Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuanzia Januari, 2021 hadi Februari, 2022 pamoja na Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuanzia Januari, 2021 hadi Februari, 2022 pamoja na Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikupatie pongezi nyingi sana na nikutakie kila la kheri kwenye nafasi yako ya Naibu Spika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona nichukue point moja tu ya kusisitiza kutoka kwenye Kamati yetu ya Kilimo. Kamati imetoa mapendekezo mazuri mno na yameandikwa vizuri mno, kwa dakika tano hizi naongelea kitu kimoja tu na ni kuishauri Serikali irudishe tena Tume ya Mipango na nitatoa sababu hapa kwa nini Tume ya Mipango ni muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Tume ya Mipango (Planning Commission) ipo chini ya Wizara ya Fedha ndiyo maana inaitwa Wizara ya Fedha na Mipango, lakini inakuwa ni kama Idara, sasa kama ni Idara ndani ya Wizara haina mtizamo wa Kitaifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano wa Mkoa wa Mara kwa nini Tume ya Taifa inahitajika. Mkoa wa Mara viwanja vya ndege kuna kiwanja cha Musoma Mjini, mimi nimezaliwa pale Mjini, kiwanja nimekikuta wanakikarabati sasa hivi, kabla ya Baba wa Taifa hajastaafu kuna eneo limetengwa kabisa Nyasurura, Musoma Vijijini ilikuwa itengenezwe airport kubwa ambayo ingehudumia hata sehemu zingine za Afrika Mashariki na nje, kwenye Ilani ya Uchaguzi kiwanja hicho kimo, juzi sisi tumekabidhi Bodi ya Viwanja kwamba jamani chukueni kiwanja mjenge.

Kwa hiyo, Musoma Mjini tuna kiwanja, toka enzi ya Mwalimu tumekuwa na kiwanja kingine kikubwa, nadhani mmesikia Serengeti Mugumu na wao wanataka kuwana kiwanja, sasa kipi ni bora katika hivi vitatu ndani ya Mkoa mmoja?

Mheshimiwa Naibu Spika, inamaanisha tunaopanga hatuna picha kubwa ya Kitaifa. Unachukua Mkoa jirani wa Simiyu na wenyewe wanataka kiwanja, Mwanza kuna kiwanja, ndiyo maana Planning Commission ingekuwepo vitu kama hivi vingeliweza kushughulikiwa kwenye picha kubwa ya kitaifa umuhimu wa hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano wa pili ni ujenzi wa barabara; tumeshauri TANROADS, huu mpangilio wa sasa wa kilometa tano/tano, Waheshimiwa Wabunge kila mtu ana furaha ana mradi wa barabara lakini kila mtu ajiulize utaisha lini? Mimi nina barabara ya kilometa 92 karibu kilometa 100, wamepewa kilomita tano, kwa hiyo muda mfupi kabisa kama pesa zinatakiwa kutoka ni miaka 20, lakini Planning Commission ingekuwepo ingeona ni barabara zipi ambazo ni muhimu kiuchumi badala ya kujenga kilometa tano/tano labda wangekuwa wanajenga angalau kilometa hamsini kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine ni mambo ya umwagiliaji; tunaongea kila mbunge hapa ana scheme yake lakini uwezo wetu wa kifedha hatuwezi kuwa na irrigation scheme kila Mkoa, kila Wilaya, hatuna ubavu huo wa fedha. Kwa hiyo, Planning Commission ingekaa ikaona ni yupi na wapi tuwekeze zaidi tuweze kuanzisha kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo, ukija kwenye ujenzi wa mambo ya vyuo vya VETA, kama nini Mbunge wa Musoma Vijijini sihitaji VETA ya kufundisha watu kutengeneza magari, ninahitaji VETA ya watu wa mifugo, kilimo na uvuvi. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Profesa Muhongo.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja muda ungepatikana ningewaeleza zaidi. Ahsante. (Makofi)