Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nami namshukuru Mungu sana kupata nafasi hii ya kuzungumza katika hii hoja ya Kamati mbili. Hoja yangu kwanza nitajikita kwenye Kamati ambayo imevuta hisia za watu wengi, Kamati ya Maliasili.

Mheshimiwa Spika, sitaki kuchukua muda mwingi kwa pongezi. Umeshapongezwa sana, nami nakupongeza wewe pamoja na wote waliochaguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mambo mengi sana yamezungumzwa hapa na Waheshimiwa Wabunge, lakini kama mtakumbuka siku Mheshimiwa Rais anawaapisha Makatibu Wakuu, alisema tuchague jambo moja kati ya mambo mawili; au tuache Hifadhi ya Ngorongoro ife iwe makazi ya watu moja kwa moja au tuihuishe ile hifadhi iendelee kuishi kwa manufaa yetu na ya vizazi vyetu. Hii ni kauli nzito sana kutoka kwa mkuu wa nchi. Mheshimiwa Rais anataka sisi Watanzania tuchakate halafu tuishauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ushauri wangu ni huu; Waheshimiwa Wabunge, wamesema hapa lakini kwa bahati mbaya sana ukweli huwezi kuufunika. Ukitazama maudhui ya kuwaruhusu wale watu 8,000 waishi mle na wanyama, kulikuwa na masharti yake; usijenge nyumba ya kudumu, jenga nyumba za kimila, ambazo zitawavutia watalii watakapokuja. Sasa ghorofa ni nyumba ya kimila? Siyo nyumba ya kimila!

Mheshimiwa Spika, sasa unapojenga nyumba za kudumu, kwanza wale watu upande mwingine tumewatia umasikini, kwa sababu mle ndani ya hifadhi mtu hamilikishwi ardhi, siyo yake. Sasa kwa nini Wizara isiweke utaratibu mzuri kuwatafutia eneo zuri wale wafugaji na kuwamilikisha? Wapeni hati ili siku nyingine msije mkawafukuza huko watakapoenda. Wapeni hati za kumiliki ardhi yao pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wapewe hati ili siku nyingine wasije kufukuzwa hapo watakapokwenda, wapewe hati za kumiliki ardhi yao pale na huu utaratibu wa kusema kuna watu maskini wamepewa mifugo, sio tu wa kabila la Kimasai, hata sisi Wagogo na makabila mengi ya Wasukuma. Sisi tunaita Ng’ozwa, mtu anakuwa hana kitu anapelekewa ng’ombe 200, yeye pale anafaidi maziwa kidogo, lakini anakula nyama mpaka ng’ombe afe, sio kwamba achinje hapana, mpaka afe na ngozi anakuwekea tajiri.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Ukija tajiri anakuja kukuonyesha ng’ombe wako fulani alikufa, hao ndio wanaishi mle. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Munde Tambwe Abdallah.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nimpe mwongeaji taarifa kwamba, amesema wale watu Serikali inaweza kuwajengea nyumba sehemu nyingine na kuwahamisha. Nakubaliana naye kwa kumpa taarifa kwamba, wale watu wanatumia shilingi bilioni tatu kwa mwaka kwa ajili ya chakula.

