Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. January Yusuf Makamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii. Kwa kuwa nazungumza kwa mara ya kwanza tangu nipate heshima ya kushika nafasi hii, napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini katika nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakushukuru wewe kwa uongozi na ushauri wako katika kipindi hiki cha siku takribani 58 ambazo nimekuwa katika nafasi hii. Nakushukuru sana na naishukuru Kamati yako vile vile kwa miongozo mbalimbali na ushauri mbalimbali ambao umefanya mpaka tumeweza kufika hapa siku ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge kadhaa wamechangia katika Mpango kuhusu mambo yanayohusu sekta ya nishati. Kabla sijajibu, naomba nimpongeze Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na timu yake kwa kazi nzuri ya maandalizi ya Mpango ambao ni mzuri, unaotoa dira, pamoja na uwasilishaji na michango mizuri iliyotoka kwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo matatu ambayo ningependa kuyazungumzia ambayo yalichangiwa na Wabunge kwenye Wizara yetu. La kwanza kubwa ni suala REA. Tunaelewa kwamba usambazaji umeme vijijini ni jambo kubwa, ni jambo ambalo linagusa maisha ya Watanzania wengi, karibu Wabunge wote wana hoja na maswali kuhusu umeme katika maeneo yao. Sisi katika Serikali tunatambua umuhimu wa jambo hilo, sasa tumejipanga upya kuhusu utaratibu bora zaidi; wa kwanza, kuwapa taarfia Waheshimiwa Wabunge kuhusu miradi iliyopo katika maeneo yao; pili, kutengeneza na kutafuta rasilimali kwa maeneo ambayo bado hayajapata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na changamoto kubwa sana ya takwimu ikiwemo classification ya wapi ni kijijini? Wapi siyo kijijini? Kwa hiyo, changamoto imetusabaishia tuwe na namba tofauti kuhusu idadi ya vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho tumeamua na kwa ridhaa yako, naomba rasmi kwamba katika Bunge la mwezi wa Pili, tutawaita Wakandarasi wote hapa Bungeni, tutakuwa na maonesho ya siku tatu kule nyuma, kila Mkandarasi wa kila Mkoa atakuwa na meza; na sisi wote tutahamia hapa ikiwemo ofisi nzima ya REA pamoja na Wizara; tutafanya semina kuhusu suala hili na kuhusu mpango wetu mpya.

Waheshimiwa Wabunge maswali yao yote yatajibiwa hapo hapo kuhusu kule ambako umeme haujaenda, umechelewa, unasuasua na unatarajiwa kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuanaamini kwamba tukilifanya hili jambo kwa wakati mmoja, hata tukikaa hapa wiki nzima kujibu maswali, kero na maoni na ushauri wa Wabunge kuhusu program hii mpya ambayo tunakuja nayo, basi itasaidia kama namna bora zaidi ya kubadilishana taarifa kati yetu sisi na Wabunge, lakini pia itatusaidia zaidi katika kukusanya takwimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi atunafahamu kwamba umeme hautumiki na Kijiji, umeme unaatumika na watu. Kwa hiyo, takwimu za kijiji ni nzuri zinatupa milestone kwamba tume-cover maeneo ya kiasi fulani; lakini mtu ambaye hajapata umeme nyumbani kwake na haujamfikia, takwimu kwamba umefika kijijini kwake, siyo takwimu ya maana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaelewa na mwelekeo mpya ni kupima nyumba zinazohitaji umeme na ambazo hazijapata umeme. Huko ndiko tunakokuja. Tunafahamu kwamba tuna idadi ya vitongoji hapa nchi 64,000; vitongoji vilivyopata umeme ni 27,000 tu na vitongoji zaidi ya 37,000 na kadhaa huko havijapata umeme. Kwa hiyo, tunakuja na mradi mkubwa zaidi ambao bahati nzuri wenzetu huko nyuma walishaanza nao kuuzungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba mahitaji ya rasilimali ni makubwa, ili vitongoji vyote 37,000 vipate umeme, tunahutaji shilingi trilioni 8. Tunafahamu kwamba haziwezi kupatikana kwa wakati mmoja, lakini support ya Bunge hili ni muhimu sana ili tuweze kupeleka umeme kila mahali.