Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021

Hon. Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala kwa kutujalia uzima, salama na afya njema.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru pia wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii ya kutoa mchango wangu katika ripoti hizi mbili muhimu za Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii pamoja na ile ya wenzetu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Spika, pia nitumie nafasi hii kuwapongeza wenzetu wa Maliasili, Waziri, pamoja na Ardhi, Mawaziri pamoja na timu zao. Kwa kweli wamefanya kazi nzuri katika kipindi hiki cha utekelezaji wa kipindi cha miezi sita na tunaona matokeo chanya katika sekta zetu zote hizi za ardhi pamoja na maliasili.

Mheshimiwa Spika, la kwanza ni ombi langu kwa Wizara ya Fedha; sekta hizi tumezipelekea fedha kidogo. Maliasili kidogo wao wana afadhali, lakini sekta ya ardhi bado hali haijaridhisha, kwa hiyo tunaweza tukawalaumu utekelezaji siyo mzuri, lakini sababu kubwa ni kwamba kiwango cha fedha ambazo tunawapelekea hawa wenzetu hakiwezi kukidhi utekelezaji wa shughuli ambazo tumewapangia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo namwomba sana Waziri wa Fedha ajitahidi kwa sababu tuna malengo tumeyapanga katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, tuweze kuyafikia katika miaka mitano na nyota njema huonekana asubuhi. Mpaka hivi sasa bado haionekani kwamba kuna uwezekano mzuri wa kuweza kuyafikia haya kama hatutaweza kuzipatia hizi sekta fedha za kutosha.

Mheshimiwa Spika, nami niungane na wenzangu na napenda kumfuata kaka yangu, ndugu yangu, Mheshimiwa Omar King. Kuna maneno ya maandishi yanazungumza “idha dhwaharal-bidaa washarus-swahaba famankanalahul-ilma falyudh-har. Wamankudhwiat alayhi laanatu-llah” kwamba unapodhihiri ufisadi au uzushi na kubughudhiwa au kutukanwa kwa wanazuoni, basi wale ambao wana utaalam wanatakiwa waudhihirishe na watakaoficha basi laana ya Mwenyezi Mungu inatakiwa iwaandame. Sasa mimi binafsi sitaki laana ya Mwenyezi Mungu ije iniandame kwa sababu tayari nina ujuzi katika haya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo suala la Ngorongoro nafikiria tatizo kubwa kwamba tumewaacha wataalam wetu na sasa tunaongozwa na vichwa vyetu. Kwa sababu wataalam toka mwaka 1959 wamefanya tafiti za kutosha za kutupa dira ya kufanya maamuzi sahihi vipi tutalifikia hili suala, lakini matokeo yake vitabu tumeviweka pembeni na tunaongozwa na hisia na vichwa vyetu. Kwa hiyo kama walivyozungumza wenzangu kwa kweli tunakwenda kuipoteza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kama hatutachukua hatua sahihi hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika masuala ya uhifadhi, suala la muda ni suala muhimu sana. kama muda ukiuacha, nakumbuka kuna Profesa mmoja, Profesa Kajembe, alifanya utafiti kule Duru-Haitemba katika kuwashirikisha wanajamii katika kuhifadhi msitu. Wananchi wale walikabidhiwa msitu katika kipindi cha mwaka mmoja walienda msitu ukawa umepotea wote umekwisha. Nafikiri wale ambao ni wenyeji wa Duru-Haitemba wananisikia hapa watakuwa wanafahamu kule Babati ukweli jinsi ulivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo na sisi katika hali halisi ya Mamlaka ya Ngorongoro kama hatutachukua hatua hivi sasa basi tujiandae Tanzania kwenda kupoteza urithi wa dunia. Kwa sababu kila sababu zinaonekana kama tulikuwa watu 8,000 sasa hivi tupo zaidi ya 120,000; tulikuwa na ng’ombe 12,000, sasa hivi kuna ng’ombe zaidi ya 800,000. Hapa projection ya ndani ya miaka 20 hadi 40 inayokuja unaitegemea itakuwaje; tutakuwa na ng’ombe zaidi ya bilioni moja na kuendelea, tutakuwa na watu zaidi ya 300,000 hadi 500,000. Kwa hiyo naomba tu, muda wa maamuzi ni sasa, lazima tuchukue hatua.

Mheshimiwa Spika, katika uhifadhi huuhuu ambao tunauzungumza ndani ya Ngorongoro tulikwenda tukapoteza faru mpaka wakabakia faru watano. Jitihada zimefanyika sasa hivi tumeweza kurejesha faru angalau idadi inatia matumaini.

Mheshimiwa Spika, sambamba na suala la Mamlaka ya Ngorongoro, kuna hali ambayo inafanana na hiyo ya Bonde la Kilombero. Bonde la Kilombero nako hali siyo salama kwa sababu tumeshaweka fedha, trilioni sita pale na hizi fedha kama hatukwenda kulishughulikia Bonde la Kilombero nako hatari inatunyemelea.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu maji ambayo yanatoka katika Mto Kilombero ni asilimia 60 mpaka 65. Kuna vijiji kama Kijiji cha Ngombo; kuna vitongoji karibu vinane katika Wilaya ya Malinyi; kuna vitongoji vitatu katika Wilaya ya Ulanga na kuna kitongoji kimoja katika Wilaya ya Kilombero kutokana na data za wataalam wetu vinatakiwa viondoke. Kama tukichelewa kuviondosha hivi, basi tusitegemee Mradi wa Stiegler’s Gorge wala tusitegemee Mradi wa SGR kwa sababu hii miradi miwili inategemeana.

Mheshimiwa Spika, mwisho, nimalizie tu kwa kuwapa pongezi wenzetu wa maliasili hasa TAWIRI kwa kuweza kufanya ile International Conference ambayo ilikuwa ikifana vizuri na ninampongeza sana Mkurugenzi wa TAWIRI na Mkurugenzi wa Wanyamapori pamoja na Waziri. Namwomba Profesa Mkenda tuwahamasishe vijana wetu wa Vyuo Vikuu, basi waweze kuhudhuria katika makongamano hayo kwa sababu yana tija kubwa na yataweza kuwasaidia Watanzania kuweza kukuza vipaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Ahsante. (Makofi)