Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia. Nitumie sekunde chache sana kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan. Kwa kuridhia na kutoa leseni ya kuchimba madini ya Nickel yaliyoko kwenye Jimbo la Ngara. Wananchi wa Ngara wana imani kubwa sana na Mheshimiwa Rais, wanampenda; na siku akitua Ngara tutayabeba yale magari ya msafara anayokuja nayo Rais. Kwa kweli tunamshukuru sana Rais kwa kuweza kutoa leseni hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze kwenye mchango wangu na niende moja kwa moja kwenye mgongano wa masilahi. Wakati tunafanya uchambuzi, tuliletewa sheria kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) na kwenye sheria ile Kifungu cha 32(2) kinaruhusu Maafisa wa Serikali na wale waliopo kwenye ofisi hiyo ya Makamu wa Rais, (Mazingira) kuweza kushiriki kwenye zabuni za kufanya tathmini ya masuala ya mazingira (environmental impact assessment) pamoja na audit.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutafakari na kuichambua kwa umakini ile sheria tuliyoletewa, tuligundua kwamba Mkurugenzi wa Taasisi ya Serikali ambaye ameajiriwa kama mtaalam wa kutoa huduma za mazingira, ana uwezo wa kushiriki kwenye zabuni, na kitakachotokea ni mambo yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mkurugenzi wa Kampuni hiyo hiyo ama Taasisi ya Serikali imetangaza zabuni, halafu naye akaomba tender, halafu Mwenyekiti wa Kamati ya Manunuzi akamnyima tender bosi wake, kitakachotokea pale ni kwamba yule mtu atapangiwa kazi ya kufagia, consequence ya kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kama huyu mtumishi wa Serikali ameshiriki naye kuomba tender ambayo imetangazwa na Serikali, kitakachotokea pale, quality ya ile kazi inaweza kuwa jeopardized. Kwa sababu, kwa mujibu wa Sheria ile ya Mazingira, wataalam hawa wa Serikali wanaofanya EIA, wanatakiwa kwenda kuhakiki taarifa iliyoandikwa na mtu aliyepewa kazi ya kwenda kufanya EIA. Sasa kama tuna sheria inawaruhusu nao kwenda ku-compete na kuomba kazi hizo, hawawezi kusimamia vizuri kule wakati nao wanatakiwa kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitafakari sana eneo hili tukagundua kwamba wataalam hawa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira walioweka Kanuni hii, waliongozwa na uroho na ndiyo maana wakaweka Kanuni inayowa-favour wao wenyewe ili waweze kuomba kazi wanazozitangaza wao wenyewe na waweze kuzifanya wao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba wewe na Serikali, kazi hizi tuwaachie private sector na twende tukafanye marekebisho ya kipengele hiki kuhakikisha kwamba tunaondoa kabisa mgongano wa masilahi kwenye shughuli zote zinazohusiana na masuala ya environmental impact assessment pamoja na environmental audit.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunafanya uchambuzi, Mezani kwetu ilitua Sheria Ndogo kutoka Halmashauri ya Bumbuli. Sheria hii inahusu ada na ushuru mbalimbali wa mazao kwenye Halmashauri ya Bumbuli. Kanuni ya 9(8) inasema mtu yeyote haruhusiwi kubeba ama kununua mazao kama hana kibali na risiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliitafakari sana hii sheria, tukagundua kwamba sisi Watanzania muda wote hatuna mahitaji ya kutosha. Ukiamua kununua kilo mbili za karanga, unakwenda dukani unachukua karanga zako unarudi nyumbani. Sasa Maafisa wa Serikali hasa wa Halmashauri wana uwezo wa kutumia vibaya vifungu hivi vya sheria na kuanza kuumiza wananchi. Katika hali ya kawaida, hakuna mwananchi anayeweza kupata kibali kwenda kununua mazao gunia moja, debe mbili au debe tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba kwa unyenyekevu mkubwa, Kanuni hii ifutwe kabisa, isipite kwa sababu Kanuni hizi tunapozipitisha ndizo zinakwenda kuleta kero kwa wananchi na matokeo yake wananchi wanaichukia Serikali yao, wanachukia viongozi wao kwa sababu ya hizi sheria tunazozipitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye Sheria ya Kudhibiti Ombaomba ambayo wenzangu wameshaisema kidogo. Nami nijielekeze kwenye concept inaitwa anthropology. Huu ni utaratibu wa kusaidiana kama binadamu. Dunia nzima ombaomba wapo, sema wenzetu wame-advance na kuita Homeless, American Beggars, Tanzanian beggars, all are beggars. Halmashauri ya Wilaya ya Chunya wametengeneza Sheria ya Kudhibiti Ombaomba kabisa. Tena wameenda mbali, Mkurugenzi amkamate ombaomba ampeleke kwa RAS. Sasa tukajiuliza RAS ana utaratibu wa kupokea ombaomba? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli hawa watu ni ombaomba au ni watu wenye uhitaji? Ifike mahali kama nchi tubadilishe baadhi ya terminology ambazo ndani yake zinaleta ambiguity. Kunaweza kukawa na tafsiri hasi kwenye baadhi ya maneno tunayoyatumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuomba Wizara husika ikiwezekana wapige marufuku kabisa hili neno ombaomba na badala yake tubadilishe tuseme ni watu wenye uhitaji. Kwa sababu watu hawa badala ya kusaidiwa, sisi tunaona ni ombaomba, sasa tunatunga sheria tuwakamate tuwarudishe walikotoka. Sheria hii ni ya kibaguzi na tunaomba isipite kabisa kwa sababu madhara yake ni kufanya wananchi waichukie Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wameshazungumza mambo mengi tuliyokutana nayo wakati tunachambua hizi sheria ndogo ndogo. Nikuhakikishie kwamba sheria inapotua kwenye Kamati yetu, tunaichambua neno kwa neno, mstari kwa mstari na tunakwenda mbali kuchambua maana halisi iliyopo kwenye vifungu vile tulivyoletewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria nyingi tulizozipokea kama ambavyo nimekuonyesha hapo, zina vipengele vya ovyo ovyo ambavyo vinaweza kutuchonganisha na wananchi na kufanya wananchi waweze kuichukia Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kabisa Bunge lako Tukufu lisipitishe maeneo yote tuliyokwishaonesha kwamba vifungu hivi havifai, vitafanya wananchi waichukie Serikali. Lengo la sheria hizi ni kuchochea maendeleo na siyo kukusanya ushuru tu hata kama wananchi wana hali mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)