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, naomba atukutane mwezi wa Pili, tutakuwa na semina na maonesho ya muda mrefu. Kila Mbunge atajibuwa maswali yake yote kuhusu umeme katika maeneo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine lililozungumziwa ni kuunganisha mikoa iliyobaki kwa gridi. Plans zipo, mipango ipo na tumeielezea; Mkoa wa Rukwa, Kigoma, maeneo ya Mkoa wa Kagera pamoja na Mkoa wa Katavi. Tunaamini kwamba mpaka mwaka 2024 mikoa yote itakuwa imeunganishwa kwenye gridi ya Taifa kwa miradi tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa la mwisho nizungumze hili kubwa lililozungumzwa na Mheshimiwa Ester Bulaya la mradi wa Julius Nyerere. Sasa sisi tulipata barua ya tarehe 3 Septemba,kutoka Ofisi ya Bunge kwamba, Kamati ingependa kupata taarifa ya tulipofikia. Tulileta taarifa hiyo ipo kwenye mtandao wa Wajumbe wa Kamati na naamini Mheshimiwa Bulaya amepata taarifa hizo huko. Kwa hiyo, ni kweli kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani iliupokea mradi huu ukiwa umechelewa kwa siku 477.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tumefikia wapi kwa kila kipengele cha mradi kwa asilimia, hazina maana sana kwa sababu zinabadilika kila siku. Hata siku ya leo kuna kazi inafanyika, maana yeke ni kwamba, nikikupa asilimia leo, wiki ijayo zitakuwa ziko tofauti. Ni kweli mradi una changamoto ambazo alipokuja Mheshimiwa Makamu wa Rais kuutembelea alizieleza na sisi tulipokutana na Kamati ya Bunge pia tulizieleza. Ni changamoto za kawaida kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya namna hii. Changamoto hizi hazifanyi mradi huu uonekane hauna maana. Changamoto hizi haziwezi kuturudisha nyuma wala kutuondoa katika nia ya kuutekeleza mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naambiwa kuna airport kubwa kule Ujerumani imechelewa miaka, akataja miradi mikubwa ya kimkakati katika nchi zilizoendelea ambayo imechelewa. Kuchelewa kwa mradi ni jambo la kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali tumechukua hatua pale ambapo kulikuwa na uzembe hatua zimechukuliwa kwa upande wa TANESCO na Wizarani, hizo ni changamoto za upande wetu. Kwa upande wa mkandarasi, mkataba baina yetu na mkandarasi unayo tiba kuhusu changamoto za ucheleweshaji na sisi tunafuata tiba hiyo. Tumeanza vikao na mkandarasi kuhusu namna ya kumaliza changamoto zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme tu kwamba, mazungumzo yanaendelea kati yetu na mkandarasi ambayo yana misingi minne. Kwanza ni kupunguza hizi siku za ucheleweshaji kutoka 477 zilizopo sasa na kujaribu kuona kama tunaweza tuka-squeeze tukaharakisha baadhi ya maeneo zikawa chache zaidi. Msingi wa pili, ni kuzuia kusiwe na ucheleweshaji zaidi. Msingi wa tatu, kazi ifanyike kwa ubora na viwango vinavyotarajiwa na msingi wa nne, kusiwe na ongezeko la gharama kwa upande wa Serikali. Kwa hiyo, mazungumzo yetu na mkandarasi yako katika misingi hiyo minne. