu kwamba itajenga, lakini hizo zahanati hazijengwi mpaka sasa hivi na ndiyo maana tunaomba Waziri akishirikiana na Waziri wa TAMISEMI waweze kututatulia hili tatizo na hela zinakwenda kwenye mambo niliyokwambia, mambo ya zimamoto na mambo mengine ya madeni.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amesema atashirikiana na wadau mbalimbali ili kuweza kutatua tatizo la ukatili wa kijinsia. Naomba Waziri aweke mikakati kwa sababu suala la ukatili wa kijinsia limekuwa kubwa, akisema atashirikiana pengine inaweza isitoshe. Kuna wasichana ambao, sisi tulitembelea Gereza la Segerea, tumekuta wasichana wadogo ambao wana miaka 14, miaka 13 ambao walikuwa ni ma-house girl wa watu, wamewaweka ndani. Cha kushangaza au cha kusikitisha au cha kuchekesha wale watoto wamefungwa miaka miwili kwa kosa la kwamba amechana dera la bosi wake. Kwa hiyo hii tunaita ni ukatili wa kijinsia.
Mheshimiwa Spika, wengine wamepoteza shilingi 30,000, anasema alitumwa mboga, bosi wake kaamua kumpeleka polisi na hatimaye kumpeleka mahakamani, hatimaye yule mtoto mdogo na innocent anakwenda kufungwa. Sasa tusipolifanyia mkakati hili jambo la ukatili wa kijinsia. Hawa watoto wako innocent, wanakwenda kule gerezani, Gereza la Segerea wanakutana na watu wengine ambao ndiyo wahalifu wa kweli, kwa hiyo, wanapokaa ile miaka miwili wakitoka kule ndani wanakuwa wameshajifunza kuwa wahalifu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaomba Mheshimiwa Waziri, watoto kama hawa kwanza napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru Chama cha Wanasheria Wanawake ambao hili jambo baada ya kuliona waliamua kulifuatilia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba umesema utashirikiana na wadau, lakini pia tunaomba uweke mikakati ambayo inaweza ikasaidia. Tunajua kabisa kwamba unapochukua mfanyakazi wa ndani, unapoamua kukaa naye, anakuwa ni part ya familia, kwa hiyo hawezi kutendewa mambo mabaya.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia mi Benki ya Wanawake. Naishukuru sana Serikali iliamua kuanzisha Benki ya Wanawake mwaka 2009, lakini cha kushangaza hii Benki ya Wanawake haisaidii wanawake walengwa, inasaidia wanawake ambao tayari wana pesa zao kwa sababu hawa wanawake walengwa wako ndani kwenye kata ambao wanafanya biashara ndogo ndogo, lakini hawawezi kufika huku na hawajui process za kufika katika hiyo Benki ya Wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna Bibi Maendeleo au Maafisa Maendeleo wako kwenye kata zetu. Wale Maafisa Maendeleo kazi zao ni kuangalia kata na kuhakikisha kwamba akinamama wanakuwa na maendeleo, lakini wale Maafisa Maendeleo hawafanyi hizo kazi. Kwa hiyo, kuna akinamama ambao wanahitaji wapate tu shilingi 50,000 ya mtaji ili aweze kupika vitumbua au kupika chapati hajui pa kuzipata. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri ili aweze kuliangalia hili jambo na kushirikiana na Mkurugenzi wa Benki ya Wanawake, waangalie watawafuata vipi akinamama ambao wako mitaani ili waweze kusaidika.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine la mwisho, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kumteua mwanamke aongoze hii Wizara. Tunaomba Mheshimiwa Waziri, akinamama wanaokwenda kujifungua hasa wa vijijini, mtu anaumwa uchungu, hivi mtu ukiwa unaumwa uchungu utabebaje mafuta ya taa au taa uende nayo ili uweze kujifungua? Tunaomba ushirikiane na Waziri wa Nishati ili hizi zahanati zipate umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Waziri tunaomba hawa akinamama ambao wanaambiwa waende na gloves, waende sijui na pamba. Naomba ukisimama katika majumuisho yako utoe tamko hii iwe mwisho, mama anakwenda kujifungua aende bila kitu chochote na kila siku sisi tunasema akinamama jeshi kubwa, ushindi ni lazima, kwa hiyo, lazima tuwakumbuke akinamama wetu ambao tumewaacha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.