Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021

Hon. Muharami Shabani Mkenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kutumia nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hoja iliyo mbele yet una nitajikita zaidi kwenye upande wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kutumia nafasi hii, kwa niaba ya wananchi wa Bagamoyo, kukupongeza kwa kuchaguliwa kuwa Spika wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia napenda kumpongeza Mwenyekiti wetu, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, ambaye anatarajiwa kuwa Naibu Spika saa chache zijazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kwanza nizungumze kuhusu suala la mahusiano yetu ya Tanzania na nchi za nje. Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kuikuza diplomasia ya Tanzania nje ya mipaka yetu. Mama Samia anafanya kazi kubwa sana. Kwa kipindi kifupi toka ameingia madarakani amefungua milango mingi ya mahusiano ya kimataifa katika nchi yetu; tunampongeza sana kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama unavyotambua katika Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuna vyombo vingi ambavyo vinahusiana na Kamati hii, lakini nizungumze moja kuhusu suala la NIDA. Wananchi wa Tanzania kwa miaka mingi sana walikuwa wakisumbuka katika kupata vitambulisho vyao vya Taifa, lakini leo hii tunakoelekea baada ya Mheshimiwa Rais, mama Samia Suluhu Hassan kuchagua viongozi wapya katika taasisi hii mwelekeo wa upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa unaelekea kuwa mzuri katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, siku zilizopita Serikali ilikuwa ikisumbuka sana na suala hili. Mashine zililetwa, mitambo ililetwa lakini kwa bahati mbaya kazi iliyokuwa ikifanyika haikuridhisha Watanzania wengi; idadi kubwa ya watu wamesajiliwa lakini hawajapata vitambulisho vya Taifa. Leo hii Kamati imejiridhisha kwamba kazi inayokwenda kufanyika kwa ajili ya upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa ni kazi ambayo itakuwa yenye kutukuka. Tunawapongeza sana viongozi wa NIDA kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea nayo mpaka sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo nataka kulizungumzia hapa ni suala la mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Jumuiya ya SADC. Jumuiya hizi zimekuwa na faida kubwa kwetu sisi Watanzania na hasa baada ya Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan, kufanya ziara katika baadhi ya Nchi za Afrika Mashariki na kugundua fursa mbalimbali ambazo tunafaidika nazo hii leo kutokana na uwepo wa jumuiya hii.

Mheshimiwa Spika, katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ni mambo mengi sana ambayo yanafanyika na hasa fursa zilizopo za kibiashara. Ni wajibu wa Serikali sasa hivi kuhakikisha kwamba fursa zilizopo za kibiashara wanaziweka wazi ili wananchi waweze kuzitambua na kuweza kukimbizana nazo ili waweze kuiletea nchi yetu maendeleo.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kuwa Tanzania tuna matajiri wengi, tuna wafanyabiashara wengi, lakini bado mpaka leo hawajapata taarifa rasmi za fursa zilizopo. Kwa hiyo ni jukumu sasa hivi la Wizara zinazohusika pamoja na Serikali kuzitangaza fursa hizi ili wafanyabiashara wetu waweze kuziendea na kuhakikisha kwamba Taifa letu linapata mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Spika, katika mtangamano wa SADC faida nyingi zinapatikana. Niipongeze Bohari yetu Kuu ya Dawa (MSD) kwa kupata tenda ya kuweza ku-supply dawa katika Nchi za SADC. Hii ni hatua kubwa sana ambayo Tanzania imeifikia. Tuna nchi nyingi za SADC lakini Tanzania imeteuliwa MSD kusambaza dawa pamoja na vifaatiba katika nchi hizo; hiyo ni hatua kubwa sana ya kimaendeleo katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa napenda nipongeze Jeshi letu, Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Pamoja na kulinda mipaka, Jeshi lina shughuli nyingi ambazo wanazifanya ili kuiletea maendeleo nchi yetu. Ukiachilia mbali ulindaji wa mipaka, Jeshi linashughulika na shughuli mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze kwa kuendesha Kiwanda cha Nyumbu ambacho kinaendesha teknolojia ya kutengeneza magari. Nafikiri kwa siku zijazo Tanzania itakuwa ni nchi moja wapo ambayo itakuwa inashughulika na mambo mengi sana ya kujitegemea na hasa katika uundwaji wa magari.

Mheshimiwa Spika, pia niwapongeze sana Jeshi letu katika suala zima la kilimo na hasa JKT, wanajihusisha sana katika kilimo na hiki kilimo kwa siku zijazo wataisaidia sana nchi yetu katika usalama wa chakula; niwapongeze sana kwa jambo hili.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)