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nirudie kwamba, kauli aliyotoa Mheshimiwa Rais hapa Bungeni kwamba, miradi yote hii mikubwa ya kimkakati lazima itakamilika na lazima itatekelezwa. Naomba kuchelewa kwa mradi kwa siku 477, naomba nirudie kusionekane kwamba, ni tatizo litakalouua mradi huu. Sisi tumejipanga vizuri sana kuhakikisha kwamba, tunautekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe ambayo inazungumzwa sana ni tarehe inayokaribia ya kujaza maji kwenye bwawa. Kwa sababu, ilizungumzwa hapa Bungeni na nimeona clip inazungumza, ngoja nilitolee ufafanuzi kwamba, ilisemekana kwamba, tarehe 15 Novemba, basi maji yataanza kujazwa kwenye bwawa lile. Si ajabu kwa kadiri siku hii inavyokaribia itakuwa ni habari kubwa ambayo inaweza kutumika kuuchafua mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, tarehe hiyo itapita kabla hatujajaza maji na sababu ni mbili. Ili ujaze maji kwenye bwawa lazima masharti mawili yatimie; lazima uwe umejenga tuta kuu ambalo ni main dam, ule ukuta mkuu wa kuzuia maji kwa mita 95 juu ya usawa wa bahari, lile tuta linapaswa kuwa na mita 190 juu ya usawa wa bahari. Sasa ili uanze kujaza maji lazima uwe umefikia mita 95. Mpaka leo bahati nzuri tumeshapita mita hizo 95 juu ya usawa wa bahari kwa hiyo, sharti la kwanza la kujaza maji tumelifikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sharti la pili, ni kwamba, wakati tunajenga hili tuta kuu tulijenga njia ya kuchepusha mto pembeni, ili tupate nafasi ya kujenga. Sasa ili sasa ujaze maji lazima uzibe lile handaki ulilolijenga kuchepusha mto. Sasa ili uzibe lile handaki unahitajika milango mikubwa na vyuma takribani 14 na kila kimoja kina tani 26, ni machuma makubwa ya kuzuia lile handaki ili mto usiendelee kuchepuka wakati unajaza bwawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ile milango imefika, lakini inahitaji crane kuibeba na kuziba, ile crane lazima itoke nje na crane hiyo haijafika bado. Kwa hiyo, tumetimiza sharti la kwanza la kujaza maji, lakini sharti la pili la kutuwezesha kuziba ule mchepusho hatujalifikia. Kwa hiyo, kwa hali na mwenendo hatutaweza kujaza maji kwenye bwawa kabla ya mwezi wa Machi. Tutawapa tarehe mahususi ya kuweza kuanza kwa kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya nikiamini kwamba, sisi ni viongozi katika Bunge hili, mradi huu ni wakwetu, ni mradi wa kimkakati, kufanikiwa kwa mradi huu ni kufanikiwa kwa nchi. Kicheko au kejeli yoyote kwa kuchelewa kwa mradi huu haimsaidii mtu yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekwishatokea kwamba, katika project management yoyote na katika miradi mikubwa haya mambo hutokea. Kwa hiyo, imani yangu ni kwamba, sisi tutashirikiana na tutaomba ushirikiano wa Bunge lako kuhakikisha kwamba, malengo yaliyowekwa ya mradi huu yanatimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kulizungumzia hili. Sasa hatuko hapa kumlaumu mtu, kazi hii tumepewa sisi ambao tumeteuliwa na tutaifanya kwa nguvu, uwezo na maarifa yetu yote kuhakikisha kwamba unakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho la LNG; naomba niwahakikishie Watanzania kwamba, mradi huu mkubwa kabisa wa kimkakati wa jumla ya shilingi trilioni 70, jana tumetengeneza historia kwa kuanza mazungumzo na makampuni ya mafuta na gesi. Kwa hiyo, nchi yetu itaenda kupata manufaa makubwa sana katika miaka ijayo kwa kuvuna gesi yetu kwa matumizi ya kuuza nje, lakini pia kwa ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo, ndugu zangu wa Lindi na Kusini na Watanzania wote, tutapata nafasi ya kueleza fursa zitakazopatikana wakati wa utekelezaji na pia tutakuwa wawazi kuhusu mfumo wa mapato yatakayotokana na gesi hii na jinsi ambavyo nchi yetu na uchumi wetu utafaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisitumie muda mrefu. Nafahamu yako mengi, tutayazungumza kwa kadri siku zinavyokuja ikiwemo mabadiliko ya mfumo wa uuzaji na ununuzi wa mafuta nchini ili kuweza kutoa nafuu kwa watumiaji wa dizeli na petroli na mafuta ya taa nchini, hatua ambazo nadhani mmeanza kuziona. Mengi na mazuri yatakuja katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)