Kwa hiyo, fedha hizo zikienda kujenga nyumba zao wakamilikishwa ardhi, wakajengewa shule hospitali na kadhalika, inawezekana. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Kweli.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, hilo nimelipokea na ndio maana nilitaka nijenge hoja yangu… (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Lusinde subiri kidogo. Naona unafanya haraka sana, lazima nikuite tena ndio uzungumze. Mheshimiwa Lusinde.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana tuna Spika wa viwango. Hebu mpigieni makofi Spika haraka sana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ndio maana nilitaka nijenge hoja yangu hivi katika nchi nzima ambayo watu wote sisi tunaishi kwa usawa, leo unakuwa na Tarafa moja ambayo ukifuga humo ndani ya hiyo Tarafa hao wote wanaoishi humo watanunuliwa chakula bure. Hao watu wanaoishi humo madawa ya mifugo yote watapata bure, hao watu wanaoishi humo watoto wao watasomeshwa mpaka Chuo Kikuu bure. Nani atakataa kwenda kuishi kwenye hiyo Tarafa? Sisi wenyewe tuna mpango hapa wa kuhamia huko. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, maana yake kuzuri kuna kila kitu ambacho unapewa bure. Kwa hiyo, nataka kusema hivi kama tumefuatilia mitandao na tumeona zile picha, kama za uongo Serikali wasimamie hili jambo ili kutenda haki. Mle ndani wameonekana mbwa kama yule mbwa wa Wema Sepetu anaitwa Nunu, wako kule Ngorongoro, wako. Kuna mbwa German Shepherd wako mle Ngorongoro. Sasa tunajiuliza hivi mbwa kama yule atakaaje na wanyama wa kawaida? Ndio maana wanyama wanakimbia wanawaacha watu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nikwambie kengele ile ya kufunga ng’ombe shingoni ile sisi tunaita chidodolo kwa sisi Wagogo. Ile kengele ikilia paaaa mara moja hivi, faru anakwenda kusimama Morogoro speed yake. Sasa niambie huyo faru atarudi saa ngapi mpaka mtalii aje amwone? Kwa hiyo, ndugu zangu tukubaliane kwamba haiwezekani, kwa hali tuliyonayo sasa kuchanganya kati ya watu pamoja na hifadhi kuishi mule ndani haiwezekani. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ukitaka upime kwamba utajiri sasa unaanza kutuondolea utu. Tumepata taarifa mle kuna vijana watatu wameliwa na simba na picha zao zimeonyeshwa. Umeona hata mtu mmoja hata Mbunge wa eneo hilo au wahusika wa eneo hilo wametoa hata pole? Jamani maisha gani haya, haya ni maisha gani? Nataka niwape pole familia ambazo kwa namna moja au nyingine wamewahi kudhurika na wanyama. Tuwape pole wenzetu ambao wamepoteza watoto wao kwa nyakati fulani kwa kuliwa na simba. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hatuwezi tukaishi maisha hayo yaani mali inatuondolea hata utu wa kushindwa kuthamini kwamba wenzetu wanaishi mule wengine wanajeruhiwa. Haiwezekani, vinginevyo watuambie kwamba ule ni uongo na wachukuliwe hatua. Hata hivyo, kama unaweza ukafuga mbwa mle hatari kabisa, mbwa wakubwa kama wale, niwaombe matajiri wachache ambao wananufaika na ile mifugo na Serikali twende tukafanye sensa. Serikali ikitaka ku- prove hilo wafanye sensa, wale kondoo wamewekwa mpaka bei. Kondoo mmoja anauzwa Shilingi laki tano halafu mimi nibaki masikini, nani kakudanganya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni wazi huyo kondoo sio wake. Kwa hiyo, watu wanafuga kondoo wakubwa mle kwa sababu huduma zote ni za bure, halafu wanakwenda kuuza wanapata fedha wananunua VX, yule mchungaji yuko mule anabaki na umasikini wake. Asikudanganye mtu zile familia za wale wanaochunga haziwezi kusoma, kwa sababu baba hachungi kila siku, siku ya pili anaachia watoto. Wanaacha kwenda shule anasema mkafanye kazi ya tajiri, ndio wale watoto ambao tunaona picha zao zinarushwa kwenye mitandao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka ni-conclude, sio kwamba naunganisha kama Waziri, lakini nataka niseme hivi, naunga mkono hoja hii. Serikali naomba niwashauri wale watu watafute namna ya kuwaondoa mle kwa namna mbili; wanaotaka kuondoka kihiari waondoke kihiari kuanzia sasa. Wakajipange waorodhoshe watu wanaotaka kuhama, wahame, wwaape kifuta jasho chao, watafute eneo la kuwapeleka. Wanaotaka kuondoka kwa sheria, Serikali ilete sheria tubadilishe waondoke kwa sheria. Yote hayo mawili yafanyike, (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba yote mawili yafanyike; anayetaka kuhama kwa hiari ahame kwa hiari, anayetaka kuhama kwa sheria, sheria sio msahafu, iletwe hapa tuibadili, sisi ndio watunga sheria, aondoke kisheria. Yote hayo yanawezekana nchi si ya kwetu jamani? Wataondoka kwa sheria, kama kuna mafao walipwe waende na huko wanakokwenda wapewe hati za kumiliki ardhi. Tusiwapeleke tena kwenye eneo la kuwapangisha. Maisha yao yakishaanza kuwa mazuri tutasema tena hapo hameni hapana. Tuwatengenezee structure nzuri ya shule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2018 wote kulikuwa na kipindupindu kwa mwaka mzima hakikuondoka. Leo hii tunashindwa kuhurumia hawa watu jamani? Mtu anawezaje kukaa na kipindupindu kwa mwaka mzima watu wangapi wamepotea pale? Watu wangapi wamedhurika pale? Lazima tuangalie maisha ya watu. Pia mle ndani kuna minada, jana nimeona kwenye gazeti limeandika. Kuna minada miwili kila wiki, minada unajua inavyokusanya watu wengi, magari mengi, sasa mnyama gani atastahimili hiyo hali jamani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono Serikali Waziri alete hapa habari wanaohama kwa hiari waorodheshwe, wahamishwe, Serikali ikafanye sensa. Kila mtu asimame na mifugo yake utashangaa hali za wale watu na mifugo wanayomiliki pale. Hapo ndio tutajua akina nani wanafugia pale na inawezekana, hata wale wanaochunga ile mifugo hawalipwi hata fedha. Anaambiwa kunywa maziwa tu, ng’ombe hizi ni za bwana mkubwa. Hii haiwezekani katika nchi yetu, mtu unaishi unawafanya wenzako kama watumwa, katika nchi ambayo tumedai uhuru na tumepigania uhuru wa nchi hii. Hilo jambo haliwezekani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niiombe Serikali ije na tamko rasmi wanaohama waanze kuhama mara moja sio suala la kuchelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea kuishauri Serikali ifanye mambo mawili. Ilete hapa orodha ya wananchi wanaotaka kuhama kwa hiari, iwasaidie kuhama. Wasije kuwa wanatishwa, wengine wanakaa mule kwa nguvu kwa sababu, kuna mabwana wakubwa wana mabavu wanawatishia. Wanaotaka kuhama kwa hiari Serikali iweke wazi orodha yao na waondoke eneo lile. Wanaotaka kuhama kwa mujibu wa sheria Serikali ilete sheria tubadilishe, wahame kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)